Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni ya leo niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. Awali ya yote, napenda kuwapongeza dada yangu Ummy na timu yake wanafanya kazi nzuri na tuna imani nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja, nitaanza kujikita kwenye suala la afya. Afya ndiyo mtaji wa mwanadamu wa aina yoyote lakini suala hili kwa baadhi ya maeneo linaonekana kama halipewi kipaumbele cha hali ya juu. Mfano nikiangalia katika Jimbo langu huwa naliita Burundi kwa sababu linahudumia asilimia kubwa ya wananchi waliotoka Burundi lakini lina jumla ya Kata 15 lakini ndani ya hizo kituo cha afya ni kimoja tu. Hali hii inasababisha msongamano mkubwa sana wa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali kwenda kutibiwa kwenye kituo hicho hali inayowafanya mpaka wahudumu kuzingirwa na wagonjwa. Pia wagonjwa wanaweza wakafa pale pale kwa sababu wanasubiri huduma kwa muda mrefu na wengine kujifungulia njiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali kwa maeneo ya pembezoni hebu tuyape kipaumbele na kuona na yenyewe yanafaa kupatiwa huduma za afya kama zahanati na vituo vya afya. Jimboni kwangu kuna kituo kimoja tu lakini kuna vituo viwili vya afya mfano Kituo cha Uyoo na Mwongozo tayari vimeshaanza kujengwa na vimefikia hatua za mwisho. Niiombe Serikali iweze kupeleka fedha kwenye vituo hivyo viweze kumalizika na vianze kufanya kazi kuwahudumia hawa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine kwenye afya hapo hapo ni bima iliyoboreshwa. Suala la bima iliyoboreshwa naona kama haiwasaidii wananchi wetu kwa sababu walivyokuwa wanakata waliona kwamba itakuwa ni suluhisho na mbadala pindi wanapokuwa hawana pesa lakini wanapokwenda kwenye hivi vituo vyetu vya afya wakifika pale, mfano kama vituo vya afya na zahanati nyingi hazina hata maabara, kwa hiyo akifika pale inamlazimu aende kwenye zahanati zingine au mahali pengine kwenda kupima ambapo inamuongezea gharama, kwa hiyo, hii bima inakuwa kama vile haina faida. Vilevile ana bima anakwenda kwenye zahanati hakuna dawa anatakiwa anunue. Tunakwenda kuanzisha bima ya afya kwa wote hivyo kabla hatujaanzisha niombe Serikali ifanye tathmini, je, hii bima ya afya iliyoboreshwa imesaidia kwa kiasi gani kabla ya kuingia kwenye hii bima ya afya mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye sekta ya elimu. Kiukweli elimu bado kwenye maeneo yetu ni changamoto kubwa sana. Miundombinu ya elimu kama madawati, madarasa, matundu ya vyoo bado hayatoshelezi. Cha ajabu tunapongeza Serikali imeanzisha mifumo mingi sana ya kupata taarifa lakini hazitumiki. Leo ikifika mwisho wa mwaka Waziri Mkuu anaanza kupiga kelele madarasa; hivi haya maoteo na hizi takwimu ambazo mnazikusanya kila mahali mnazitumia kwa shughuli gani kiasi kwamba tunafanya haya mambo ni kama vile dharura. Niiombe Serikali mifumo iliyoianzisha basi itumike kusaidia mambo yasifanyike kwa ghafla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni masharti ya uhamisho. Mtumishi kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni suala la kawaida na lipo kisheria na anapokwenda kuhamia sehemu nyingine ana sababu ambazo yeye zinamfanya mpaka ahamie kule lakini masharti ya uhamisho sasa hivi yamekuwa magumu mno. Leo mtu anaambiwa kuhama kituo kimoja kwenda kituo kingine mpaka apate mtu wa kubadilishana naye, anamtoa wapi? Unakuta watu wengine mfano wa vijijini; shule nyingi za vijijini kule watumishi wengi ni wanaume wanataka wafuate wake zao au wanawake wafuate waume zao, inafikia wakati kama walimu wanaamua kutumia watoto wetu kujipoza. Hali hii kweli ni mbaya, inawaingiza watu kwenye majaribu makubwa, wanaume wanajiingiza kwenye mambo ambayo hayafai, ndoa zinavunjika na wanafunzi wetu tunawaingiza katika mtego mkubwa wa kufanya mapenzi na walimu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni TARURA. Kiukweli TARURA bado ni changamoto, barabara zetu huko vijijini hazipitiki. Niombe TARURA basi iongezewe bajeti lakini tofauti na hapo TARURA izilazimishe Halmashauri kama nilivyoongea Bunge lililopita ziweze kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuongeza bajeti ya TARURA ili iweze kuhudumia barabara kwa kiwango kinachotakiwa. Unakuta sasa hivi TARURA kwanza hawashirikishi hata Madiwani au Wabunge, unaambiwa barabara yako hii itatengenezwa bila hata wewe Mbunge au Diwani kushirikishwa wakati wewe Diwani au Mbunge ndiyo unajua barabara zipi zina changamoto na barabara zipi zina manufaa kwa ajili wananchi wetu. Nimuombe Waziri awaambie TARURA waweze kushirikisha Madiwani na Wabunge kwenye upangaji wa ujenzi wa hizi barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kwenye mgawanyo hizi asilimia 10 za vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Hizi pesa kwa kiasi kikubwa sana zinakwenda kwa vikundi ambavyo vinakuwa vinarejesha lakini vile ambavyo vinaonekana vinasuasua bado havipewi kipaumbele. Nina maana kwamba tunakwenda kwa kuangalia vile vinavyorejesha lakini hatujui ni changamoto gani zinasababisha hao wengine wasirejeshe ili watu wengine wapate. Hivyo niombe sasa kwenye vikundi ambavyo vinakuwa labda havirejeshi ile pesa ambayo inapangwa kwa ajili ya kwenda kufanya ufuatiliaji ifanye kazi ikiwa ni pamoja na kujua changamoto ambazo wanapitia hivi vikundi ambavyo vinashindwa kurejesha ili waweze kuwasaidia kwa sababu lengo ni kuwafanya hawa wananchi waweze kujikwamua kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni nyongeza ya mishahara. Watumishi wetu ndani ya miaka mitano hawajapata nyongeza yoyote ya mishahara. Ndugu zangu hata sisi humu ni watumishi wa Serikali lakini ndani ya miaka mitano kweli hata kanyongeza kidogo! Jamani maisha sasa hivi yamekuwa magumu na vitu vimepanda bei. Nyongeza ya mshahara inamfanya huyu mtumishi apate morale ya kufanya kazi lakini kama hawa watu wananung’unika wanakwenda kutafuta vyanzo vingine mpaka walimu wanakuwa bodaboda, hebu mwaka huu tuwaongeze za mshahara. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)