Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukushukuru, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya njema hata siku ya leo nikawa sehemu ya wachangiaji kwenye Wizara hii muhimu kwa Taifa letu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwenye eneo ambalo wananchi wa Jimbo la Mlimba wameniagiza niseme hapa halafu baadaye nitazungumza masuala ya kitaifa. Wananchi wa Jimbo la Mlimba wameniagiza nizungumze mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, hoja kuu ni mgawanyo wa miundombinu ya huduma ya afya na elimu kitaifa. Tuna changamoto kubwa sana juu ya mgawanyo wa huduma hizi za elimu na afya kitaifa. Ni kweli hakuna ubishi Wizara hii hasa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa katika ujenzi wa vituo vya afya na kazi kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya sekta ya elimu.
Hata hivyo, swali langu la msingi tufanye tathmini ya kina kitaifa tuone mgawanyo wa huduma hizi, wapo baadhi ya wananchi ukizungumzia habari ya huduma ya afya, ukiwaeleza takwimu ya ujenzi wa vituo vya afya hawaelewi lugha hii. Kwa sababu katika Jimbo zima, mfano naomba nizungumzie Jimbo la Mlimba, jimbo hili lina kata 16, vituo vya afya ni viwili tu. Uzuri wananchi wa Jimbo la Mlimba ni wachapa kazi na kauli mbiu yetu Jimbo la Mlimba ni “tunaanza wenyewe Serikali itatukuta”. Sasa tunaomba kuungwa mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tumeshakamilisha ujenzi wa kituo cha afya, jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI dada yangu Ummy, maombi ya wana Mlimba tunataka tuanze kufungua kile kituo cha afya, tafadhali Mheshimiwa Waziri atuletee Waganga pamoja na wahudumu ili tuanze kufungua.
Mheshimiwa Spika, pia ikimpendeza Mheshimiwa Waziri anavyokuja kuhitimisha bajeti yake siyo mbaya akasema anakwenda kukamilisha kituo kile cha afya. Maadam tumeanza na siku zote unavyotaka kusafiri unaanza kukaa barabarani ndiyo unaomba lift. Kwa hiyo sisi tunaomba lift tusaidie tu tumalizie kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la hii hii sekta ya afya, kwa wahudumu, hebu tufanye tathmini Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, wapo wanaopewa nafasi hizi kwenye ngazi za Halmashauri hawana sifa, sasa tufanye tathmini ya kina halmashauri kwa halmashauri kama kuna mtu anayeshughulika na let’s say Mkuu wa Kituo cha Afya au Mganga Mkuu wa kituo cha afya tuone elimu yake, hebu tufanye tathmini ya kina kitaifa tuone kwa sababu sekta hii ni muhimu na nyeti sana.
Mheshimiwa Spika, labda nieleze tu ikama ya sekta ya afya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, mahitaji ni watumishi takriban 432 waliopo kwa sasa ni 169 unaona disaster hiyo, yaani zaidi ya nusu hawapatikani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atusaidie katika eneo hilo na wananchi wa Mlimba wamenituma hayo.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine niende kwenye suala zima la sekta ya afya kuhusu maboma. Tumeshajenga sisi Mlimba maboma 10 ya zahanati. Tunaomba tumalizie tu, kama tunaanza wenyewe siyo mbaya tukaungwa mkono na Serikali.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la elimu; kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, nitoe tu mfano mathalani elimu ya msingi, mpaka sasa tuna maboma ya madarasa 41. Ushauri wangu hapa kama wametuletea fedha kujenga madarasa, watu wa Mlimba tunaomba sana zile fedha waturuhusu hata kama kwa ajili ya kujenga shule au madarasa tuzitumie kukamilisha maboma haya kwanza, watusaidie sana.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine, ikama ya Walimu wa elimu ya msingi. Mahitaji ni Walimu 1,420, waliopo ni 654 maana yake tuna upungufu wa Walimu takriban 766. Sasa tungeomba maeneo haya yatiliwe mkazo kidogo kwa sababu ni maeneo nyeti sana na kwa mustakabali wa watoto wetu na wanafunzi wanaosoma ndani ya Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine niende upande wa TARURA; yapo mengi yamezungumzwa kuhusu TARURA. Mimi binafsi niseme tu, kwangu Jimbo la Mlimba mnyonge mnyongeni haki yake mpeni na nimwombe Mheshimiwa Waziri, watumishi hawa asiwahamishe ndani ya Jimbo la Mlimba. Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero kwa maana ya Mlimba super, aniachie tufanye naye kazi. Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro super, tauachie tufanye nao kazi. Nitasema baadaye huko kwenye maji maana yake wako wazuri zaidi kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, nijikite kwenye eneo la mgawanyo wa fedha hizi za TARURA. Nilikuwa najaribu kuangalia haraka haraka Jimbo la Mlimba lina kilometa zaidi ya 1,000, tunapata bajeti ya milioni 500 kwa mwaka. Nimeangalia na jirani zangu pale Kilosa kidogo, wao wana kilometa takriban 900 hivi wana bilioni 1.3. Sasa napata tabu kwenye mgawanyo wa hizi fedha, milioni 500 unafanyia nini pale Mlimba, kilometa zaidi 1000. Yaani hata daraja moja halikamiliki. Hebu tuangalie maeneo haya, niombe tu na nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha bajeti yake aeleze ni vigezo gani vinatumika katika mgawanyo wa hizi fedha kwenye halmashauri, nivijue vizuri. Hii itatusaidia pia kupata elimu.
