Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Moshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa salam zangu za pole kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu na Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza Rais wetu Hayati Dkt. Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pole hizo, nitoe pongezi kwake Rais sasa Mheshimiwa Mama Samia kwa kuchukua nafasi yake kama Rais. Vile vile nawapongeza Mawaziri wote na viongozi wote ambao wengine wamebaki kwenye nafasi zao, wengine wamebadilika na wengine wameingia ili kuweza kulisongesha gurudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyo vipengele kama kumi ambavyo nitaviongelea kama muda utaruhusu. Naomba nianze na kilimo. Tumeshakubaliana kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu. Yako maeneo ya kufanyia kazi na mengine ya meshatajwa au kusemewa na viongozi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni eneo la utafiti. Nafikiri ni muda muafaka sasa Wizara itumie nguvu kubwa kwenye maeneo yote, wajue ni mazao gani yanalimika kirahisi wapi na kwa njia ipi. Nchi ambazo zinaweza kutusaidia sana kwenye hili tukichanganya na wataalam wa ndani kutoka kwenye vyuo vyetu pamoja na SUA ni pamoja na Egypt, Israel na Netherland ambao wamefanikiwa sana kwenye kilimo pamoja na mazingira yao kuwa magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine muhimu sana kwenye kilimo ni la umwagiliaji. Bwawa la Nyumba ya Mungu lilijengwa na Serikali yetu miaka ya 1960, nafikiri ni mwaka 1967. Eneo lile lilipojengwa limekuwa ni kichocheo kikubwa. Mzungumzaji aliyepita ameongelea mafuriko huko kwao Kyela. Serikali ikiweka nguvu katika namna ya kuyachukua haya maji na kutengeneza mabwawa kwenye maeneo yenye kilimo, itasaidia sana kuondoa utegemezi wa kilimo hiki ambacho kinategemea mvua na ambavho hakina tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo, nafikiri kuna vitu ambavyo tuna uwezo navyo, ambavyo tuna mahitaji navyo sana hapa ndani. Tuna upungufu wa mafuta ya kula. Kwa hiyo, tukiwekeza kwenye alizeti, tayari soko lipo, la ziada litakuja tu baadaye. Tuna upungufu wa ngano; tukiwekeza hapo maana yake soko la ndani lenyewe linaanza na linatosheleza. Hata sukari, tuna upungufu na tunatumia fedha nyingi sana kuagiza kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa na mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha miaka kama ni mitano au kumi hili tatizo linaisha, tunaweza kabisa na tutakapofanikiwa hilo, basi nyongeza itakayopatikana, itaweza kuuzwa nje na kutupatia fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kugawa maeneo ya kimkakati, yaani block zone pamoja na kuwashirikisha wakulima wadogo. Ningependa sana kama ningeona mkakati wa kuwavutia wakulima wakubwa wa ndani na wa nje kwa kuwatengea maeneo na kuweka sera ambazo zitawavutia waje walime hapa kwetu. Wakilima, watatusaidia kwenye soko la ndani na vile vile kwenye kuuza nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa ambalo linawezekana hapa na ninalitolea mfano kwenye taasisi ile ya TAHA ni kutumia hii block zone. Ukishawaweka watu kwenye block ni rahisi kuwafuatilia na kuwapelekea wataalam wanaowashauri kama inavyofanya Taasisi ya TAHA kwenye mboga mboga pamoja na matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishaweza kuwekeza vizuri tukaweka hizi sera vizuri kwenye kilimo, tunahamia kwenye viwanda. Viwanda vitakuwa ndiyo watumiaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo. Hapa ndiyo sera tunayokwenda nayo, lakini sijaona sera au incentives zinazosababisha watu watoke maeneo mengine waje waweke viwanda vyao hapa. Sijaona. Ni muda muafaka sasa Wizara ione namna ya kuendelea kutafuta na kuweka mazingira yatakayovutia wawekezaji wa nje na wa ndani kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia, tukiweka viwanda vya vile vitu ambavyo tuna upungufu navyo ndani, maana yake tunahakikishia wawekezaji kwamba soko lipo; hivyo ambavyo nimetaja hapo juu kwenye kilimo; suala la mafuta, sukari na vitu vingine ambavyo tayari tuna uhitaji navyo sana ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengine yanatia hasira. Nami nilisema mara ya kwanza na ninarudia tena. Naunga mkono wale waliobinafsishiwa viwanda kwa nia ya kuviendeleza ili vitoe ajira na viingize kodi wakashindwa, wanyang’anywe tuvitangaze tena upya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Moshi kuna Kiwanda cha Magunia, kimefungwa, hakifanyi kazi; kuna Kiwanda cha Viberiti, Kibo Match, kimefungwa na wana nyumba pale zimefungiwa chini, hazifanyi kazi. Ili kulitilia nguvu hili, ni muda muafaka sasa tuvichukue, halafu tutangaze upya viwanda hivi viweze kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la afya. Hili kidogo niliongelee kwa choyo kwa kuangalia Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa huu una Hospitali ya Rufaa moja, inajulikana kama Mawenzi, imejengwa miaka mingi iliyopita, 2022. Hospitali ile imekuwa ya kizamani sana na miundombinu yake iko kwenye hali mbaya sana. Kinachosikitisha zaidi, kuna Jengo la Mama na Mtoto ambalo lingekuwa na huduma nyingine za kisasa katika design yake kama IMR, X-Ray za kisasa na vitu kama hivyo; lakini imeanza kujengwa 2008 mpaka leo haijamalizika na ni jengo moja na sijaiona kwenye ripoti ya CAG kwamba ni nini kilisababisha inachukua muda mrefu namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iende ikaangalie pale Mawezi kuna nini? Tangu mwaka 2008 jengo moja halimaliziki. Naomba sana kwa sababu Mkoa wa Kilimanjaro hatuna Hospitali ya Rufaa inayoendana na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Moshi Mjini au Moshi kama Wilaya hatuna Hospitali ya Wilaya, tunatumia hospitali za binafsi sasa hivi. Mheshimiwa Rais aliyetangulia mbele za haki, Hayati Dkt. Magufuli alituahidi. Nami naomba ahadi hiyo iendelee kuhamishiwa kwa viongozi waliopo na sisi tupate Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya suala la afya, nakwenda kwenye miundombinu. Kwanza naipongeza Serikali kwa mafanikio iliyopata. Kwenye SGR, ATCL, Bandari zinazoendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na barabara nyingi zinazojengwa. Natamani sana nione Wizara zinazohusika zikifanya juhudi ya kuhakikisha tunakuwa na economic diplomacy ya kuwashawishi kwa mfano watu wa Kongo. Kwamba ni kwa nini wapitishie mizigo yao kwa barabara kupitia Zambia badala ya sisi kuboresha bandari ile ya Kigoma na Rukwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliongelee kidogo. Upande huu wa Mashariki wa nchi yetu tayari kumeshafunguka, lakini upande wa Ziwa Tanganyika pale ambapo tunapakana na Kongo ambapo ni milking cow, inatakiwa zile bandari ziboreshwe. Pale Rukwa reli iende mpaka pale bandarini, ziwekwe meli za kuweza kuvusha vitu viende kule Kongo. Balozi wetu pale atusaidie kuongea na watu wa Kongo nao wafungue barabara kwa upande ule wa kwao mambo yaende. Hakuna sababu ya mizigo kutoka kwenye bandari ya Dar es Salaam, ipitie Zambia ndiyo iende Kongo. Ni hela tumezikalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba hilo tuliwekee nguvu kidogo liweze kuleta…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Ahsante sana.
MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)