Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuleta hoja yake hapa ambayo ni Mapitio na Maelekezo ya Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge 2021/2022. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia kuhusiana na Mkoa wa Dodoma lakini baadaye nitazungumzia kuhusiana na suala zima la ugonjwa wa UKIMWI, madawa ya kulevya pamoja na kifua kikuu. Sisi katika Mkoa wa Dodoma kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu na pia kuifanya kuwa Jiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna miradi mikubwa ya kimaendeleo ambayo inatakiwa itekelezwe katika Mkoa wa Dodoma ili kusudi iweze kuleta picha halisi na sura halisi ya Makao Makuu. Ipo mingi ambayo imetekelezwa, lakini nina ushauri kwamba tuna uwanja wa ndege wa Msalato, sisi wananchi wa Dodoma tunafurahia sana kuwepo uwanja huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi uwanja huu pesa zake zipo, lakini tatizo lipo kwenye fidia, kwamba wale wananchi ambao walitakiwa walipwe fidia, wako wananchi kama 1,053 kati yao waliolipwa fidia ni 874, kwa hiyo bado 176. Kwa hiyo tunaiomba Hazina iharakishe kuwalipa wananchi hawa ili kusudi mwisho wa siku kazi iweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna waathirika ambao ni outer ring road ya Dodoma, barabara ambayo ikijengwa itaondoa sana msongamano wa magari katika Mkoa wetu wa Dodoma. Barabara hiyo ina kilometa 112 na waathirika ambao wanatakiwa kulipwa ni 2,672 ambao wanatakiwa kulipwa zaidi ya bilioni 15.7. Kwa hiyo naiomba Serikali ione umuhimu wa kuharakisha kuwalipa waathirika hawa ili kusudi kazi iweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba niikumbushe Serikali kuhusiana na barabara muhimu ambazo zitaleta maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Dodoma, barabara hizi zikijengwa kwa kipindi muafaka ina maana kwamba wananchi wa Dodoma tutafaidika Zaidi. Tunaishukuru sana Serikali kwa maendeleo yote ambayo imeifanya lakini pia tukipata barabara hizi zitatusaidia sana. Miongoni mwa barabara hizo ni pamoja na Barabara ya Mpwapwa - Gulwe - Kibakwe ambayo ina kilometa 124; Stesheni ya Gulwe - Kongwa Junction - Simanjiro hadi Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna daraja la TANESCO Mpwapwa linahitaji kufanyiwa matengenezo na daraja la Godegode ambalo limekuwa tatizo kubwa sana. Sambamba na hilo, Marehemu aliyekuwa Rais wetu pia alituahidi kwamba itajengwa bandari kavu ya kilometa sita katika eneo la Ihumwa. Kwa hiyo tunaomba Serikali ione kwamba mambo haya yanafanyika. Pia naomba nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba pale anapokuwa akitembea kuhusiana na mazao ya kimkakati, yale mazao matano, basi aone pia na zao la zabibu katika Mkoa wa Dodoma, tufanyiwe liwe zao la mkakati ili wananchi wa Dodoma waweze kuondokana na suala la umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie kuhusu masuala ya UKIMWI. Mimi ni Mwenyekiti wa Masuala ya UKIMWI kuna mambo kadhaa nilitamani kuyakumbusha, lakini niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo imeifanya ya kufanya maambukizi yaweze kupungua. Hata hivyo, naomba kutoa ushauri kwamba, kundi la vijana inabidi liangaliwe sana kwa sababu hili ndio kundi la waathirika wakubwa, Serikali iweze kuweka nguvu Zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna ule Mfuko wetu wa Aids Trust Fund, Serikali ione umuhimu wa kuwa na vyanzo vya kudumu vya kutunisha Mfuko huu. Jambo kubwa ambalo nataka pia niwaambie Waheshimiwa Wabunge hasa wanaume, kwa sababu takwimu imeonyesha kwamba wanaume wengi hawajitokezi kupima UKIMWI. Kwa hiyo tunaomba tuanze mfano na Wabunge wanaume humu ndani, waweze kupima UKIMWI na wakitoka hapo waweze kwenda kuhamasisha kwenye zile jamii zao kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara zetu tulikutana na wenye VVU, wakasema wao wanaishi kwa malengo kwa sababu wanaijua afya yao na sisi tunaoishi kwa matumaini maana yake hatujui afya zetu. Kwa hiyo natamani kwamba hebu idadi ya wanaume wajitokeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu tohara. Kwa kweli tohara ya wanaume pia ni muhimu sana kwa sababu imeonekana kabisa inasaidia kutokuleta maambukizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu madawa ya kulevya. Vijana wetu wengi sana wameathirika na madawa ya kulevya. Kwa hiyo tunaishauri Serikali ijenge Ofisi ya Kanda ili kusudi kuweza kuwahudumia hawa vijana hasa wale waraibu waweze kupata hizi dawa za methadone.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo napenda niishauri Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya UKIMWI, kifua kikuu na dawa za kulevya watoe elimu ya lishe katika vituo vyote vya tiba na mafunzo, kwa sababu hii elimu ya lishe itawasaidia wale wenye VVU au wale wagonjwa ili kusudi afya zao ziweze kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda sio rafiki sana naomba niseme kwa uchache kwamba, kwenye magereza yetu kumekuwa kuna shida sana ya msongamano, hivyo kusababisha magonjwa ya kuambukiza hasa TB. Kwa hiyo naomba Serikali iliangalie hili jambo, tuweze kupambana na kifua kikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja na nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)