Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya TAMISEMI.

Kwanza nianze kwa kutoa pole kwa familia mojawapo katika Kata ninayoishi, Kata Qurus Karatu kwa kuondokewa na mtoto mdogo wa Darasa la Kwanza aliyefariki leo asubuhi wakati anaenda shuleni akavamiwa na fisi, akafiriki, nawapa pole sana.

Mheshimiwa Spika, hii ni ujumbe kwa Serikali kwamba ipo haja ya kuangalia hizi shule zetu za msingi, zijengwe katika mazingira karibu na jamii ya maeneo yale. Vile vile muda wa kwenda shuleni asubuhi kwa hawa watoto wadogo wa Darasa la Kwanza na la Pili kwa sababu ya umri wao kwa kweli sidhani kama ile asubuhi mapema lazima wawe wanafika shuleni ili kuwaweka katika mazingira salama zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, inaweza ikafikiriwa kuwa reviewed hawa watoto wadogo wa Darasa la Kwanza wanaoenda shuleni asubuhi wakawa wanaingia hata mchana ili kuwaweka katika mazingira salama zaidi wanapoenda shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, nichangie katika mambo matatu yafuatayo: kwanza, ni kuhusiana na uhaba wa nyumba za walimu katika shule zetu za msingi na sekondari. Ili tuweze kutoa elimu katika ubora na viwango vinavyotakiwa, pamoja na uwepo wa walimu, pia ni kuhakikisha tunakuwao na miundombinu rafiki yenye kutosheleza ili tuweze kutoa elimu inayotakiwa kwa watoto wetu na kupata ubora ambao tunaoutarajia kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kitabu cha takwimu cha elimu Tanzania, uhaba wa nyumba za Walimu katika shule zetu za msingi, tuna upungufu wa nyumba za Walimu 204,141na kwa shule za sekondari tuna upungufu wa nyumba za Walimu 67,699; jumla ya upungufu nyumba za Walimu katika shule zetu za msingi na sekondari kama nchi tuna upungufu wa nyumba 271,874. Sasa ukiangalia takwimu hizi na ukiangalia kilichotengwa kwa mwaka huu fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu maana yake Serikali inatarajia kujenga nyumba za Walimu 300 tu katika upungufu wa nyumba 271,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukifanya mahesabu, maana yake kila mwaka kama tutakuwa tunajenga 300, wakati tuna upungufu wa 200,000 plus, maana yake tunahitaji miaka 906 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi za Walimu hapa nchini. Sasa ni vyema Serikali ikalitazama hili, kama kweli tunataka elimu iliyo bora na kama tuna upungufu wa kiwango hiki, basi waje na mikakati thabiti ya kuona namna gani tunaondokana na upungufu wa nyumba za Walimu hapa nchini katika shule zetu zote za msingi na za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia pia uhaba wa madarasa; uhaba wa madarasa unapelekea wanafunzi wengi kutokupata nafasi za kwenda kuendelea, mfano wakimaliza darasa la saba wanataka kwend form one mara nyingi tumeshuhudia ikifika ule wakati ufaulu ukiongezeka Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wanakimbizana, yaani tunafanya zimamoto kujenga madarasa ili wanafunzi waliofaulu wote waweze kwenda shuleni. Sasa takwimu zipo zinaonesha kabisa wazi, mfano, mwaka 2018 wanafunzi waliokosa nafasi ya kwenda kidato cha kwanza kwa sababu ya uhaba wa madarasa ni 134,000; mwaka 2019 imepungua kidogo imekwenda 21,000; mwaka 2020 waliokosa nafasi ni wanafunzi 59,700.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu, kuna Sera ya Elimu bure, hii sera ndio inakuja kuleta matokeo haya ambayo tunayaona, kwamba ufaulu ukiongezeka maana yakje wanapokwenda huko form one wanakosa madarasa, hili linajulikana. Sasa kwa nini Serikali isiweke pia mkakati wa kuhakikisha upungufu wa madarasa unakwisha, wanafunzi wote waliofaulu wanakwenda shule. Takwimu zinaonesha shule ya msingi, upungufu ni madarasa 82,200; shule za sekondari upungufu ni madarasa 4,647. Huu upungufu ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunapojadili suala la elimu na tukitaka kweli tutoe elimu iliyo bora kwa wanafunzi wetu, tukitaka nchi yetu itoe product nzuri kwenye sekta ya elimu hatuna budi kuwekeza kuhakikisha nyumba za Walimu na madarasa yanakuwepo na kuhakikisha kwamba wanafunzi waliofaulu wanakwenda shule na isije ikatokea sababu hawaendi shule eti kwa sababu tu hakuna madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie hoja ya mwisho ambayo nimejikita kuzungumzia leo, ni suala la udhibiti ubora katika Idara ya Udhibiti Ubora...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)