Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Mpango huu wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia suala la elimu; Elimu ya Msingi na Sekondari pamoja na Vyuo. Mwaka 2016 Serikali ilianza Mpango wa kusomesha watoto bure katika shule za msingi na sekondari kidato cha kwanza mpaka cha nne (O- Level). Mpango huu wa Serikali uliungwa mkono sana na ukafurahiwa na wananchi kila kona ya nchi hii. Watoto waliokuwa wanakwenda kuchunga ndege katika mashamba ya mpunga, wanachunga ng’ombe, wote walipelekwa madarasani. Sasa hivi ni mwaka 2021 watoto hawa ambao walianza kusoma elimu bure wanakadiriwa kufikia milioni mbili na mwaka kesho watafanya mtihani wa darasa la saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesema Serikali ina mpango wa kujenga shule 1,000 mpya za sekondari. Upungufu ninaouona kwa idadi hii kubwa ya wanafunzi takriban milioni mbili, hata kama wanafunzi hawa watafaulu kwa asilimia 80, inaonekana mpango huu wa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa madarasa kujenga shule 1,000 bado ni mdogo sana. Mimi napiga hizi hesabu naona hapa kuna upungufu wa karibu madarasa 103,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna madarasa 103,000, mnakuja na mpango wa kujenga shule 1,000 mpya, hawa watoto watasomea chini ya mti? Bahati mbaya sana watoto hawa ni wajukuu wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ndio aliyeleta Mpango huu wa kusoma bure; na watoto wameupokea wakaenda darasani na sasa hivi wanasoma siyo mchezo. Baadaye tutatengeneza tension kubwa sana ya nchi hapa. Mheshimiwa Waziri Mkuu ataanza kuzuia watu wasiende likizo na wapi, sasa hii ni hatari. Hili jambo inaonekana kama anaachiwa Waziri Mkuu peke yake, wakati hili ni janga la nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana mpango huu wa bajeti kwa haya madarasa 1,000 Wabunge muyakatae. Ninyi Wabunge shauri yenu mwaka kesho watoto watakuja kwenye majumba yenu, hakuna Mbunge atakayekuwa salama, hizi shule ni chache. Mheshimiwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Manaibu tafadhalini sana rudini mkaandae mpango mwingine mpya mjenao hapa vinginevyo hali itakuwa tete hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna kitu kibaya kama Waziri Mkuu bajeti yake watu wakang’ang’ania shilingi, hii itakuwa ni hatari sana katika nchi. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakuheshimu sana katika jambo hili, lakini wasaidizi wako ulionao naona wanataka kukutengezezea bomu haya madarasa ni madogo. Mimi kwangu tu kwenye Jimbo la Sengerema nahitaji shule mpya 30 na nchi hii ina majimbo karibu 200, itakuwaje? Hii ni hatari Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la walimu; walimu wa shule za msingi na sekondari katika nchi hii wako laki mbili na sitini na moja kama na mia mbili hamsini na tatu. Walimu wa shule za msingi wako laki moja na sabini na tano na amia nane, walimu wa sekondari wako elfu themanini na tano. Upungufu walimu elfu arobaini. Kwenye mpango ajira zinazoonekana hapa ni chache. Hawa wanafunzi 40,000 Serikali iliwekeza, imewasomesha hawa wanafunzi kwa pesa za mikopo, leo hawa walimu wako mitaani halafu ninyi mna upungufu wa walimu 40,000, hamtoi ajira. Mwaka kesho ni janga la kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani bajeti yetu hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu, msimfedheheshe Waziri Mkuu. Waziri wa Fedha, Waziri wa Kazi, Waziri wa Elimu liangalieni hili suala kwa sababu huko shuleni sisi ndio tunajua shule moja unakuta ina walimu 16 wanafunzi elfu moja na zaidi. Kwa mfano, kwangu Shule moja ya Msingi Mnadani wanafunzi wa darasa la sita ni 500, sasa kwa shule nilizonazo mimi tu peke yake kwa Sengerema Mjini wanafunzi watakaofanya mtihani ni zaidi ya wanafunzi 7,000 sasa hii si ni hatari, tutawapeleka wapi hawa wanafunzi?

