Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi. Niungane na wasemaji waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu, lakini pia Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Dugange kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na niwapongeze pia kwa kumpata Katibu Mkuu mzuri Profesa Shemdoe.

Mheshimiwa Spika, nataka nijielekeze katika maeneo machache ya kushauri ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na hasa yenyewe ikiwa ni kiungo kikubwa katika kuwafikia wananchi maana yake kutekeleza sera na miradi mbalimbali kwa wananchi wetu. Nianze na utayari wa kazi na ari ya kazi ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama Taifa. Mojawapo ya sifa ya kiongozi mwema ni kuweza kutambua upungufu au mahitaji halisi ya watendaji kazi wake ambao wanategemea waweze kutekeleza sera na miradi mahsusi mbalimbali ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sifa nyingine ya pili ni kuweza kuwapa motivation, maana yake kuwaamini na kuwatambua. Nimekuwa nikiongelea hili suala mara kwa mara na leo limepata wizara yenyewe inayohusika. Eneo la halmashauri nikimaanisha Wakurugenzi wa Serikali za Mitaa na Wakuu wa Idara, nisikitike kusema kwamba imekuwa ni kama punching box ya viongozi wa aina mbalimbali, viongozi wa ngazi mbalimbali kuwa kundi hili la watendaji ambao tunawategemea kufanya kazi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia mazingira wanayofanyia kazi hawastahili kuhukumiwa kama wanavyohukumiwa. Mheshimiwa Ummy Mwalimu amefanya kazi ya Uwaziri katika Wizara mbalimbali kwote alikotoka ameacha alama na watu wanamkumbuka, nimwombe sana katika michango tunayoitoa hapa aipokee, aitafakari na akaifanyie kazi kule. Wale watu wanafanya kazi usiku na mchana, watu hawalali wanatekeleza miradi. Haya anayoyasikia tunayasema humu mengine ni kweli yana ukweli wake, lakini wachache hawawezi kufanya wote waonekane kwamba hawafai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana baada ya kipindi chake cha bajeti atenge muda wake, bahati nzuri amepata viongozi wazuri Profesa Shemdoe ni tunda la U-DED, Dugange huyu amekuwa DMO na amekuwa RMO, anajua mazingira mazima kwenye halmashauri. Mheshimiwa Silinde anajua, akaa nao aangalie mapungufu waliyonayo, akiwa-console matokeo makubwa ndani ya TAMISEMI atayaona, lakini tukikaa kuwanyooshea kidole, kila anayesimama Mkurugenzi, Mkurugenzi wengine hatujajifunza taratibu za uendeshaji wa halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea haya nilikuwa Mkurugenzi na nimetoka hapa naingia hapa Bungeni, lakini mazingira yaliyopo kule kama tungekuwa tunapima job weight inawezekana Wakurugenzi wangekuwa kati ya watu wanaofanya kazi nyingi ndani ya Taifa hili, kuliko watu wengine, lakini ni kwa sababu ni kundi ambalo halisemewi, kila mtu anawageuza wale ni punching box, hivyo niombe auchukue ushauri wangu aufanyie kazi. Wale wachache ambao ni kweli wameshindikana, tutawachukulia wameshindikana, lakini wale learned brothers and sisters wanafanya kazi kwa weledi, naomba wawatumie wafanye kazi tutekeleze miradi kule chini.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili, ni upande wa afya. Naomba niipongeze TAMISEMI kwa kazi nzuri ambayo wamefanya hasa katika eneo la afya. Tunaona tumejenga hospitali nyingi katika kipindi hiki, tumejenga vituo vya afya, tumejenga zahanati. Haya mambo yamewezekana kwa sababu ya usimamizi mzuri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo niombe tu tuendelee na speed kubwa ya kuweza kuboresha. Katika eneo hili naomba nishauri, nimesoma randama ya Fungu 56, kuna fedha ambazo Serikali wanazipata kutoka kwa wafadhili za Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Sector Basket Fund).

