Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kusimama hapa leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuunga mkono hoja iliyopo mbele yetu ambayo ni hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa kweli imesheheni na imegusa maeneo yote, hususan kwenye maendeleo ya nchi yetu. Vile vile niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kipindi chake cha miaka mitano kuweza kutuingizia fedha nyingi za maendeleo katika Wilaya ya Nyang’wale zaidi ya shilingi bilioni 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kutekeleza yale yote ambayo yaliyoanzishwa na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, tunamuunga mkono kwa nguvu zote Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, tuko naye bega kwa bega na ninawaomba Watanzania waungane na wananchi wa Nyangh’wale kuwalaani wale ambao wanayaponda na kuyapuuza mazuri yalioanzishwa na Hayati Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia maeneo machache sana. Namwomba Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda mnisikilize vizuri. Kuna changamoto nyingi kwenye upande wa kodi na huwa nalizungumza kila mara, lakini hamlichukuli maanani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikilize vizuri. Nimeshauri mara nyingi sana tupanue wigo wa kukusanya kodi. Kuna maeneo mengi sana tunapoteza kodi na mnasema wale ni wafanyabiashara wadogo lakini wanapoteza mapato ya Serikali. Mfano, ukienda Chako ni Chako pale, ukiangalia yule mtu anauza kuku zaidi ya 300 kwa siku moja, lakini mtu huyo hatoi risiti. Hilo ni eneo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, nilishasema kwamba TRA na wafanyabiashara kuna usiri mkubwa. Kwa nini nasema hivyo? Leo hii wafanyabishara wenye maduka, ushahidi ninao, nimeamua kujilipua Mheshimiwa Waziri wa Fedha, naomba unilinde; baadhi ya maduka, katika maduka 10, matatu tu ndiyo yanayotoa risiti. Maduka saba hayatoi risiti na ushahidi ninao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimekwenda kwenye duka fulani Dar es Salaam muda wa saa saba mchana, nikanunua bidhaa zaidi ya shilingi 200,000/=, wamenifungia mzigo. Wakati nataka kuondoka nikawaambia nipeni risiti, wanadai kwamba hapa tangu asubuhi anayetoa risiti hayupo. Mauzo kiasi gani Serikali imepoteza fedha pale? Naomba lifanyieni kazi. Kama utataka ushahidi zaidi, niko tayari kuvaa kofia na kanzu iliyoisha, niende na kuonesha maeneo ambapo upotevu wa fedha za Serikali upo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa ushauri kwa upande huo.Hakikisha kwamba unawasajili wafanyabiashara wa kati ama wafanyabiashara wadogo, wagawie zile mashine ya EFD ili waweze kutoa risiti. Nakuomba Mheshimiwa Waziri achukue ushauri mwingine, punguzeni VAT kutoka kwenye asilimia 18 na iende mpaka 13 ili watu waweze kulipa VAT. Huo ni ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme jambo lingine. Walipa kodi wa nchi hii juzi nilisikia ni takribani milioni 3.9, lakini kuna walipa kodi zaidi ya milioni 3.9 ambao hamjawasajili na wapo, fanyeni utafiti wa kina. Hizi fedha mnazosema mnakusanya shilingi trilioni mbili kwa mwezi ni kidogo sana. Mimi ni mfanyabiashara, ni mchimbaji, ninaelewa. Tuliweza kulisaidia Taifa kwenye upande wa madini, tulitoa ushauri na leo hii Waziri wa Madini yuko pale, anazungumza kwa kutamba, yuko vizuri, Wizara yake inakusanya pesa vizuri. Nakuomba Mheshimiwa tuiteni wafanyabiashara tuweze kusema yaliyoko kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania hao wafanyabiashara hawana nia ya kukwepa kodi ila kuna matatizo upande wa TRA. Tunaomba mtuite tuje tutoe ushauri. Pia hatuwezi kusema yote hapa; siwezi kumwaga mchele kwenye ndege wengi, kwa sababu kuna mapapa wapo ambao wanapoteza mapato makubwa ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa TBS. Leo hii ukienda Dubai ukaleta mzigo unaozidi dola 5,000, TBS watakupiga faini ya asilimia 15, lakini kuna watu wale mapapa wanaingiza makontena na hawatozwi hiyo TBS. Leo hii mnaenda kuwakamua hao watu wadogo, watu wachache lakini kuna mapapa wapo. Mheshimiwa nitafute kwa wakati wako na unilinde nitakupa siri za wafanyabiashara ambao wanapoteza mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)