Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupatia uhai na hata sasa tunaendelea kuhudumu katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya bajeti iliyosheheni matumaini makubwa katika mwaka 2021/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwenye maeneo mawili; la kwanza kuhusu watumishi wa Idara ya Afya; kwa uzoefu na observations nyingi za Mkoa wa Lindi, vituo vingi vya afya vinahudumiwa na wahudumu wa afya yaani Medical Attendants. Sasa hii inaathiri utoaji wa huduma ya dharura ya uzazi yaani CEmONC na hiyo itaashiri kufikia malengo ya kupunguza vifo vya akinamama wakati wa ujauzito na kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mifano michache tu, najua wilaya zote zina shida hizo, lakini mfano Kituo cha Afya cha Nanjilinji, kimepata huduma nzuri za majengo na tunashukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, lakini watoa huduma ambao wana ujuzi hawapo. Kunapotokea dharura ya uzazi, mzazi huyo anakimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya jirani ambayo ni Ruangwa ambapo kuna kilomita 44 kutoka Nanjilinji, tofauti na kutoka Nanjilinji kwenda Hospitali ya Wilaya Kinyoga kule Kilwa ambayo kuna kilomita 174.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayotoka Nanjilinji kwenda Ruangwa nayo sio nzuri, ni barabara ya vumbi lakini pia inapita kwenye Mto Nakiu ambao hauna daraja, sasa masika kama haya ukijaa, hebu ona sasa hapo, mgonjwa yule ni mama anayehitaji kujifungua, anayehitaji operation ya kujifungua, lakini anashindwa kuvuka pale na ambulance unayo lakini kuna shida. Mkoa wa Lindi una shida sana una changamoto za huduma za afya, majengo tumepata tunashukuru na vifaa sehemu nyingine vipo, lakini watoa huduma ni wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia kwenye miundombinu, Mkoa wa Lindi kuna sehemu chache sana ile barabara kutoka Kibiti – Lindi – Masasi – Tunduru – Songea; ni hiyo tu ndiyo ya lami, lakini tunaomba ile barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea; Nanganga – Ruangwa; Ruangwa - Nachingwea, Nachingwea – Liwale; na Nangurukuru -Liwale, tunaomba ijengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto ya barabara za vijijini; natolea mfano kwa sasa ni masika, barabara zingine hazipitiki, mfano barabara ya kutoka Mipingo kwenda Mnyangara mpaka kule Namapwia ambako anatoka yule mjusi unayemsikia, sasa hivi hakupitiki kabisa. Pia kuna barabara ya kutoka Hoteli Tatu kwenda Pande na Lihimalyao kwenyewe ni changamoto kubwa. Pia kuna barabara inayotoka Somanga kwenda mpaka Kibata, nako ni changamoto; kwa ujumla barabara za vijijini Mkoa wa Lindi kuna changamoto kubwa. Jamani, tafadhali tunaomba mkoa ule uangaliwe kwa jicho la pekee ili kuwanusuru wananchi wale, ili nao angalau na wenyewe wachangie kwenye maendeleo ya nchi hii na wajisikie kwamba kwenye nchi yao ya kufaidi matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)