Mheshimiwa Spika, mwaka jana fedha hizi kutoka kwa wafadhili zilichelewa fourteen point something billion, tukafunga mwaka tunazo, lakini mpaka leo hizo hela bado hazijaingia kwenye mfumo kwenda kufanya kazi kule. Fedha hizi ni za muhimu sana kuweza kuongeza nguvu kwa fedha zinazotokana na Serikali kwa ajili ya kununua dawa, kununua vifaa tiba, chanjo lakini na supervision kule chini, lakini mpaka mwezi Februari kwa ripoti ya TAMISEMI hizi fedha fourteen point one billion bado hazijaenda.

Mheshimiwa Spika, suala hili sio la TAMISEMI kwa sababu sisi tunashauri Serikali na Serikali ni moja tuiombe Wizara ya Fedha masuala haya ya kutopata vibali vya matumizi ya fedha yamekuwa ni mengi. Serikali yetu yenyewe inaweza ikawekea checks and balance yenyewe kwamba fedha zikija nje ya muda kuna jinsi ambavyo wanaweza wakaingia kwenye bajeti wakazipa vibali. Haya tumeyaona sio kwa TAMISEMI peke yake hata kwenye fedha za barabara tumeona hapa zilikuwa zimechelewa sana, wakandarasi, Wizara ya Ujenzi wakawa wamesimama kazi. Kwa hiyo naomba kushauri kwamba hizi fedha ni za msingi najua TAMISEMI inawezekana wanakimbizana kuomba vibali ili waweze kuhakikisha kwamba zinaingia katika mfumo na zinafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa tatu ni kwenye force account. Nchi hii imepiga hatua ndani ya miaka mitano kwa utaratibu mzuri wa force account ambao tumeutumia katika miradi mbalimbali, lakini tumepata michango mingi kutoka kwa Waheshimiwa wengine. Eneo hili lina mapungufu kidogo na hasa upungufu kidogo na hasa kama walivyosema ni kwa upande wa wataalam.

Mheshimiwa Spika, tumeanzisha TARURA ma-engineer wote tumewachukua tumewapeleka TARURA, kwa kweli mimi niombe hatuhitaji kuwa na majengo ambayo lifespan yake itakuwa ni chini ya miaka mitano baada ya miaka mitano unakuta jengo linapasuka, lote linaharibika. Niwaombe sana TAMISEMI Waheshimiwa Wabunge wengine wametangulia kulisema, tujitahidi tupate Wahandisi wawe stationed moja kwa moja kwa Wakurugenzi, wale wanaoazimwa TARURA ikitokea kazi ya TARURA wanaacha ile kazi ambayo ni ya msingi ipo pale. Najua eneo hili kwa force account tutaendelea kusonga mbele, tuombe basi tuongezewe watalaam.

Mheshimiwa Spika, suala lingine nishauri kwenye suala la TARURA. Najua kuna formula ambayo wanaitumia TARURA kuweza kupata fedha ndani ya wilaya fulani, lakini kuna vigezo vingine nahisi hatuvipi kipaumbele. Ukiangalia Mkoa wa Kagera ni Mkoa ambao kwanza una mvua nyingi katika kipindi kizima cha mwaka, karibu asilimia 75, lakini sehemu hiyo imejaa mito, imejaa maziwa kila sehemu kuna maji na water table ipo juu sana. Sasa tukipewa bajeti sawa na eneo lingine ambalo kimsingi lina hali conducive kwa barabara hatuwezi kulingana, hizo barabara ndani ya muda mfupi zinaharibika.

Kwa hiyo niombe sana kupitia Ofisi yetu ya Rais, TAMISEMI wauangalie kwa jicho la pekee Mkoa wa Kagera na specifically Wilaya ya Misenyi. Tunao mtandao wa barabara kilometa 921, tunapopata milioni 700, hata ile formula ambayo wanapiga kilometa moja kwa milioni mbili haitoshi. Kwa hiyo niombe sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo, nakushukuru kwa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)