Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Wizara ya Elimu kudahili Walimu tarajali 5,690 katika vyuo vya UDOM, Kleruu na Monduli. Pamoja na kudahili wanafunzi hao inaonyesha kuna upungufu wa Walimu 22,000 wa sayansi bado tuna hitaji kubwa sana la kudahili Walimu zaidi. Wizara ingefikiria kufanya programu maalum walau miaka nane (8) ili kuzalisha Walimu wa Sayansi nchini kwa wingi kwa kuwapeleka vyuo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kujenga maabara katika kila sekondari za kata. Naipongeza pia Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweka bajeti ya kununua vifaa kwa ajili ya maabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, inaonekana pia kuna upungufu wa Walimu wa lugha hasa Kiingereza. Je, kwa nini Wizara isirejee utaratibu wa miaka ya themanini hadi miaka ya tisini ambapo Walimu walikuwa wanasoma kwa michepuo? Kwa mfano:-
(i) Marangu – Kiingereza
(ii) Korogwe – Kiswahili
(iii) Mkwawa – Sayansi
(iv) Monduli – Kilimo
(v) Mandaka/Monduli - Kilimo
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa michepuo ulidahili wanachuo kutokana na ufaulu wao. Je, kwa nini Wizara isirejee mtindo huu ili kupata Walimu waliosomea masoma hayo? Wizara iangalie wapi tulikosea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri kuna mradi wa Education and Skills for Productive Jobs Programme (ESPT). Mradi una nia ya kukuza stadi za kazi na ujuzi. Sekta zilizopo ni sita (6) nazo ni za kukuza uchumi, kilimo, uchumi, utalii, uchukuzi, ujenzi, nishati na TEHAMA. Nashauri fani ya ushonaji na upishi nazo ziongezwe. Wizara inaweza kuona fani hii si hitaji lakini fani ya ushonaji/upishi ni fani ambazo zimeinua wananchi wengi katika ujasiliamali. Inabidi wanafunzi waanze kufundishwa fani hizi tangu msingi ili kuwaandaa wakifika VETA waweze kupata ujuzi mzuri zaidi na itasaidia vijana wengi kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu maalum wengi wameizungumzia. Nashauri Wizara ifanye utaratibu wa kufanya sensa ya watoto wenye ulemavu kwani watoto wengi wenye ulemavu wanafichwa. Katika ukurasa wa 97, kiambatanisho (6) kinaonesha idadi ya wanachuo wenye ulemavu wanaodahiliwa katika vyuo ni kidogo sana. Tunataka kujenga Taifa lenye uchumi wa kati ni budi Serikali ikaona umuhimu wa kudahili wanachuo wengi zaidi wenye ulemavu ili nao waweze kupata fursa nyingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sula la maslahi ya Walimu TSD ambayo sasa ni TSC inabidi ipewe nguvu ya kufanya kazi. Ni vema Wizara ya Elimu na TAMISEMI kuona jinsi ya kuipatia fedha za kutosha ili Walimu waweze kuhudumiwa vizuri zaidi. Kwa kuwa TSC inasimamia Walimu wa shule ya msingi/sekondari katika masuala ya nidhamu, maadili, kupandisha vyeo, kuthibitisha Walimu kazini na kutoa vibali vya kustaafu, vikao vya kisheria (statutory meetings) havifanyiki kutokana na ukosefu wa fedha. Inabidi Wizara ya Elimu na TAMISEMI waiangalie TSC kwa jicho la pekee ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri kwa ajili ya ustawi wa Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wadhibiti Ubora wa shule za msingi/sekondari, ukurasa wa 18. Naipongeza Serikali kwa kusomesha Wadhibiti Ubora 1,435 ambao wamepata mafunzo ya stadi za KKK ili kutoa msaada kwa Walimu wanaofundisha KKK. Pamoja na kuwepo kwa Wadhibiti hao ni vema Wizara ikaweka utaratibu maalum wa kuwapeleka masomoni Walimu kipindi cha likizo ili wapate mafunzo rejea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 10, kipengele cha 5.0, mapitio ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2015/16, katika kusimamia utekelezaji na mambo yaliyobainishwa nazungumzia kipengele (v), naomba pia Walimu wa michezo wapewe mafunzo ili waweze kuwafundisha watoto wetu michezo kwani hakuna ubishi michezo ni ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza tena Wizara ya Elimu, Waziri na timu yote. Nawatia moyo waendelee na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.