Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo kwa kweli imesheheni vipaumbele vyote vitakavyokwenda kurekebisha uhalisia wa maendeleo ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekuwa mtumishi wa CCM kwa muda mrefu sana na nimepitia nafasi mbambali mpaka hapa nilipofikia. Hapa niliposimama inawezekana nikazungumza nitakayoyazungumza sitoweza kusahau au sitaweza kumsahau Hayati John Pombe Magufuli. Hata hivyo, siyo tu Hayati Magufuli, tunao viongozi ambao wameondoka wako mbele za haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka wakati Sokoine anafariki takribani zaidi ya miaka ya 10 hakuna impact yoyote ambayo ilikuwa inaonyesha kwamba tumkumbuke kwa matendo yake. Tulikuwa tunasikiliza kwenye asasi mbalimbali wakiwa wanatukumbusha wanasiasa na Serikali jinsi ya kuenzi viongozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri Hayati Magufuli amekuwa ni kiongozi bora Barani Afrika na ni kiongozi ambaye Marais wa Afrika walikuwa wanatamani kuiga mifano yake. Sasa ikitupendeza pale Morogoro roundabout twendeni tukaweke picha yake. Kwa legacy ambayo ameiacha Hayati Magufuli na kama Bunge hili kila Mbunge anayesimama anamzungumzia na sisi tufike mahali sasa tuwaonyeshe Watanzania kwamba tunamuunga mkono kwa vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa Bashe. Tulipokuja Disemba kuapa nilikaa naye hapa kantini lakini nilimueleza kuhusu zao la korosho na TMX, namshukuru sana amekuwa msikivu na alituelewa watu wa Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema Wabunge wengine wakaijua TMX. Kule kwangu Mtwara zao kubwa la biashara ni korosho. Nilikuwa nasoma kwenye ripoti yao wanasema watakuja kuwa madali lakini udalali wao korosho zetu zitanunuliwa online. Makampuni yote ya korosho ambayo yako Tanzania hususani Mtwara, yana wazawa na matajiri wengine wapo Vietnam, India na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia TMX kufika mahali wao wakala number one, kinachotokea ni nini? Ni kwamba mfanyabiashara aliyeajiriwa yuko Mtwara tayari atakuwa amepoteza ajira kwa sababu korosho zitakuwa zinanunuliwa online. Kampuni ambayo iko India na iko Tanzania na hapa kuna wafanyakazi, kama wako 20 watapunguzwa atabakia mfanyakazi mmoja. Kwa hiyo, niipongeze Serikali kwa kuwa wasikivu na kukubaliana kwamba TMX sasa ifike mahala ikae pembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru Waziri wa Maji. Waziri wa Maji alinitembelea Mtwara kuja kuangalia chujio na nikamueleza shida ya Mtwara siyo chujio ni maji na Serikali ikiweza kutupatia maji ya Mto Ruvuma tatizo la maji litakuwa limekwisha. Pia nikamueleza Waziri wa Maji kwamba mabomba yanayotumika hususani kwenye Jimbo la Mtwara Mjini yalifungwa na mkoloni, ni ya chuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata leo kama mtaweka chujio likawa linafanya kazi lakini linapita kwenye bomba ambazo zina kutu. Kwa hiyo, maji yale hayatakuwa na usalama, yataendelea kuwa na ukakasi na chuma. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Maji atusaidie kwenye mpango wake kwa sababu ameshafika mahala amesema kwamba atatutengea fedha na upembuzi yakinifu utafanyika basi hilo naomba alisimamie kwa makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tumekuwa tunazungumza ajira za vijana, kweli hili ni janga la kitaifa. Sisi Wabunge wa Mkoa wa Mtwara tuna maeneo mengi sana ya mapori na yanahitaji kufanyiwa kazi kwenye suala la kilimo lakini hatuwezi. Hii ni kutokana na jinsi tulivyowaandaa vijana wetu kwenye familia zetu hawawezi ku-compete na kwenda shamba kulima bila Serikali kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe mfano, leo tunawatibu vijana ambao wanakula madawa ya kulevya kwa gharama kubwa sana lakini tunapeleka asilimia 10 kwa ajili ya vijana, akina mama na walemavu, twende sasa na mpango endelevu, wapo vijana wako tayari kwenda kulima shambani lakini Serikali ichukuwe hatua sasa ya kuwawezesha vijana hawa tuwapeleke mashambani wakalime kilimo cha kisasa ili sasa tuweze kutoa ajira zingine mpya tofauti na zile ambazo tunazungumza.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagongwa.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)