Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza kwa unyenyekevu mkubwa naomba kukushukuru sana kwa kunifanya kuwa mchangiaji wa kwanza wa hotuba hii ambayo ni muhimu sana. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufanya wote tuamke salama tuko hapa ndani.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie dakika zangu kumi kuongea kuhusu TARURA. Naomba niiongelee TARURA katika Wilaya ya Same, TARURA ndani ya Same Mashariki, halafu nikipata nafasi nitakwenda mahali pengine kidogo.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba mpate picha kamili ya Wilaya ya Same. Wilaya ya Same iko ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro lakini ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro Wilaya ya Same imeketi kwenye asilimia takribani 40 ya Mkoa mzima wa Kilimanjaro. Kwa hiyo, nikiwa na maana kwamba katika Mkoa mzima wa Kilimanjaro wenye wilaya saba, Wilaya ya Same imeketi kwenye asilimia takribani 40, mki-google mtaikuta hapo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wilaya ya Same ni kubwa sana ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro. Hata hivyo, Wilaya ya Same ndiyo inayopata pesa kidogo ukilinganisha na wilaya nyingine. Hapo naona kidogo nimeeleweka.

Mheshimiwa Spika, TARURA haikuanzishwa siku nyingi sana, imeanzishwa tarehe 2 Julai, 2017. Malengo ya TARURA yalikuwa ni kuimarisha uzalishaji, kwamba wananchi waweze kuzalisha lakini mazao yao yafike sokoni. Hata hivyo, nikiwa mkweli TARURA kwa sababu ya upungufu wa pesa zinazotolewa haifanyi kazi ambayo ndiyo lengo la kuanzishwa kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye Jimbo langu la Same Mashariki, dakika siyo nyingi. Same Mashariki niseme ukweli ni jimbo korofi. Serikali fanyeni taratibu za kupitia majimbo yote myatambue majimbo ambayo ni korofi, laini na madogo ili ufike wakati mgawe sawa hizi rasilimali ndogo tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Same Mashariki lina tarafa tatu; Tarafa ya Ndungu, hii ni tambarare, tarafa zinazonisumbua sana ni tarafa mbili ambazo ni za milimani, siyo miinuko, ni milimani. Hao wanaoishi milimani wana winter na summer kama Ulaya. Wananchi wanaoishi milimani tatizo lao kubwa, nikiri na naomba Serikali muende huko ni barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara zote za wananchi wangu wa Same Milimani ni za TARURA. Niseme ukweli, TARURA Wilaya ya Same hatupewi fedha, japo wananchi wa Same Mashariki nina uhakika kuwa ni wananchi tofauti na wananchi wengine, kwani wanachimba barabara zao wenyewe. Asilimia kubwa za barabara za milimani katika Tarafa ya Gonja, Tarafa ya Mambavunta kwenye milima mikubwa na wanachimba barabara zao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi hiki sikuwa na njia, maana wananchi wa milimani wako kipindi cha mavuno, wanavuna tangawizi; na wa maeneo ya tambarare Tarafa ya Ndungu wanalima mpunga. Barabara za TARURA ambazo ndiyo zingewezesha wananchi kutoa mazao yao kutoka mashambani kufikisha barabara kuu, zote zimekufa. Sikuwa na njia nyingine, ila mimi mwenyewe kama Mbunge niliongea na Mkurugenzi, nikatumia fedha za Mfuko wa Jimbo, nikaweka Mkandarasi. Fedha zile zingenisaidia kwa vitu vidogo vidogo, lakini uone sasa fedha za Mfuko wa Jimbo nimefanya kazi ambayo ingefanywa na TARURA, siyo haki! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimechonga barabara kilometa 93.16. Mpaka sasa hivi ninapoongea hapa, Mkandarasi yule bado yupo kwenye eneo anaendelea kuchonga barabara zile. Zile fedha ningetengeneza matundu ya vyoo, ningenunua madaftari na nini, zote nimeweka mkandarasi. Nimezungumza na Mkurugenzi, maana sikuwa na njia nyingine. Naomba nilete documents za huyo Mkandarasi huko kwako.

