Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza kabisa, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuaminiwa na kupewa dhamana hii kubwa pamoja na Naibu Mawaziri wa Wizara hiyo, watendaji bila kusahau Kamati ya Bunge iliyohusika na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado imeendelea kuwa na vipaumbele vyake katika kuwahudumia Watanzania. Moja ya kipaumbele cha Serikali katika kuwahudumia Watanzania ni kuhakikisha Watanzania wote ikiwezekana wanapata matibabu kwa kutumia mifuko ya bima ya afya hasa wale ambao wako katika sekta ambazo siyo rasmi, kwa maana ya wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo wadogo, bodaboda, mama ntilie na kadhalika, watu hawa ndiyo wako wengi kwenye jamii yetu, makundi haya ni zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali ikaja na wazo zuri sana katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuanzisha huu Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ulioboreshwa. Mfuko huu umekuja kwa nia njema sana, una muundo mzuri, una watendaji na wasimamizi kuanzia ngazi ya mkoa mpaka ngazi ya kijiji na mtaa. Nia ya mfuko huu ilikuwa kuhakikisha wanachama wote hawa wanapatiwa huduma za msingi za jamii kwa maana ya kupata ushauri wa daktari, kupima vipimo maabara, kupata dawa zile za msingi kwenye ngazi husika kama ni zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya na mkoa tunaita essential drugs katika kituo husika, pia huduma ya mama na mtoto. Pia kutokana na kituo cha huduma ya afya kwa mfano kwenye zahanati atapata mapumziko, kwenye kituo cha afya atalazwa na upasuaji mdogo, kwenye hospitali ya wilaya atapata upasuaji mkubwa na mdogo pia ila kwenye hospitali ya mkoa atapata vyote pamoja na huduma zote za rufaa ambazo zimethibitishwa katika huduma za mfuko huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto katika kupita kwetu, watanisaidia Waheshimiwa Wabunge; kwenye kampeni zetu kule vijijini akitokea mtu kuchangia suala la afya, kama hajachangia changamoto za mfuko huu; na akichangia changamoto za mfuko huu anapokewa na wanachama wote au Wajumbe wote kwenye Mkutano husika, kuona jinsi ambavyo changamoto ni kubwa. Wanasema, Mheshimiwa uliyesimama hapo tunakuheshimu, kama wanakuheshimu watakwambia hivyo. Mimi nakwenda hospitali nakosa hata Paracetamol japo ya kunishusha homa nikajipange kutafuta fedha kununua hiyo dawa ambayo haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, changamoto ni kwamba wale wale wanachama wetu wa mfuko huu ndio wamekuwa wahamasishaji wakubwa wa kuwatangazia wenzao wasijiunge na mfuko huu, lakini siyo kosa lao ni kwa sababu ya upungufu uliopo kwenye huduma zinazopatikana kwenye mfuko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine, unapokwenda kwenye kituo cha afya, unajaziwa Form C2, inaitwa kwenda kutafuta dawa kwenye pharmacy nyingine, pale imekosekana. Kuna tatizo; ukiangalia ile form yao, ile dawa inaweza ikawa labda ni ya shilingi 5,000, lakini ukienda kwenye pharmacy nyingine ambayo zimesajiliwa anakujazia form, lakini ile dawa anaandika shilingi 15,000.

Kwa hiyo, mfuko utaendelea kupwaya kwa sababu utawanufaidisha watu wengine. Kwa hiyo, iundwe mamlaka ya kudhibiti na kusimamia suala la madawa kwenye mfuko huu, tunapigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine, uhamasishaji wa wananchi kujiunga na mfuko huu, sasa uendane na upatikanaji wa huduma ambazo nimezitaja, kwa sababu hatuwezi kupata nguvu sisi wanasiasa na vyombo husika kwenye ngazi husika kuwashauri watu wajiunge, wakati tukisema kiukweli, hizi huduma hazipatikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tunajua Serikali inaendelea kuchangia sawa sawa na wanachama wanaochangia pamoja na wadau, wanaita tele kwa tele. Kwa hiyo, ina maana fedha ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niieleze Serikali, katika muundo uliowekwa ambao ni mzuri tu, kutoka ngazi ya mkoa mpaka Kijiji, wajiwekee malengo angalu ya miezi miezi mitatu mitatu tu, halafu wajifanyie tathmini. Hii itaongeza uwajibikaji na commitment. Kwa hiyo, huu mfuko badala ya kuwa wa hasara na watu kuvunjika moyo, utawasaidia kama ilivyokuwa lengo la kwanza la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri hivyo, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)