Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza kabisa, nimpongeze Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri sana. Niseme tu nilifarijika sana kuwaona Machifu wale kutoka Iringa na nguo zao za asili. Tujue tu nchi yetu ina tamaduni nyingi sana na style ziko nyingi sana za namna ya kutambua tamaduni hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TAMISEMI ni hati ya kila kitu kinachoendelea nchi hii. Kama nilivyokwishasema siku nyingi tu Mwenyezi Mungu awabariki sana watu walioandika ilani hii. Niwatambue Mheshimiwa Dkt. Bashiru na Mheshimiwa Polepole wako hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunatafuta kura safari hii hatujatoa ahadi zile nyingi za wanasiasa kwa sababu Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeweka kila kitu. Kwa hiyo, kazi yetu iliyobaki sasa ni kuhakikisha Ilani hii inatekelezwa kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wameongea Wabunge wengi hapa kuhusu TARURA. Nimshukuru, nilikuwa na jirani yangu hapa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii ameniambia imeongezwa karibu bilioni mia moja na kitu kwa TARURA; kama ni kweli tuwapongeze sana, lakini bado Kamati imeendelea kusisitiza nia ya kuiongezea pesa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya yangu ya Kiteto tunatengewa shilingi bilioni moja, milioni 400 na…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO Mheshimiwa Spika, nampa Taarifa mzungumzaji, anasema TARURA imeongezewa bilioni 100 ni pesa ndogo sana hizo, hazitoshi kabisa. Naomba uendelee. (Makofi)

SPIKA: Unapokea Taarifa hiyo Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto?

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakubali na ninapokea Taarifa hiyo, lakini lazima tuseme kwamba wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anafunga Bunge la mwezi wa pili, alisema hivi, naomba nimnukuu: “Mheshimiwa Spika kumejitokeza mjadala unaohitaji uboreshwaji wa miundombinu ya barabara za mijini na hasa vijijini. Vyombo vya TARURA na TANROADS vinafanyia kazi na sasa tutakusudia kuongeza uwezo wa vyombo hivi na hivyo Waheshimiwa Wabunge tumepokea ushauri wenu.” Kwa hiyo, waliyofanya tuwashukuru, lakini kama walivyosema Kamati na kama alivyosema Mbunge aliyenipa taarifa, tuendelee kuongeza pesa kwa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natoa taarifa tu kuhusu Kiteto, mfano, tunapata karibu shilingi bilioni moja na mia nne na hamsini na nne na chenji kidogo, lakini uhalisia ni shilingi bilioni saba. Huo ni mfano tu kwamba tunahitaji pesa nyingi sana kwa TARURA.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mbunge wa Same, Mheshimiwa Mama Kilango, ni kweli Wilaya ya Kiteto ni kubwa unachukua Mkoa wa Kilimanjaro unachukua na Jimbo la Kongwa, combine, ndio Wilaya ya Kiteto, kubwa sana. Kwa hiyo, nakubaliana naye kwamba tunapotengeneza vipaumbele hapa tuangalie jiografia ya majimbo haya, ni kubwa sana. Mheshimiwa Spika alikuja kunitafutia kura, tumetembea kata nne tu, nakushukuru sana, lakini kila mkutano tulioufanya kero namba moja ni barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Kata yangu moja inaitwa Dongo, yaani ni kubwa saba, kwa hivyo ndugu zangu tuangalie sana suala hili. kila mkutano niliofanya na nilikuwa naangalia notice zangu wakati natafuta kura, kila mahali nimekwenda changamoto naandika, barabara. Tukifanya hivyo Watanzania watakuwa wamefarijika sana. Barabara za Kata za Sunya, Asamatwa, Magungu, Dongo, Makame, Katikati, Robosoid, Mserengine, Olpopori, Kiberesa, Nigish, Mbeli na Kiteto ni bread basket, mahindi yote yanayokuja huku yanatoka Kiteto, kwa hivyo, tuongeze juhudi katika kutengeneza barabara hizi ili wananchi hawa waongezee bidii.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo hata Kamati imesema, ni hizi asilimia 10 ambazo ziko kwenye Ilani yetu. Kwa hiyo, sisi ni kutembea na Ilani tu, ukurasa wa 30, tuwe wakali kwa halmashauri zile ambazo hazitengi asilimia kumi. Sio kwamba tu wana-violate takwa la kisheria, lakini hawasomi Ilani yetu. Kati ya vitu ambavyo Wabunge tunatakiwa tuwe wakali sana hapa ni tuhakikishe Ilani hii inatekelezwa kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vituo vya afya. Ndio maana mimi nasema Ilani hii naipenda sana, inasema kila mahali tutajenga vituo vya afya, Wilaya ya Kiteto kati ya kata 23 tuna vituo vya afya viwili tu. Kwa hiyo, nafikiri tukija hapa mtuulize Bwana Olelekaita una kata ngapi ambazo hazina vituo vya afya, halafu tufanye mathematics simple, kila mwaka mnatakiwa mnipa ngapi ili baada ya miaka mitano tutekeleze, hivyo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukisema tunapeleka computer kwenye sekondari kadhaa, mimi ninazo 18, kwa hiyo, ningekuja tu hapa nidai computer zangu 18. Labda kitu cha kufanya pia ni kujaribu ku-cost hii Ilani yetu ili tujue tunahitaji gharama ya shilingi ngapi miaka mitano ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi sasa kwa muamko huu ambao umeoneshwa kupitia TAMISEMI wamechanga michango kwa ajili ya vituo vya afya; Dosidosi, Matui, Ndedo, kazi zinaendelea. Kwa hivyo, inatakiwa tu mkono wa Serikali kidogo ili tushirikiane kutekeleza Ilani hii. Kwa hiyo, tuangalie vipaumbele hivi na tutembelee maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mimi nimekwenda kwenye kata moja katika mkutano wa hadhara, kumbe nikagundua wananchi wala hawataki hata ule mkutano wananiambia tu twende tukuoneshe kituo cha afya. Nilivyofika pale ikabidi niseme na mimi kwa Mfuko wa Jimbo nitaweka mkono hapa na nimeshafanya hivyo, lakini sasa pesa ya Serikali, mtuunge mkono ili wananchi wale wajue kwamba wakihangaika Serikali na yenyewe inaweka mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni hati. Walimu wapo wengi sana wanajitolea, wanaomba ajira hizo tena kwa miaka mingi tu. Mimi nilikuwa naongea na Afisa wangu hapa akaniletea karibu majina 100 tu kwa Kiteto na wako walimu wazuri wenye taaluma tena za Kiswahili, mabingwa. Tumepitisha sheria hapa ya kuruhusu Kiswahili sasa kianze kutumika na tuna wataalamu wamejaa wanasubiri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)