Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni ufunguo wa maisha, pia elimu ni bahari na haina mwisho. Hivyo elimu ni muhimu sana katika maisha yote na ya kila mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu kuna changamoto zake zikiwemo za taaluma yenyewe na wanaotoa taaluma hiyo. Nazo ni kama ifuatavyo:-
(1) Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa vitabu vya kufundishia. Hili ni tatizo mojawapo katika sekta hii na suala ambalo linakatisha tamaa kuwa tunataka wanafunzi wafaulu lakini hatuna vifaa vya kuwawezesha kufaulu.
(2) Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa maabara. Hili nalo ni tatizo kubwa katika Sekta ya Elimu. Hii inasababisha hata kutokuwa na Walimu wa sayansi, kwani mambo mengi tunasoma kwa theory kuliko practical, kwa mfano skuli au vyuo havina maabara z kutosha.
(3) Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala mibovu. Pia hili linachangia elimu kuzorota na hatutafika tunakotaka kufika katika elimu na hata katika Tanzania ya viwanda.
(4) Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mfumo wetu wa elimu ni mbovu. Wenzetu wamefanikiwa katika nchi zao kwa kuipa kipaumbele elimu, hali hiyo inatokana na kuijengea mfumo mzuri kwa kuwafundisha wanafunzi wao fani maalum wakiwa wadogo na wakubwa yaani primary hadi vyuo vikuu. Mfano, wanafunzi “x” wanasomea fani ya ufundi kulingana na kipawa chao na “y” wanasomea fani ya unesi kuanzia mwanzo wa masomo yake hadi mwisho. Leo hii katika Taifa letu tumeifanya elimu kama mzigo wa masomo mengi na kupelekea wengi kukatisha njiani au kusoma kwa kukariri zaidi ile nyanja kuliko kufahamu ili aweze kupata kufaulu tu. Hivyo, huwa tunapata wanafunzi ambao si wafanisi bali ni waigizaji tu, hivyo Serikali izingatie ushauri wetu kwa uzalendo wa Taifa letu.
(5) Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu hawana makazi bora; hivyo Serikali iwajengee Walimu makazi kama inavyofanya kwenye sekta nyingine, mfano, Sekta ya Ulinzi, Sekta ya Jeshi la Taifa na sekta nyingine.
(6) Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wapewe posho za kuwakidhi mahitaji yao kama usafiri na uhamisho kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna changamoto katika Sekta ya Elimu katika Taasisi ya Mikopo kama ifuatavyo:-
(1) Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwafikii walengwa, kama tunavyoelewa kanuni ya mikopo iliwekwa kwa wale wasiojiweza kupata elimu hususan maskini, lakini la kushangaza wanaofaidika zaidi ni watoto wa vigogo kama vile Mawaziri, Wabunge, Maafisa na wengine na kupewa mikopo kwa asilimia 100, lakini wale walengwa hupewa wachache tena kwa asilimia chache kwa mfano asilimia 40, 30, 20 na hata asilimia 10 na wengine kukosa na kushindwa kuendeleza masomo yao.
(2) Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mikopo haifiki kwa wakati na badala yake wanafunzi wanadhalilika kwa kujiuza, kuwa ombaomba kwani huwa wako mbali na familia na hata familia zao zinashindwa kuwasaidia kutokana na hali zao za ugumu wa maisha.
(3) Mheshimiwa Mwenyekiti, kutorejeshwa kwa mikopo hii; Serikali na Wizara ya Elimu hawajajipanga wala hakuna kanuni inayosimamia haya. Kwa mfano, wanafunzi wengi wanaona ni takrima ama hisani imepewa tu jina la mkopo na ndiyo maana toka waajiriwe hawajakatwa hata siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu kwa upande wa Zanzibar, ni mgagaisho mtupu; hatutofautishi elimu ya juu ni ipi na elimu ya sekondari kwani wanafunzi wa O Level na A Level wanafanya mitihani kutoka Tanzania Bara wakati suala hili ni la Zanzibar. Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inapora madaraka ya Serikali ya Zanzibar? Naomba majibu kwenye hili; kama ni suala la Muungano mbona haiwaajiri Walimu hawa kwa Jamhuri ya Muungano na wanaajiriwa na Serikali ya Zanzibar na hawalipwi sawa na Jamhuri ya Muungano wakati wanafanya kazi za Jamhuri ya Muungano isipokuwa kusimamia mitihani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.