Mheshimiwa Spika, sasa nijikite katika eneo la mapato na hapo kwanza natangaza maslahi na kwa kuwa nimehudumu kwenye Serikali za Mitaa kama Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na tulifanya vizuri sana kwenye mapato, naomba nitoe elimu kidogo kwa ufupi kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, hakuna muujiza kwenye kuziimarisha halmashauri kimapato, jambo la msingi niombe Wizara hebu tufanye tathmini, tuangalie fursa za kila halmashauri, nilivyokuwa Dodoma niliitazama Dodoma Jiji nikaona sina fursa nyingine mbadala zaidi ya ardhi, tukapima Dodoma zaidi ya viwanja 200,000 tukapata fedha na tulikusanya bilioni karibu 73 kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Tukasema hapana hii fedha viwanja siyo sustainable yaani sustainability ya mapato ya viwanja ni ya muda mfupi tu, nikakaa na menejimenti timu yangu tukakubaliana tubuni vyanzo mbadala vya mapato ya ndani, leo tumeacha hoteli kubwa hapa inayojengwa kwa mapato ya ndani bilioni 9.9 inakamilika, ndiyo tunafungua mwezi ujao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Jiji la Dodoma kwa maana ya own source ipo. Ukienda Mji wa Serikali kuna hoteli, kuna apartment, kuna kumbi zinajengwa, mapato ya ndani bilioni 18. Sasa niombe na niseme tu zipo halmashauri zina fursa ya kilimo, wawekeze kwenye kilimo, zipo halmashauri zina fursa kwenye maeneo mengine wawekeze huko, hakuna eneo ambalo halmashauri tunazuiliwa kwa mujibu wa sheria kuwekeza. Tukiendelea kusubiri haya sijui kodi na nini nadhani tuta-mark time kidogo.
Kwa hiyo niombe na sisi pale Mlimba waturuhusu nitamwomba Waziri wa Ardhi baadaye lakini kwa sababu hapa tunazungumza na TAMISEMI, kuna shamba la Serikali la hekta 500 limetelekezwa leo hii almost ni miaka kama mitatu, sisi tutalichukua lile na tutalima kuanzia mwakani. Tutaanza kilimo cha mpunga, tuvune mpunga kama mapato ya ndani, tutalichukua tu sisi maana Serikali haifanyi chochote pale. Kama halmashauri tutalitumia, tutaliwekeza ili tulime kilimo cha mpunga, tuone namna gani tuweze kujikwamua na shughuli za maendeleo Jimbo la Mlimba kupitia kilimo cha mpunga.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme jambo moja tutengeneze clusters ya hizi halmashauri. Huwezi kulinganisha Jiji la Dar es Salaam kwa maana Ilala na Halmashauri ya Mlimba hata kidogo. Kwa hiyo hata fedha za maendeleo tunavyopeleka tuzitengenezee madaraja. Daraja A ni halmashauri zile zote zenye uwezo kwa mapato ya ndani, tuangalie namna gani tunapeleka kwa sababu ukisema mgao wa Ilala uwe sawa na wa Mlimba, tunawaonea haziwezi kuwa sawasawa. Kwa hiyo tuzitengenezee madaraja, kama hawa wana uwezo wa mapato ya ndani, basi ziende fedha chache za maendeleo, wale wenye changamoto kubwa tuwapelekee za kutosha na hili ni tatizo la nchi nzima. Ilala ana zaidi ya bilioni 60 unampelekea fedha za nini, Dodoma Jiji sasa wanakwenda kukusanya bilioni 48, sisemi zinatosha lakini tuangalie namna ya mgawanyo kwa kuzingatia fursa au uwezo wa halmashauri kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo nadhani nitoe mchango wangu ni 10%. Sheria imetungwa na nalipongeza sana Bunge lililopita na nakupongeza na wewe binafsi kwa sababu mlitunga sheria nzuri sana. Tuweke eneo kwenye kanuni au sheria, nadhani kanuni kwenye utekelezaji kwa sababu kanuni ndiyo inatekeleza sheria. Tuweke eneo ambalo halmashauri zenye uwezo mkubwa wa kuchangia 10% zisipeleke fedha kwa sababu tija zile hela tunapopeleka kwa wananchi hazifanyi chochote, tunafanya siasa tu. Dodoma sasa hivi tumepeleka bilioni sita, ziko mtaani, hebu fanya tathmini hizo bilioni sita zimefanya nini? Utaona hamna kitu kwa hiyo kama ni siasa tu. Kwa hiyo halmashauri zenye uwezo wa fedha nyingi ziruhusiwe badala ya kupeleka fedha watengenezewe shughuli yoyote kiuchumi yaani halmashauri iamue kununua kama ni vifaa au namna gani yoyote lakini siyo kupeleka.
Mheshimiwa Spika, kingine kuwe na ukomo wa hizi fedha, leo hii Dodoma kama inatoa zaidi ya bilioni sita, maana yake itafika mahala 10% ni zaidi ya bajeti yake tunapeleka kwa wananchi, kwa hiyo kuwe na ukomo kwa halmashauri kubwa kwamba sasa ifikie mahali kama utachangia 10% mpaka bilioni 30 i-stop, zile changa ziendelee kwa sababu wakati inatungwa sheria hii hatukutathmini kwa kina uwezo wa halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache niliyochangia, nadhani yatasaidia Wizara yetu, lakini nimwombe anapokuja kuhitimisha bajeti yake, haya niliyomwomba ayaseme na niyasikie na wananchi wa Mlimba roho zao zitapona. Ahsante sana. (Makofi)