Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya TAMISEMI. Kwanza nianze kwa kusema naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja nisije nikasahau.

Mheshimiwa Spika, kilio kikubwa kila mahali kwa kweli ni TARURA na waathirika nadhani ni sisi wote Wabunge ambao tupo humu. Nilikuwa na wazo moja, hivi haiwezekani kuunganisha Wakala wa barabara TANROADS na TARURA? Maana yangu ni kwamba wangeunganishwa hawa halafu labda Waziri akawa mmoja na watendaji kama Makatibu Wakuu wakawa tofauti ili center ya fedha iwe moja kwa ajili ya ufanisi wa hii TARURA.

Mheshimiwa Spika, maana yake TARURA kwa kweli bajeti yake pamoja na kwamba imetengwa, lakini bado ni ndogo ukilinganisha na matatizo ya TARURA yaliyoko kila mahali. Kwa mfano, Tabora tunaitwa Toronto; ni pale mjini. Ni kweli Tabora ukitelemka usiku ni kama Toronto kweli, lakini ni mjini. Ukienda vijijini hali ni mbaya, barabara ni mbaya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la walimu. Walimu wengi wamejaa mijini na hasa kwenye Shule za Msingi. Wengi wamejaa mijini na shule za mjini zimefurika. Vijijini kuna shida sana ya walimu kukaa. Sasa najiuliza ni kwa nini? Moja ya sababu ni mazingira yenyewe ya maeneo ya vijijini ambayo walimu wanakimbia kukaa huko. Nilikuwa naishauri Serikali iangalie ni njia gani mbadala watafanya kuweza kuwashawishi walimu wapende kukaa vijijini kama ambavyo wanakaa mjini. Vinginevyo huu wimbo wa upungufu wa walimu vijijini utaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye vituo vya afya kuna juhudi kubwa zinafanyika, nyingine ni za wananchi wenyewe kujitolea kujenga vituo vya afya. Hali bado siyo nzuri, nadhani ni katika nchi nzima ingawa kwa mfano Tabora tunacho Kituo cha Afya cha Maili Tano; kituo kile, kile chumba chake cha upasuaji theater kuna kitanda tu ambacho alitoa mdau mmoja. Hakuna vifaa vingine vyovyote vile vya kuwezesha kile kituo kiweze kufanya kazi. Kwa hiyo, naomba Wizara iweze kutusaidia katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lingine kwa idhini yako, nimejaribu kuangalia kwenye kanuni kama ningeweza kuomba mwongozo kwenye kanuni, nimeona siyo jambo ambalo limetokea leo, lakini kwa idhini yako hata hii Wizara naomba uniwezeshe au unipe ruhusa niweze kuchomekea jambo. Kuna vijana wale ambao wamefukuzwa, walikuwa wanajenga Ikulu, wapo kama 854. Vijana wale walikuwa miongoni mwa wale 2,400.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkuu wa Majeshi ameshatoa ruling ya vijana wale kuondolewa au kufukuzwa, maana yake wamesharudishwa makwao. Nilikuwa na ombi, siyo kwamba naunga mkono vitendo ambavyo wamefanya wale vijana vya kutaka kugoma, lakini naangalia pia impact yake kule walikokwenda kwenye maeneo yao na sehemu mbalimbali. Hawa vijana wamefanya kazi kwa miaka karibu mitatu na kweli waliahidiwa ajira na Mheshimiwa Rais ambaye sasa ni Hayati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninahisi ni pamoja na mkanganyiko wa mawazo. Kwanza kwa kuondokewa na Mheshimiwa Rais, lazima watakuwa walichanganyikiwa. Walisahau kwamba na Mheshimiwa Rais ambaye yupo sasa majukumu yale atayatekeleza kama kawaida. Nadhani iliwachanganya; nahisi, mimi kama Mwakasaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaombea vijana hawa kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Mama Samia Suluhu Hassan, kama wanaweza kusamehewa, ni kweli wamefanya jambo ambalo kijeshi wanaita ni uasi, walitaka kuandamana, lakini tuangalie na fate zao wenyewe na familia zao wanakoenda. Namwomba sana Mheshimiwa Rais kama itampendeza kuwasamehe vijana hawa wamejitolea sana kujenga Ikulu yetu na nina hakika waliko wanajutia kile walichotaka kukifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)