Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru dakika tano ni chache sana niliambiwa nitakuwa na saba nianze kwa kueleza changamoto ya walimu wa wilaya ya Kyerwa, na hii nimepigiwa simu mpaka jana usiku saa tisa walimu walioajiriwa mwaka 2012 hawajawahi kupandishwa madaraja naomba muwafikirie sana na hilo suala lao mlifanyie kazi wanahisi kama wamesahauliwa tafadhali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nongelee changamoto ya stendi kuna shangamoto ya stendi ya mabasi Nkweda, Nkwenda ni mji mdogo na kumekuwa na ajali nyingi kutegemea kwamba mabasi yanageuzia eneo lile dogo, kwa hiyo, kuna changamoto ya ajali nyingi sana naomba hiyo muifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa tathmini fupi naona muda ni mfupi nimepitia miaka tofauti kuangalia bajeti hii ya Wizara ya TAMISEMI na kwa kifupi naweza nikaeleza fedha imekuwa itatengwa lakini haipelekwi.

Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja tu ambao ni mwaka jana ndio fedha imeenda kwa asilimia 62 lakini miaka mingine yote inaenda kwa asilimia 54, 52, 50 na hiyo inakuwa reflected kwenye hoja za Wabunge nikulalamikalalamika kwasababu mambo hayafanyiki fedha haiende.

Mheshimiwa Spika, nirudi tena kwenye Wilaya ya Kyerwa tunachangamoto ya huduma za afya tuna hospitali moja ambayo ni hospitali ya Wilaya lakini pia na hospitali ambayo ni ya mission. Lakini tunaambiwa kutakuwa zahanati kwa kila Kijiji tutakuwa na Kituo cha Afya, Kyerwa ina zahanati tatu, kata 24 zina Zahanati 3 ikiwa ni upungufu wa zaidi ya asilimia 80 kwa hiyo, watu wa kerwa hawana huduma za afya kwa asilimia 80.

Mheshimiwa Spika, tunaangalia huduma za afya kwa asilimia 80 tunaangalia zahanati, zahanati zipo 24 tuna vijiji 667 tukiwa na zahanati 23 ambayo ni upungufu wa asilimia 97 kwa hiyo watu asilimia 97 kwenye vijiji hawana huduma za zahanati au za kuweza kupata matibabu wanayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia watumishi wa umma kwa kada ya afya kuna upungufu wa asilimia 67, tuna watumishi asilimia 24 tu. Kwa hiyo, tunategemea watu wa Kyerwa waishiishi tu, wakiumwa wao wenyewe wanajua itakuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea kwa uchungu mkubwa sana, fedha za bajeti zinavyoshindwa kupelekwa kuna maeneo mengine yanafaidika, mengine yanazidi kuwa disadvantaged, moja wapo ni Kyerwa na wilaya zake nyingi za Mkoa wa Kagera; fedha ikiwa haiwezi kwenda haipelekwi kwenye hayao maeneo.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye habari ya barabara, sitaki kuongelea, muda hautoshi lakini kule hakupitiki. Mimi narudia kusema kilio chao, wale ni Watanzania wanalipa kodi, wanastahili huduma. Kwa mfano, Kituo cha Afya cha Nkwenda nimezaliwa mimi, yaani mimi mama yangu alijifungulia pale Anatropia lakini hakijawahi kufanyiwa ukarabati mpaka leo. Pale kwenye wodi alikolazwa haijawahi kufanyiwa ukarabati mpaka leo mimi nakwenda mama mtu mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kituo hicho nachokisema kinahudumia out patients zaidi ya 1,000 kwa mwezi; wanawake wanaojifungua ni 300 mpaka 400 kwa mwezi; operesheni zinazofanyika pale ni zaidi ya 60 mpaka 70 kwa mwezi lakini hicho kituo cha afya kina upungufu wa majengo, hakina hata mashine ya kufulia. Wanawake zaidi ya 400 wanajifungua pale watu wanafua kwa mkono, it is totally unfair. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Anatropia ukae chini upewe taarifa. Ndiyo Mchungaji, Mheshimiwa Bilakwate.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nimpe taarifa. Pamoja na changamoto anazozisema kwenye upande wa afya, zipo, lakini Kituo cha Afya Nkwenda wamejenga maabara kubwa, wameweka jengo la upasuaji, wamepeleka vifaa vya kufulia na vya upasuaji na upasuaji unaendelea. Leo hii kuna jengo kubwa pale la mama na mtoto lina zaidi ya vyumba 24, Serikali inaendelea kuvikamilisha. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Anatropia.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa waipokee watu wa Kyerwa waone Mbunge wao anavyowatelekeza kwa sababu changamoto anazijua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze, hii siyo siasa, wanaoumia ni wananchi wa Kyerwa, wanaokosa huduma za afya ni watu wa Kyerwa, tusilete drama hapo. Asitafute legitimacy kwa kuumiza watu, tuseme ukweli, pelekeni fedha Kyerwa watu waweze kupata huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimeeleza habari ya changamoto ya watumishi wa afya na wale wachache ambao tuko nao, asilimia 24, wamekuwa wanabaki kwenye maeneo yaleyale madogo. Nitakwenda kutoa suluhisho; Kyerwa bado tuna nafasi ya kuongeza mapato, nimesoma ripoti ya CAG, inaonesha Mkoa wa Kagera ni moja kati ya mikoa ambayo haijafanya vizuri kwenye kupeleka ile asilimia 10 ambayo wanapaswa kurudisha kwa wazee, akina mama na watu wenye ulemavu. Hawapeleki fedha hizo kwa sababu hatuja-exhaust vyanzo vya mapato. Tuna uwezo wa kujenga stendi, tulikuwa na masoko ya kimkakati, yametelekezwa.

Mheshimiwa Spika, tuna uwezo wa kufanya biashara na Waganda, tuna uwezo wa kuwa na masoko tukafanya kazi na halmashauri ikawa na fedha. Tunaomba Kyerwa mtukumbuke kwenye masuala ya miundombinu tuweze kuzalisha vya kutosha, tutaweza kufanya maendeleo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Muda hauko upande wako Mheshimiwa.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)