Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Itilima
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze kuwapongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya katika Awamu ya Tano na Awamu hii ya Sita. Serikali ya Awamu ya Tano na Serikali ya Awamu ya Sita tulijikita sana kuhakikisha tunapeleka huduma bora kwa wanachi wetu. Tumejenga vituo vya afya tumejenga zahanati na tumejenga Hospitali za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo kila Mbunge na kila maswali yanapoulizwa tuna tatizo kubwa la watumishi wa kada ya afya. Ningeishauri Serikali katika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilete bajeti mahsusi kwaajili ya kada ya watumishi hawa ili kusudi fedha nyingi ambazo tunaendelea kuziwekeza kwenye zahanati zetu na kwenye hospitali pamoja na vituo vya afya ili majibu kwa wananchi wetu yaweze kupatikana kulingana na utekelezaji wa kazi tunazoendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo ambalo linakuwa la kusikitisha wakati mwingine Kijiji kimoja kina wakazi 4,000, 2,000 huko Usukumani lakini nesi anakuwepo mmoja kwa siku nzima yule nesi tunampa wakati mgumu wa kutoa huduma kwa wananchi wetu ambao tunakuja kuwakilisha humu. Ningeomba jambo hilo Serikali ilichukue na ilifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Waziri Mkuu imezungumzia mambo ya Ushirika imezungumzia mambo mengi sana. Tunaotoka kwenye mazao ya kimkakati haya ambayo tunayaona kabisa Serikali ina nia nzuri ya dhati kuhakikisha kwamba inatengeneza ushirika, inatengeneza AMCOS, inatengeneza TMX lakini yako majukumu ambayo TMX anatakiwa ayafanye lakini yako majukumu ambayo watu wa ushirika wanatakiwa wayafanye, lakini yako majukumu mwananchi naye ayatekeleze kulingana na jinsi alivyohangaika kupata hayo mazao yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la TMX ni taasisi ya Serikali lakini inatakiwa kutafuta masoko nje ya nchi lakini kinachotokea kwenye TMX ya hapa kinachofanyika yeye anaondoka anaenda kijijini anaenda kuusimamia ushirika na anaenda kuchukua 1% ya bei inayopatikana jambo hili haliwezekani na jambo hili tunawaumiza wakulima wetu na halina tija yoyote katika Taifa letu hili. Nitatoe mfano kwa miaka ya nyuma kulikuwa na chombo kinaitwa Mamlaka ya Pamba ambacho ilipewa jukumu la kuuza pamba yote ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yaliyotokea Shirika lile lilifilisika na lilileta madhara makubwa na hatima yetu leo ushirika wote ulifilisika kwasababu ya vyombo hivi. Na mfano TMX wameanza tangu mwaka 2018 kwa kasi 2019 tukainga na tatizo la kukosa masoko ya zao la pamba TMX hawa nilidhani wangeonyesha njia yao kubwa kuhakikisha kwamba sasa wanauwezo wa kutafuta masoko na kuuza mazao yetu yale lakini matokeo yake hakuna kilichofanyika na Serikali ilibidi kuingilia kati kuhakikisha kwamba wanatatua changamoto hiyo TMX alikaa pembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba sana Serikali ijaribu kuangalia inapoleta mipango mizuri hasa inapokwenda kwa wananchi wetu na tuelewe 70% ya watanzania ni wakulima na wafugaji
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, (Kicheko)
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa. (Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njalu Silanga naona Jirani yako anataka kukupa taarifa Mheshimiwa Boniventura Kiswaga
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba TMX imejiondoa kwenye jambo lake la kimsingi la kutafuta masoko na kuwa dalali wa wakulima kuwanyonya wakulima badala ya kuwaongezea masoko wakulima. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njalu Silanga unaipokea taarifa hiyo?
