Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha sisi sote kukutana kwenye ukumbi huu tukiwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kuzungumzia issue ya elimu kwa sababu ni mwalimu na nina interest kubwa sana kwenye elimu. Tumekuwa tukizungumza suala la miundombinu ya elimu kwa maana kuanzia Shule ya Msingi mpaka Kitado cha Sita kwa TAMISEMI. Pia tumekuwa tukizungumzia uhaba wa nyumba za walimu, hilo linajukana hivyo Serikali tunawaomba mwendelee kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mtwara. Changamoto kubwa ninayoiona kwenye Mkoa wetu ni kwamba kuna baadhi ya maeneo upungufu wa walimu hali yake inatisha. Inatisha kwa maana ipi? Unakuta shule moja ina walimu wawili au watatu. Ukimwuliza Afisa Elimu, anasema, sisi tunagawa walimu kulingana na idadi ya wanafunzi; mwalimu mmoja wanafunzi 45, sawa. Kwa mfano, shule ina wanafunzi 90, maana yake unapeleka walimu wawili. Sasa wakati unapeleka walimu wawili ujue wale watoto kuanzia Chekechekea au kuanzia Awali mpaka Darasa la Saba wanasoma masomo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hao walimu wawili, maana yake pale una Mkuu wa Shule, una Makamu wa Mkuu wa Shule, hapo anatakiwa atokee Mtaaluma, atokee mtu wa nidhamu, atokee mtu wa mazingira, apatikane Mwalimu wa Zamu; hawa walimu wawili, pata picha wanajigawaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, hao hao walimu wawili, Mkuu wa Shule kila siku anaitwa kwenye vikao. Maana yake na huyu mmoja akiumwa au akipata tatizo, shule inafungwa, watoto wanakaa nyumbani. Kwa hiyo, wakati tunapiga kelele sana kwamba mtaala ubadilishwe, sijui kitu gani kibadilishwe, tuangalie pia, hao tunaowapa kazi ya kufundisha watoto wetu wako katika mazingira gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Darasa la Saba lina masomo saba lakini una walimu wawili. Mimi ni mwalimu, ndiyo maana nimeanza kusema hivyo. Kuna kitu tunaita content mastery, yaani mimi leo kwa sababu nimesoma Physics, Chemistry na Biology, huwezi kuniambia nitakuwa mzuri kwenye Chemistry, nitakuwa mzuri kwenye Biology na nitakuwa mzuri kwenye Physics, never! Kwa hiyo, ni saw ana wale walimu wawili waliopo kwenye shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo shule ambazo nitakuletea Mheshimiwa Waziri, siongei kutoka hewani. Wale walimu wawili waliokuwa kwenye zile shule, unamtaka huyo mwalimu afundishe history, afundishe geography, afundishe hesabu na kadhalika, mtu mmoja haiwezekani. Ndiyo hapo tunapoanza kuwaharibu Watoto. Wakija huku juu tunataka wawe competence based. Competence hiyo wameipata wapi ikiwa kule chini alikotoka hali ilikuwa hiyo bora liende!
