Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia jioni hii ya leo, lakini kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima, afya, hatimaye nimeweza kusimama mahali hapa siku hii ya leo. Nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Ni hotuba ambayo imetuonesha tulikotoka, tulipo na tunakotaka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, tumeona wametenga bilioni mbili na milioni 600, lakini milioni 600 ni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ofisi na bilioni mbili ni kwa ajili ya maafa. Niombe sana kwasababu kila mwaka tunapata mabadiliko ya tabia nchi, tunapata maafa na majanga mbalimbali, niombe sana fedha hizi ziongezwe ili ziweze kusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano katika Jimbo langu la Mvomero katika Kata ya Muhonda na Kata ya Sungaji vijiji zaidi ya vitatu vipo kwenye hatari. Na mwaka jana tulipoteza nyumba zaidi ya 150 ziliondoka na mto, lakini mwaka huu vijiji vile ambavyo viko pembezoni yam to vipo kwenye hatari kubwa sana ya kuondoka na mto kama mvua zitaendelea kunyesha mvua kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sana wenzetu wa mazingira watusaidie kwenda kuona yale maeneo ili kuweza kuokoa nyumba ambazo zipo katika maeneo hatarishi. Tunaweza tukapoteza vijiji kwa pamoja zaidi ya vitatu kwa hiyo, niombe sana waweze kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tunatambua kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa hili, lakini tuna tatizo moja ambalo tukichangia wengi tunajisahau, Maafisa Ugani ambao kimsingi hawa ndio wataalamu wa kilimo na sisi wananchi wetu wanalima kupitia jembe la mkono. Maafisa Ugani wengi wanakaa maeneo ambayo hakuna kilimo, wanatoka katika vijiji wanakwenda kufanya mpango wa kuishi katika maeneo ambayo kwao ni rafiki, wale wakulima wetu kule walipo hawana wataalamu na tunajua kila mwaka kunakuwa na mabadiliko ya kalenda ya kilimo kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Wilaya yetu ya Mvomero ina tatizo kubwa sana la tembo. Tumepata bahati ya kupakana na Hifadhi ya Mikumi, lakini bahati hii sasa imegeuka kuwa laana kwa watu wa Mvomero, tumeshapoteza zaidi ya watu 23 mpaka sasa hivi. Na jana niko hapa nimetumiwa message mwananchi mmoja amekanyagwa na tembo kichwani na nimewachangia nikiwa hapahapa ndani ya Bunge, lakini hali ni mbaya hakuna mwananchi yeyote ambaye analima katika maeneo ya Tarafa nzima ya Mlali zaidi ya kata sita hakuna mtu ambaye anashughulika na shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana kwa Serikali waende wakatusaidie. Tusipoenda kuwasaidia kuwaondoa wale tembo ambao wako katika lile eneo la Tarafa ile ya Mlali tutashindwa kulima. Nilienda kumuona Waziri wa Maliasili, alinipa ushirikiano, alituma timu yake ilikwenda, lakini tatizo bado liko palepale, lakini mbaya zaidi sheria ambayo iliwekwa kwa ajili ya fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria inasema eka moja shilingi 150,000/= lakini mbaya zaidi mtu ambaye amelima chini ya eka moja hawezi akalipwa fidia kwa mujibu wa sheria. Sasa niombe sana tufanye mabadiliko kidogo katika eneo hili kwa sababu, tunajua wakulima wetu wengi wanalima chini ya eka moja. Lakini mtu mwenye chini ya eka moja akipata madhara ya tembo basi hawezi akapata fidia yoyote, lakini wale ambao wamefariki dunia wanatakiwa kwa mujibu wa sheria walipwe shilingi 1,000,000/=, lakini mpaka sasa hivi wananchi wengi bado wanadai hizi fedha na hawajui lini watalipwa hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuna hawa watu wanaoitwa TFS. TFS ni tatizo sana nchi hii, hawa ni Wakala wa Misitu Tanzania, sisi tunapotoka kule vijijini shule zetu nyingi hasa za pembezoni hazina madawati na tunayo misitu ya asili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoenda kuomba vibali kunakuwa na urasimu mkubwa sana wako tayari kuona miti inaanguka na kuoza, lakini sio kutoa kibali kwa ajili ya kuvuna na kutengeneza madawati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia hawa ndio wanasimamia hifadhi zetu Tanzania. Wanaacha wananchi wetu wanaingia kwenye hifadhi, wanaanza kusafisha shamba, wanapanda, wanalima, kama ni mahindi ama mpunga, wakifika kwenye hatua ya kuvuna ndio wanakuja na kuanza kuharibu mazao yao, lakini wakati wanafanya maandalizi ya kupanda wanawaangalia. Kwa hiyo, niombe sana hawa wati wa TFS kuna mambo mengi sana ambayo Serikali inatakiwa wafanye mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Haya, kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, imegonga ya kwanza.

NAIBU SPIKA: Zikiwa dakika tano wanagonga moja.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)