Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara napenda kuanza kuwashukuru viongozi wa TAMISEMI kwa kuweza kuidhinisha mafungu mbalimbali ya fedha ambayo tayari yameshafika kwenye Jimbo langu la Ngara. Mathalani naomba niwashukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa David Silinde, Mheshimiwa Dugange na Dkt. Riziki Shemdoe.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miezi michache iliyopita, Jimbo langu la Ngara limepokea mafungu mbalimbali ya fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya aina mbalimbali kwenye vituo vya afya, shule za sekondari, na kwenye shule za misingi. Nawashukuru sana kwa kuweza kutupatia fedha sisi wananchi wa Jimbo la Ngara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwa watumishi. Watumishi hasa Walimu pamoja na wale wa kada ya afya wana changamoto nyingi sana mtambuka ambazo wamekuwa wakiishi nazo kwa muda mrefu. Kuna malipo call allowance wanayotakiwa kulipwa watumishi wa kada ya afya, kwenye Jimbo langu la Ngara, kuna watumishi wana miaka nane mpaka kumi na zaidi hawajalipwa hii fedha inayoitwa call allowance, wanaishi kwenye mazingira magumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Walimu, kama ambavyo wenzangu wamechangia, kwenye Jimbo langu la Ngara, Walimu wana changamoto nyingi sana, Walimu wanadai kupandishwa madaraja, wanadai malimbikizo ya uhamisho pamoja na allowances za matibabu, hawajalipwa kwa muda mrefu. Kama kuna watu wako hoi, basi ni hawa watumishi na uhoi wenyewe unatofautiana. Kuna mtu yuko hoi anaumwa anameza Panadol, mwingine ni hoi yuko ICU na mwingine yuko kabisa kwenye vitu vingine. Hawa wako hoi, naombeni sana TAMISEMI wa-coordinate na watu wa utumishi ili Ngara tupate kibali cha kupandisha vyeo. Toka mwaka 2008 hatujapata kibali ambacho tumeshakiomba mpaka sasa. Kwa hiyo hawajapandishwa madaraja toka mwaka 2008, 2009, 2020 na sasa ni 2021. Napenda kuiomba TAMISEMI wa-coordinate na watu wa utumishi ili tuweze kupata vibali angalau kwa kuanzia kibali cha mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kinaitwa Bodi ya Walimu kama kuna kitu kinaenda kutuvuruga Tanzania ni hii inaitwa Bodi ya Walimu. Walimu wana makato ya aina mbalimbali mpaka sasa kwenye mishahara yao. Sasa tupo hapa kuna kitu kinaendelea huko TAMISEMI, wanatengeneza Bodi ya Walimu na inakuja na sheria inayotaka walimu wawe wanakatwa fedha kila mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna jambo walimu hawataki kulisikia ni hili hapa la kuja na sheria inayotaka walimu wakatwe fedha na kila mwezi hela yao iondolewe. Kwanza mishahara yenyewe ni midogo, halafu tunataka tena kuwakata hela. Hilo jambo litaleta vurugu, halikubaliki walimu kwenye jimbo langu wamesema hawataki kusikia kitu kingine kipya kitakachokuwa na madhara ya kukata fedha zao kwenye mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu, hasa ya shule za sekondari na msingi; Jimbo langu la Ngara lina changamoto kubwa hasa katika upande wa matundu ya vyoo. Mathalani, shule za sekondari zina upungufu wa matundu 132, ukiangalia hapa maana yake wanafunzi 2,640 hawana mahali pakujisaidia. Ninaomba sana TAMISEMI watakapokuja wana-consolidate michango yetu basi Ngara watuongezee matundu ya vyoo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa nyumba za walimu, tuna upungufu wa nyumba za walimu 344. Maana yake ni kwamba walimu wenye familia ya watu watano, zaidi ya watu 1,720 wanaishi katika mazingira yasiyoeleweka eleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa upungufu wa walimu, tuna upungufu wa walimu 197; maana yake ni kwamba inapotokea fursa ya kuajiri walimu wapya kwa upande wa Jimbo la Ngara, wachukue walimu wawaambie waingie kwenye vyumba vya madarasa. Vyumba vya madarasa viwili vikijaa wafunge mlango halafu hao wote watuletee kwenye Jimbo la Ngara.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa walimu 197 ni sawasawa na madarasa mawili yaliyojaa wlaimu. Ninaomba sana, ninawaomba TAMISEMI itakapotokea fursa ya kuajiri walimu wapya basi Ngara watuletee idadi ya walimu wanaolingana na madarasa mawili yaliyojaa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa afya sera ya afya inasema kila kijiji kiwe na zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya. Nina upungufu wa vituo vya afya 17, nina upungufu wa zahanati 29; maana yake ni kwamba upungufu wa zahanati 29 unasababisha watu 72,000 wakose mahali pakwenda kupata huduma za afya. Ninaomba sana TAMISEMI watakapokuja ku-consolidate angalau Ngara waniongezee vituo vitatu vipya vya afya. Hizo ni zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vituo vya afya, ninaomba sana kwasababu tuna upungufu wa vituo vya afya 17 ambapo watu 340,000 hawana mahali pauhakika pakwenda kupata huduma za afya kutokana na ukosefu wa vituo vya afya. Ninaomba angalau TAMISEMI watuongezee vituo vya afya angalau vitatu katika mwaka huu wa fedha ili kuweza kuondokana na changamoto za eneo hili la miundombinu ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa TARURA; kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwenye michango ya nyuma, TARURA inahitaji ongezeko la bajeti, hili halina mjadala. Kwa upande wa Jimbo langu la Ngara, TARURA wamekuwa wakipewa ukomo wa bajeti unaolingana kwa miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba kwa Jimbo langu la Ngara tuna madaraja, tuna makalavati 652 na fedha tunayopewa ni ya kutengeneza kalavati 15 kwa mwaka; maana yake ni kwamba tunahitaji miaka 43 kuweza kujenga makalavati ya Jimbo la Ngara, a good 43 years! Ina maana kwamba hili jambo halikubaliki, ninawaomba sana waweze kutu-consider. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)