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu suala la kufundisha niwaambie ndugu zangu, haliishi darasani, ama halianzii darasani. Kuna kitu kinaitwe Scheme of Work unatakiwa uandae kila somo, kuna kitu kinaitwa Lesson Plan, unatakiwa uandae kila somo na kila kipindi. Mwalimu kwa siku anaingia madarasa matano au sita, tofauti tofauti aandae hivyo vitu vyote, unategemea atamfundisha mtoto vizuri! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule ziko Halmalshauri ya Wilaya ya Newala. Ninayo orodha hapa, zipo kama tisa, zina walimu wawili au watatu. Nikutajie kwa mfano, halafu ufuatilie na mpeleke walimu. Matokeo yanapotoka, hatutaki kusikia Mtwara imekuwa ya mwisho, tunataka iwe ya kwanza kwa maana watoto wapate walimu, wafundishwe vizuri. Wanazo akili, lakini hawapati mazingira bora ya kuweza kujifunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna shule inaitwa Mpalu, ina walimu watatu; kuna shule inaitwa Mpotola, ina walimu watatu; kuna shule inaitwa Chikalule, ina walimu wawili; ziko nyingi, orodha ninayo na nitakuletea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulisema, walimu wetu hawapati mafunzo kazini. Mwalimu akishamaliza mafunzo yake yawe ya cheti au ya nini, akiingia ndiyo tumemsahau hiyo mazima. Tunaomba walimu wapatiwe mafunzo kazini. Kuna TRCs kwenye Vyuo vya Ualimu viliwekwa kwa sababu ya kuwasaidia walimu kutoka kwenye hizi shule kwenda kupatiwa ujuzi, kama mnabadilisha vitabu, mtaala, na kadhalika, tunategemea walimu wale waendee kule. Hata hivyo, sasa hivi ukienda zimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetokea Chuo cha Ualimu ndio nikawa Mbunge, naelewa hakuna kinachoendelea kule. Kwa hiyo, hizo Teachers Resource Centre zilikuwa zinawasaidia sana walimu kwenda kunolewa ili kuongeza ujuzi kwa sababu elimu kila siku inabadilika, kuna mambo mapya, kuna zile crosscutting issues ambazo tunategemea mwalimu aweze kuzipata na kuongezewa ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu huyu mwenye stress ya kutokupandishwa madaraja, kutokuongezewa mshahara, hana nyumba ya kuishi, anakotoka ni mbali mpaka afike kazini, bado leo unamlundikia vipindi kufundisha kutoka awali mpaka Darasa la Saba, halafu tunakuja humu ndani tunalalamika kwamba watoto wetu sasa hivi hawaelewi, hawafanyi nini, hata wale kule wanachoka. Tuwaangalie kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongea hayo, sasa naomba nizungumzie issue ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Suala hili naliunga mkono sana kwa sababu najua umuhimu wake, lakini naomba Serikali iangalie, hata ukisoma hotuba ya Kamati imewapa ushauri. Tusiwaze sana kwenye mambo madogo madogo. Leo siyo wakati wa kumpa tu mtaji wa shilingi 50,000, anafanyia nini? Ndiyo swali tujiulize. Mnawaambia watu wakae kwenye vikundi 10, wanakaa hapo, wanazunguka usajili mpaka waje wasajiliwe unawapa shilingi 500,000. Tunataka tuwatoe kweli kwenye umasikini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu mfuko kwanza uangalie vizuri, uwekewe utaratibu vizuri na watu tuwe na mind kubwa ya kuona kwamba tunataka tuwawezeshe watu. Unaweza ukampa mtu shilingi milioni 100 akafanya shughuli, akaajiri watu hata 20, 30, wakawa wanapata kipato kupitia yeye. Tusiangalie sana kwenye mind ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea kidogo kwenye Jimbo la Mtwara Mjini, Manispaa ya Mtwara Mjini. Niliuliza swali juzi, tuna tatizo kubwa Mheshimiwa Waziri mkatuangalie, maji yanajaa sana. Yaani watu wa Mtwara Mjini sasa hivi wakiona wingu limekaa huko juu, wanajiuliza, hii mvua ikishuka hapa itakuwaje?
Mkatuchimbie mifereji, barabara nyingine zinajengwa, maana yake zinasababisha yale maeneo yawe chini. Sasa kama yako chini na mifereji haiko ya uhakika, matokeo yake kila siku maji yanaingia ndani ya nyumba za watu. Kata ya Magomeni, Kata ya Chuno, Kata ya Likombe, Shangani, maji yanaingia kweli kweli ambapo zamani maji yalikuwa hayaingii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kabisa, mfanye jitihada za makusudi mwende Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkaangalie tatizo lile na mjue mnalitatuaje kwa sababu wananchi wale walipimiwa viwanja, wananchi wale wana maeneo yao ya biashara, lakini kila siku maduka yanaingia maji. Hiyo haileti afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana. Mimi ni mtu wa kwenda muda. (Makofi)