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui bwana mwaka kesho itakuwaje. Kila atakayekuwa anaingia humu atakuwa anameza dawa za ugonjwa wa moyo, hatari itakuwepo kubwa sana mwaka kesho. Tunaiomba Serikali katika jambo hili ilitilie mkazo wa hali ya juu sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, hilo la ugonjwa wa moyo kila anayeingia humu ndani ni unabii au ni kitu gani?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, hali itakavyokuwa kwa sababu, nachotaka kukwambia sasa hivi bado tuna maboma kule. Kwa mfano, mimi nina ujenzi wa sekondari 15 ambazo hazijakamilika jana nilikuwa naangalia hii hesabu mimi mwenyewe nikawa naogopa, hawa nilionao sasa hivi elfu saba sijamaliza kuwapeleka sekondari, mwaka kesho kuna bomu lingine linakuja na mwaka huu bado wanakuja hawa watu, sasa najiuliza…

NAIBU SPIKA: Sawa, sasa kuhusu ugonjwa wa Wabunge, hilo hata wewe fanya mazoezi usijenao humu ndani. Wabunge hawa wa Mheshimiwa Spika Ndugai watarudi wazima kabisa humu ndani. (Makofi/Kicheko)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kukwambia mimi niko serious katika jambo hili. Mimi nafikiri huu mtaala wa ualimu muufute katika vyuo vikuu kwa sababu mnawapeleka watu wanakwenda kusomea ualimu, una upungufu wa walimu hamtaki kuajiri wako mtaani, inakuwaje? Mnafikiri hawa wazazi ambao watoto wao wamekwenda kusomea ualimu na wako nyumbani mnategemea nini? Hawa vijana wetu itakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu tunao, lakini katika huo upungufu tulionao wa walimu hamtaki kuajiri, mnakuja na ajira 6,000. Mimi nashindwa kuelewa jambo hili. Jamani twendeni mbele ya safari, lakini mjue kwamba tunakwenda kufanya kampeni 2025 na kampeni tuanze sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe kama hunisikilizi ananisikiliza Mheshimiwa Samia. Mheshimiwa Samia ndiyo atajua hawa 40,000 upungufu utakuwaje. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, hebu tuelewane kidogo, hebu kaa kidogo nikueleweshe.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii inakuwa hatari.

NAIBU SPIKA: Wewe changia hoja, hakuna mtu anayehitaji kutishwa, hayupo. Mara useme watu hawatarudi, mara watu watarudi na pressure, aah aah, wewe changia tu hoja yako umalize.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu umezilinda hizo maana tayari umeshanipotezea moja hiyo. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam inabidi nikupeleke darasani. Usiwe unabishana na Kiti. (Kicheko)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, sibishani.

NAIBU SPIKA: Eeh, usibishane. Na mimi pia sipangiwi muda wa kuzungumza humu ndani unayepangiwa ni wewe, malizia mchango wako.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa walimu elfu arobaini. Mheshimiwa Waziri Mkuu utaangalia katika bajeti yako uone namna gani tutafanya ili tuondoe hili tatizo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni maboma. Yako maboma yaliyojengwa kwa ajili ya madarasa, yako maboma yaliyojengwa kwa ajili ya nyumba za walimu, lakini yako maboma yaliyojengwa kwa ajili ya zahanati na yako maboma yaliyojengwa kwa ajili ya vituo vya afya. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba uunde kikosi kazi kipite nchi nzima, kitakuletea taarifa iliyo sahihi kwa sababu, kuna taarifa nyingine zinafichwa kwa ajili ya usalama wa hawa wakuu wetu walioko kule. Wanaogopa kusema maboma yaliyopo kwa sababu wanaonekana tayari pesa zinazokusanywa katika halmashauri zetu zinatumika vibaya. Maelekezo yako uliyokuwa unayatoa kwa ajili ya hizi Halmashauri zetu kutenga fedha, hazina mapato ya kutenga fedha kumaliza maboma haya ni lazima Serikali isaidie mpango huu wa haya maboma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine tulilonalo sisi kule ni la vyuo hivi vya VETA pamoja na maendeleo ya jamii. Hivi vyuo naombeni vitumike vizuri kwa sababu uwekezaji uliotumika hapa; kwa hii miaka sita tumewekeza shilingi trilioni moja na milioni mia sita na hamsini, kila mwezi tunawekeza katika elimu shilingi bilioni 23. Sasa hizi shilingi bilioni 23 kwa miaka yote hii mpaka sasa hivi leo ni miezi 72 sawa na shilingi trilioni moja na milioni mia sita, halafu baadaye hawa wanafunzi wakishindwa kufaulu wanarudi nyumbani. Ushauri wangu, darasa la saba wakishindwa kufaulu wapelekwe moja kwa moja kwenda kwenye hivi Vyuo vya Maendeleo ya jamii pamoja na vyuo vya VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)