Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kutuwezesha kuuona mfungo huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuongoza Wizara hii ya TAMISEMI, lakini pia niwapongeze sana Manaibu, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange pamoja na Mheshimiwa Silinde kwa kazi nzuri ambayo wameanza kuifanya. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kujikita katika ujenzi wa miundombinu ya shule za sekondari. Hata hivyo, nikiri kwamba shule hizi zina upungufu mkubwa sana wa walimu. Naiomba Serikali itazame Mkoa wangu wa Singida kwa jicho la kipekee, kwani Wilaya zangu za Mkalama, Singida DC, Iramba, Manyoni zina upungufu mkubwa sana wa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nangependa kujikita katika suala zima la afya katika Mkoa wangu wa Singida. Tunayo hospitali yetu nzuri ya Wilaya ya Manyoni, lakini hospitali hii ina changamoto kubwa sana ya majengo, majengo mengi ni finyu na pia ni chakavu kwasababu hospitali hii imejengwa muda mrefu sana, miaka ya 1950.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri yetu ya Wilaya ya Manyoni imetenga eneo, naiomba sana Serikali katika bajeti hii iweze kutujengea hospitali mpya ya wilaya na vilevile kukarabati hospitali hii ambayo sasa ni chakavu na majengo yake ni finyu na hospitali hii ibaki kama Kituo cha Afya kwa kuwa kata yetu ya Manyoni haina Kituo cha Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba nichangie kuhusu hospitali yetu ya Wilaya ya Singida DC. Hospitali hii imekamilika lakini changamoto kubwa, jengo la wazazi halijakamilika. Naiomba sana Serikali ituwezeshe kutupa fedha ili jengo hili nalo liweze kukamilika na sasa wanawake na akina mama waweze kupata huduma bora za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunacho kituo chetu kizuri kabisa cha Mgori kimeshakamilika. Nakushukuru na wewe uliweza kukitembelea kituo hiki wakati wa kampeni, lakini kituo hiki hakina vifaa tiba. Naiomba sana Serikali pia itutazame kwa jicho la kipekee iweze kutupatia fedha kwa ajili ya vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la uwezeshaji wa vikundi vya wanawake na vijana. Tunazo asilimia 10 zinatolewa katika halmashauri zetu, lakini nikiri kwamba asilimia hizi hazitoshi kukidhi mahitaji ya wananchi wetu. Ipo Mifuko ya Maendeleo ya Wanawake na Maendeleo ya Vijana. Naomba sasa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI washirikiane ili sasa wananchi waweze kuitambua mifuko hii na waweze kupata mikopo mingi zaidi kwani mahitaji ni makubwa sana. Naiomba Serikali itazame upya utoaji wa asilimia hizi 10 kwani wanatoa fedha, itakuwa ni jambo jema sana iwapo watatoa vifaa ili mikopo hii sasa iweze kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzagu kabisa ambao wamesimama hapa na kuzungumiza suala la barabara za TARURA. Naiomba sana Serikali iweze kutenga fedha za kutosha ili sasa tuweze kuwa na miundombinu mizuri katika vijiji vyetu na katika kata zetu. Natambua kwamba Serikali imefanya kazi kubwa kwa kuunganisha wilaya na wilaya na mikoa na mikoa, lakini upande wa vijijini bado hali ni tete especially katika wilaya zangu zote za Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie suala la mwisho la kuomba tuongezewe watumishi katika vituo vyetu vya afya pamoja na hospitali zetu za wilaya. Katika Mkoa wangu wa Singida kuna uhaba mkubwa sana wa watumishi wa Kada ya Afya. Namwomba sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu atuongezee watumishi wa kutosha ili wananchi wa Mkoa wa Singida waweze kupata matibabu kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja na ninakushukuru kwa nafasi. (Makofi