Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu. Niungane na wenzangu kutoa pole kwa familia na Watanzania kutokana na kifo cha Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Pia nampongeza Rais wetu wa Awamu ya Sita, mama yetu Mheshimiwa Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri Mkuu kwa hotuba hii nzuri ambayo nitapenda kujikita kwenye Sekta ya Madini. Kama ambavyo tunajua, Serikali ya Awamu ya Tano wakati inaingia madarakani ilirekebisha mazingira ya uchimbaji na tukaweza kutoka pale tulipokuwa na kupata mapato kutoka shilingi bilioni 150 mpaka kufikia takribani shilingi bilioni 550, kwa kiwango hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi watu wa Wilaya ya Chunya tuliweza kutoka uzalishaji wa kilo 20 kwa mwezi mpaka sasa hivi tunafika kilo 230 kwa mwezi. Haya ni mafanikio makubwa ambayo yanaweza kupelekea kulipa kodi. Mwanzoni wakati Serikali Awamu ya Tano inaingia madarakani tulikuwa tunalipa kodi ya shilingi milioni 150, lakini sasa hivi tunaweza kulipa kodi zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa mwezi. Haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima twende mbele zaidi, tusiridhike na hapa tulipofika. Ili tuweze kwenda, kuna sheria mbalimbali ambazo kubadilishwa; na moja kati ya sheria ambazo zimebalishwa iliweza kuwataka wale wanaofanya utafiti kwenye madini, kuhakikisha majibu ya tafiti zao yanapelekwa kwenye Taasisi ya Jiolojia (GST).
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wetu ni nini? Ushauri wetu ni kwamba zile tafiti ambazo zimeshapelekwa GST, zinyambuliwe katika lugha nyepesi ambapo wachimbaji wetu wazipate na kuweza kuzitumia ili uchimbaji wao sasa ufanyike vizuri. Badala ya uchimbaji huu wa ramli unaofanyika kwa wachimbaji wadogo, itatuwezesha sasa kupata mapato mengi zaidi na mapato haya yatasaidia kuongeza wigo wa mapato ya Serikali na kuleta mapato makubwa zaidi kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa GST hawa wenzetu, bado ofisi zao ziko Dodoma. Nchi nzima huku tukitaka kupima viwango vyetu vya madini, ni lazima tuje Dodoma. Nashauri sasa kwa Wizara kuhakikisha kwamba washuke chini zaidi kwenye level ya kanda ili GST wawepo kwenye kanda na wachimbaji wetu wadogo wasifunge safari kutoka Chunya kuja Dodoma, waishie kwenye kanda. Hiyo itaweza kutusaidia sana. Ni imani yangu kwamba Serikali itawasaidia wachimbaji wadogo na uzalishaji wao kuongezeka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee pia kwa upande wa kodi. Kwa sisi wachimbaji wadogo, kodi imekuwa siyo Rafiki. Tunaomba Serikali iangalie namna gani ambavyo itaweza kutusaidia. Leo hii kwa mchimbaji huyu anaweza akapata leo kiasi cha shilingi milioni 50, lakini akiipata leo, inawezekana mwaka mzima asipate tena. Sasa nini cha kufanya? Namna nzuri ya kufanya na kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo, tuone namna bora zaidi ya kubadilisha sheria, ili wakati ambapo mchimbaji anaenda kuuza madini yake na kodi hii aweze kukatwa pale pale; kama ambavyo kodi hii inakatwa kwenye mrabaha wa 6% na inspection fee 1%, unapouza unakatwa pale pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia yale malalamiko tuliyonayo wafanyabiashara na wachimbaji wetu kwa akaunti zetu kufungwa na TRA, hili suala halitakuwepo. Maana nikienda kuuza madini yangu, pale pale nitakwa na kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, itawasidia wachimbaji wetu. Kwa kauli ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama yetu Samia amesema tusifungiwe akaunti. Kwa hiyo, akaunti za wachimbaji hazitafungwa na sheria hizi zikibadilishwa, hawataweza tena kupata matatizo yoyote ya kikodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninaloweza kulielezea ni namna ambavyo ile Service Levy tunavyoilipa kwenye Halmashauri. Service Levy tunayolipa kwenye Halmashauri ni asilimia 0.03, ndivyo wachimbaji wanavyoilipa. Sasa kwa maeneo ya Wilaya, kama Wilaya ya Chunya ambako ndiko tunakochimba madini, tunalipa kodi zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa mwezi, lakini malipo yanayobakia kwenye Halmashauri ni asilimia 0.03. Ni kiasi kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kuona namna bora zaidi ya kubadilisha hii sheria angalau kiwango hiki sasa hivi kiweze kupanda kutoka 0.03% iweze kwenda 1% au 2% ili mapato mengi yaweze kubaki kwenye Halmshauri zetu kule ambako wachimbaji wanafanya uchimbaji huu. Hiyo itaweza kusaidia haya matatizo madogo madogo tunayokimbizana nayo sasa; ya madarasa, madawati na kadhalika, kile kiwango ambacho tunakipata kitaweza kufanya kazi vizuri zaidi kwenye Halmashauri zetu kule na Serikali haitakimbizana na hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, naiunga mkono hoja iliyoko mbele yetu na ninampomgeza sana Waziri Mkuu. Ahsante sana. (Makofi)