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwasababu ni mojawapo ya waathirika katika wilaya yake ya Magu, ilitokea sana mwaka jana na mwaka huu kwenye zao la choroko pale Maswa ulifanyika mnada wakati korosho inanunuliwa katika bei za kawaida ilikuwa 1500 mpaka 1400. TMX walipokuja kufungua mnada wao waliwauzia wakulima bei ya 1350 kwa hiyo, tayari shilingi 1500 ikawa ni short kwa wakulima wetu hawa na ikatolewa order RAS wa Simiyu akasema halmashauri i-top ile tofauti kwa wakulima jambo ambalo yako mambo mengine inabidi Serikali iyatazame na kuyachunguza hasa Wizara ya Fedha kwasababu TMX wako kwenye Wizara ile wahakikishe kwamba unapoleta mikakati ya kuja kuwasaidia wakulima si mikakati ya kuja kuwanyonga wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba…
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Taarifa
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njalu Silanga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Bashe
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kumpa taarifa msemaji na Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara ya Kilimo imeshachukua hatua kwenye suala la TMX na haitofanya shughuli za minada katika msimu wa mwaka huu na tunafanya tathmini ya ujumla kwahiyo wasiwe na hofu majaribio yaliyofanyika mwaka jana tumeona matokeo na tumeona athari kwahiyo tumeshafikia maamuzi kwamba ushirika utaendelea kufanya shughuli zake za ushirika na TMX itarudi kwenye core function yake. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Nadhani hiyo inatoa picha namna ambavyo Serikali inasikiliza sana maoni ya Wabunge humu ndani mmefanya jambo jema. Mheshimiwa Njalu Silanga.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa lakini iwe taarifa ya vitendo maana mwaka huu Bunge la Kwanza tulipokaa humu Waziri Mkuu aliulizwa swali la papo kwa papo akaeleza kwamba ushirika TMX hawataingilia katika mazao haya. Kilichotokea mikoa mingine ilianza kutekeleza walipofika Shinyanga wafanyabiashara gari zao zilizuiliwa na kupigwa mnada.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kauli yake Mheshimiwa Naibu Waziri anayoizungumza iwe kauli ya kulieleza Bunge na iwe kauli ambayo ni mahsusi kwa watanzania. Maana tunachozungumza hapa tumetumwa kuja kuwawakilisha watanzania na tumetumwa kuja kuzungumza changamoto zao ambazo wanazipata na cha ajabu zaidi yako mazao mengine hayahitaji hata kuyaingiza kwenye mifumo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoamini choroko ni zao la wakinamama ambalo walikuwa wakililima vizuri kwa mahitaji madogo madogo sasa unapobeba kilo 3, kilo 7, kilo 7 kwenda kuziweka kwenye godauni unatengeneza umaskini na manung’uniko kwa wananchi wetu hawa. Jambo hili halikubaliki na kwa sababu Serikali hii ni sikivu ya Chama Cha Mapinduzi ninaamini haya ninayoyazungumza wataenda kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu Serikali katika maeneo ambayo imefanya upembuzi yakinifu katika maeneo yetu mfano kutoka Bariadi kuja mpaka Singida ningeomba jambo hili kwenye bajeti hii basi watengee barabara ile iweze kutengenezwa na watu waweze kusafiri na kupata huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna uwanja wa ndege pale Mwanza kuna njia ya kutokea pale Ilemela by pass ya kuingia kwenda airport ningomba Serikali nalo hili ichukue ilifanyie kazi ili wananchi waondokane na msongamano wa kupita pale Mwanza katikati ambao unakuwa ni msongamano mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo Serikali ningeomba kuendelea kuishauri kwamba mambo mengi mazuri yameendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na naamini na Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kufanya hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tunahitaji sisi ndege ziendelee kununuliwa kwasababu ndege ndiyo huduma mbadala ya haraka kuleta huduma. Lakini ningeomba sana ipatikane ndege ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza kwasababu ni watu wengi wanaotoka Mwanza kuja hapa hata viongozi wa kiserikali hawa wakati mwingine inabidi waende Dar es Salaam ndiyo waende Mwanza jambo ambalo linatupotezea muda. Naiomba Serikali ndege zile tatu zije sisi tuendelee kusafiri kwa ndege, tuendelee kutoa huduma nzuri kwa watanzania ili mambo yaende vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)