Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia leo humu Bungeni.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, nianze kumshukuru Mungu kwa kunijalia leo kuongea hapa ikiwa ni kipindi changu cha nne. Pia niwashukuru walionileta hapa, wapiga kura wangu wa Mkoa wa Shinyanga nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwape pole Wabunge wote, nafahamu kwa mujibu wa Kanuni pole zilishatolewa lakini kuna kitu kinaniambia kwamba nirudie kuwapa pole Wabunge wote kwa msiba mkubwa uliotokea wa kiongozi wetu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa, naomba kumpogeza Mheshimiwa Waziri, Ummy Mwalimu sina shaka naye, najua ni mfuatiliaji, ni mtu wa vitendo zaidi na nafahamu kwamba yale yote ambayo sisi kama Wabunge tuna kiu nayo ana uwezo nayo. Hongera sana Mheshimiwa Ummy. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini maendeleo yoyote yale kwenye Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hayataweza kufikiwa ikiwa hakutakuwa na umoja na mshikamano kuanzia juu mpaka chini, kwenye ngazi za Mikoa maana Wizara hii inagusa kuanzia Mikoa, Wilaya mpaka kule chini kabisa kwenye Kijiji. Lipo jambo ambalo jana Mheshimiwa Rais amelisema, kwa nafsi yangu siwezi kuliacha likapita kimya kimya. Mheshimiwa Rais alisema kwamba humu ndani Bungeni mwenendo wetu lazima tuuangalie. Kauli ile unaweza kuiona kama ndogo fulani hivi lakini vipo vitu ambavyo vinatusababishia humu ndani kukosa umoja na mshikamano.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba wapo watu tena ni wengi, ambao mtu akipinga anapinga kutoka moyoni na mtu akiunga mkono bila kungalia vyama, kuna mtu anaweza akawa yupo chama kingine wala siyo CCM, lakini akisema jambo akikosoa au akipinga anapinga kutoka moyoni. Mimi naomba niwaelezee Waheshimiwa Wabunge kuhusu uzoefu wangu wa humu ndani, kidogo tu, miaka niliyokaa wala sio mingi kiasi hicho. Mimi ambacho nakiona lipo kundi la watu ambalo wao wanataka wamchomoe Mheshimiwa Samia kutoka kwenye utawala wa Magufuli kama vile hakuwepo. Kundi hili kazi yake wanakaa, wengine wanamsifia kwa nia njema kweli kama kumsifia lakini wengine wanamsifia kwa maana ya kudhoofisha legacy ya Magufuli. Jambo hilo hatuwezi kulikubali hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini lipo kundi lingine ambalo wao tunatofautiana yaani kila siku tangu Magufuli alivyokuwa yupo madarakani wao ni kumpinga Magufuli. Leo mtu yule yule anasimama anasema, Mheshimiwa Samia nakupongeza sana bora umekuja wewe na mtu yule hata alivyokuwa Magufuli alikuwa anapinga sana leo ukimpongeza Mheshimiwa Samia kuna ajenda za siri. Mimi naomba kusema mkakati wenu tunaujua na mfunge midomo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu Samia na hapa naomba pia niseme inatakiwa sisi tusimame kwa nguvu moja kwa haya mambo ambayo yanayotokea na tuseme hapana. Lazima tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo na siyo kumuunga mkono kwa kuzungumza humu ndani Bungeni, tumuunge mkono hata huko nje ambako tunatoka. Hiki kinachofanyika ni kumchonganisha Rais wetu Samia na umati wa watu kule nyuma. Mheshimiwa Rais Magufuli alikuwa na watu wake ambao walikuwa wanampenda na kumtegemea leo unaposimama unasema kwamba wewe ulikuwa unampinga Magufuli halafu unaamua makusudi kabisa kwa mkakati ambao mmekaa huko uchochoroni mmeupanga mnaanza kusema kwamba sisi tulikuwa tunampinga Magufuli tuanze kumsifia Samia sio jambo la sawasawa. Huu mkakati naomba niwaambie utafeli kwa sababu Mheshimiwa Samia hana kundi hata moja, Mheshimiwa Samia hajajiunga na mtu yeyote, Mheshimiwa Samia nafasi aliyonayo ni Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu gani? Mambo kama haya yaliwahi kutokea mwaka 2016/2017 wapo watu ambao ndiyo hawahawa yaani kila siku ni hawa hawa, kwanza najiuliza hivi ninyi ni akina nani kwa sababu kila siku huwa ni hawa hawa wenye maneno, makelele. Mimi nilikuwa natamani siku moja nimwambie Rais hata Mheshimiwa Samia kwamba hawa watu wakipewa vyeo siku wakiondolewa mtuambie sababu.
Nasema hivi kwa sababu wakati mwingine mtu anafanya mambo ya ajabu lakini mkija kuangalia mambo yake huko mengine yanatia aibu na yalikuwa ni mabaya lakini ukisamama hapa sasa hili ni Bunge jipya Wabunge wengine wapya wanatuuliza sisi ambao kidogo wa zamani jamani Mheshimiwa Mbunge …
SPIKA: Mheshimwa Lucy sasa turudi kwenye bajeti. (Makofi/Vigelegele)
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ujumbe umefika na umekuwa delivered. Cha msingi ni kwamba naomba sisi tuache hayo mambo ya ajabu, tukae kwenye mstari tumuunge mkono Rais wetu kwa asilimia 100 na kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu TAMISEMI, kama nilivyoeleza hapo awali najua uwezo wa Mheshimiwa Waziri wetu. Ripoti ya CAG imeeleza bayana kwamba yapo mambo ambayo yamekuwa yakifanyika huko kwa Wakurugenzi bila kusema ni wa maeneo gani lakini kwa kweli hayaridhishi. Naomba Mheshimiwa Waziri ashuke kule chini aende akafanye kazi hii kwa vitendo. Kwa kuwa najua kwa uwezo wako utafanya kazi hii kwa vitendo, ile field aliyokuwa anaifanya alipokuwa Wizara ya Afya naomba aende pia field kwenye Wizara hii kwa sababu yapo maeneo ambayo watu wanalalamika sana, matatizo ni mengi, watu wanajichukulia sheria mkononi. Utawala huu kwenye Serikali za Mitaa kuna baadhi ya maeneo huko vijijini kwenye kata na kadhalika na hasa kwenye Mabaraza ya Ardhi, naomba Wizara hii ya TAMISEMI iweze kuwa na mkakati maalumu yale mambo ambayo yanazungumzwa kwenye masuala ya ardhi na kadhalika ambayo yanahusu Wizara hii yaweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile kwa kuwa Waziri ametoka Wizara ya Afya najua Wizara hii ya TAMISEMI inahusika pia mambo ya afya, naomba afuatilie kuhusu matumizi ya pesa za Serikali zinazoshushwa kule chini. Pesa nyingi sana zinashushwa kule chini lakini tija inaonekana kwa kiwango fulani cha kawaida lakini kwa kiwango kikubwa upigaji unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)