Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nashukuru sana kwa kuweza kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia nguvu, uwezo, uhodari na umahiri wa kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutambua Tanzania yetu jinsi tulivyoweza kuridhika na kujidai na kujivuna kwa kuweza kupata Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Jemedari Mkuu mwanamke kuiongoza nchi yetu. Yeye ni Rais mwanamama wa mwanzo katika block hili la Afrika Mashariki. Niseme kwamba Mheshimiwa Jemedari wetu Mkuu Mheshimiwa Rais Samia ninaweza ku-quote ‘is one of our own’ ni mwenzetu. Anatoka kwenye block ya akinamama. Uhodari wake na umahiri wake na ujasiri wake kwenye kazi tunamjua tangu asubuhi. Kwa hivyo niwatoe wasiwasi kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu viatu hivi vimemfaa sawasawa, tena vimekuwa high heels atakwenda mdundo wa kuchumpachumpa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kumpa ushirikiano kama vile tulivyokuwa tunampa kipenzi chetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye ametangulia mbele ya haki. Kwa nukta hiyo, namwombea rehema. Mungu ampumzishe kwa amani na natoa pole sana kwa familia ya Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na mchango wangu kwa kugusia program za kukuza ujuzi wa vijana ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Ni dhahiri vijana wengi wanapotoka vyuoni wanakuwa hawana ujuzi wa kutosha katika kufanya kazi zao na hivyo kuweza kushindwa kuhimili ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi. Programu hii inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu imetumia gharama kubwa sana kwa kuwawezesha vijana hawa kupata nauli, fedha ya chakula wakati wanapokwenda kufanya mafunzo ya uanagenzi katika mashirika mbalimbali. Kwa sababu baadhi ya wanufaika hawalipii gharama hizi, lakini ni hii programu imewawezesha vijana wengi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uko umuhimu wa kuongezwa bajeti ili kuweza kuwafaidisha vijana wengi waweze kupata hii programu ya uanagenzi. Katika Ofisi hii ya Waziri Mkuu iko shida moja ambayo tumeiona sisi na hii nayo inatokana na tatizo la kukaimisha watumishi kwa muda mrefu na tatizo la kutoajiri watendaji wakuu wanaostahili na hivyo kuleta shida katika kuchukua hatua wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, shida hii ya kukaimisha kwa muda mrefu iko kwa taasisi mojawapo naweza kuitaja ni ya OSHA. Mkurugenzi anayekaimu OSHA amefanya kazi muda mrefu tangu sisi tunaingia hapa, tulipowezeshwa kipindi cha mwanzo, huyu anakaimu na anafanya kazi nzuri mpaka sasa hivi. Niulize, hivi huyu Mkaimu mwanamama tena wa OSHA ataendelea kukaimu mpaka lini? Awamu ya Tano Mkaimu huyu alikuwepo, Awamu hii tulivyoingia kwa bahati ya kuwezeshwa na wajumbe wetu watu wazuri sana tumemkuta tena anakaimu. Sasa nishauri Ofisi ya Waziri Mkuu ichukue hatua ya kuwa-sort out hawa watu mapema sana, ingawa shida hii ipo pia kwenye taasisi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nigusie masuala ya watu wenye ulemavu. Ofisi ya Waziri Mkuu imechukua hatua za dhati kuimarisha kitengo cha kuratibu masuala haya na jambo zuri nipongeze Wizara hii imeongeza bajeti kutoka milioni 978.50 kwenye mwaka 2019/2020 hadi bilioni 1.29 kwa mwaka 2021/2022. Hili ni jambo zuri na hili kundi litafaidika kwa programu mbalimbali zitakazoandaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko shida nyingine inayoikumba ambayo haijafanyiwa kazi ambayo ni kutokuanzishwa kwa kanzidata. Kwa hiyo tunashauri kuanzishwe kanzidata ili kuweza kuwajua watu hawa wenye ulemavu kwa nchi nzima. Hii itasaidia kuratibu vizuri mipango kwa kuwatambua na kujua nini shida zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye jambo letu hili ambalo linatuadhibu sana katika Taifa hili, nalo ni maambukizi ya maradhi ya UKIMWI. Tunahitaji huduma kukabiliana na kadhia hii, kwa hivyo Mfuko huu wa UKIMWI lazima uweze kutunishwa. Hapa nazungumzia Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI wa ATF, Serikali ichangamkie kutenga fedha zaidi za ndani na kuzitafuta kama tozo kutoka sehemu yoyote ambayo itaona inafaa mradi Mfuko huu uweze kutuna kwa sabbau kazi yake ni muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba kusisitiza kampeni ya kuwezesha wanaume zaidi kufanyiwa tohara. Kwa sababu ugunduzi wa kisayansi umegundua maambukizi ya UKIMWI yanatokana na shida hiyo. Kwa hivyo hilo jambo lifanyiwe kazi, kampeni tuipige, tuhakikishe na kama itabidi pia basi tutakwenda kujifunza namna gani ya kucheza jando kwa watu wa Mtama huko. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la dawa za kulevya; hii ni kadhia kubwa sana inayolikumba Taifa letu. Fedha za kutosha inabidi zitengwe ili kudhibiti na kuhakikisha kwamba kundi hili, Mfuko huu wa Kudhibiti Dawa za Kulevya unafanyiwa kazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)