Naomba mchukue hizi documents mpeleke kwa Spika. Mpe Spika. (Makofi)

(Hapa Mhe. Anne K. Malecela alimkabidhi pageboy nyaraka ziweze kumfika Mezani kwa Spika)

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, lazima Serikali ipite iangilie haya majimbo. Haya majimbo hayafanani. Zile fedha za Mfuko wa Jimbo ningependa kufanyia mambo madogo madogo ya kuchochea maendeleo, lakini zote nimekwenda. Nimeweka Mkandarasi mwenyewe wakati ni kazi ya TARURA. Kwa kweli hapo sikufurahi sana. Imenibidi nifanye hivyo niokoe maisha ya wananchi wangu. Wananchi wa Same Mashariki waliniheshimu wakanichagua kwa kura nyingi sana, wakamchagua Rais wangu kwa kura nyingi, wakachagua Madiwani, tena siyo kwamba kura zimeibiwa, acheni maneno; na Madiwani wote 14. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipoona wananchi hawana uwezo sasa wa kusafirisha mazao, nikachukua fedha nilizopewa na Serikali, tena Serikali angalieni vizuri, ongezeni hizi fedha kidogo. Hizi fedha mtuongezee maana mlikuwa mnaangalia na population, wananchi wameongezeka sana, tuongezeeni hizi fedha.

Mheshimiwa Spika, kutokana na nilivyoongea hapa kuhusu ukubwa wa Wilaya ya Same ambayo ni takribani asilimia 40 ya Mkoa wa Kilimanjaro, tuna tatizo sana la upande wa afya. Tuna Hospitali ya Wilaya moja ambayo ipo Same Magharibi, ipo mpakani mwa Wilaya ya Same na Wilaya ya Mwanga. Wananchi wa Same Mashariki wapo mpakani mwa Mkoa wa Kilimanjaro na Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Spika, nawanyenyekea Serikali, nimeshukuru juzi alikuja Naibu Waziri wa Afya, alitembelea lile Jimbo, akatembelea upande wa afya kwa siku mbili, aliona hali halisi. Niinyenyekee Serikali, oneni umuhimu wa kuweka Hospitali ya Wilaya nyingine upande wa Mashariki kwa sababu eneo ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa TARURA, nilisahau kukwambia kitu kingine, nina barabara moja ambayo ni kubwa sana, inatoka Hedaru kwenda Vunta mpaka Miamba. Hii barabara inabeba wananchi takribani asilimia 40 ndani ya Jimbo langu. Hii barabara haipitiki kabisa na ndiyo barabara inayochukua asilimia 40 ya wananchi, lakini imekufa. Barabara hii magari yanapita kwa shida na ndiyo iliyobeba tangawizi yote ya Jimbo langu. Hii barabara naomba isipewe fedha kidogo kidogo na TARURA, TARURA watafute fedha za Mradi wa Maendeleo, zipelekwe kwenye Tarafa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali…

(Hapa kengele ya kwanza ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, hiyo ni kengele ya pili?

SPIKA: Ni ya kwanza.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, tena sasa nasimama vizuri.

Mheshimiwa Spika, Serikali ifanye kazi ambayo ni ya muhimu na ninaomba jibu hapa, mpite mwangalie majimbo yote ya nchi ya Tanzania. Haya majimbo hayafanani. Hayafanani! Huwezi kuzungumzia Jimbo la Same Mashariki ukaja kulinganisha na Dodoma Mjini. Hapana, hapana!

Mheshimiwa Spika, Serikali ni lazima mtuambie, mnatuangaliaje kwenye haya majimbo? Wengine tunateseka, wengine wanastarehe. Sipendi kupiga kelele hivi, isipokuwa naumia. Wananchi wangu ambao hawana hali inayoridhisha, wana hali mbaya sana. Nafikiri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amenisikia. Nitaomba nifanye naye ziara tukimaliza hii hotuba, nipite naye kwenye lile Jimbo hata siku moja tu, kama zaidi, si ataugua!

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)