Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Igalula nianze kuchangia kwasababu ya ufinyu wa muda, nianze kwa kuchangia suala la barabara, Jimbo la Igalula tumekuwa tukipiga kelele mara kadhaa hapa kulalamikia barabara zetu, nyingi hazipitiki hasa wakati wa masika.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya baadhi ya barabara na baadhi ya kata tangu dunia iumbwe, tangu tumepata uhuru hawajawahi kuona caterpillar la kusafisha barabara limepita katika maeneo yao. Kwa mfano katika kata ya Male toka tumeanzisha hii kata, halijawahi kupitiwa na barabara yoyote kwa bahati mbaya kupitia Serikali. Pia, Kata ya Nsololo haijawahi kupitiwa na caterpillar ambalo linasafisha barabara katika kata hiyo. Vile vile kuna barabara za Ipururu – Igalula haijawahi kupitiwa kabisa. Barabara za Kawekapina kuja Igalula hazijawahi kupitiwa. Ziko changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwasababu tuna chombo na taasisi ambayo kimeanzishwa na Serikali TARURA, tuiombe Serikali iongeze fedha kwasababu yawezekana caterpillar haziendi katika maeneo haya kwa sababu ya ufinyu wa bajeti lakini TARURA ikiongezewa fedha na halmashauri yetu ikaletewa fedha kupitia mfuko wa TARURA nina imani katika maeneo haya na wananchi wataona ma- caterpillar yamepita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ya daraja, jana Naibu Spika amesema katika Jimbo lake kuna watu watano wamepoteza maisha, roho inamuuna sana. Kila mwaka zaidi ya watu 20 wanapoteza maisha katika Kata ya Loya ili mtu aweze kuja kupata matibabu katika Kijiji cha Loya kutoka Mwamabondo lazima avuke mto. Kila mwaka akinamama wajawazito, watoto wanaoenda shule wanapoteza maisha zaidi ya 20 kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imekuwa likipigiwa kelele Daraja hili la Loya tangu mwaka 2013. Nimejaribu kupitia Hansard za Wabunge waliopita mwaka 2013 mpaka 2015 Mbunge aliongea, 2020 Mbunge alizungumza na baadaye akaamua kuwa maji yamemfika shingoni akaamua kwenda kuwadanganya wananchi akawaambia kuna fedha imetengwa ya kuja kujenga daraja.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupita kuwa Mbunge nilikuja kufuatilia fedha hizi sijaona fedha yoyote iliyotengwa. Niiombe Serikali, kwa haya madaraja ambayo ni kiungo ya kijiji na yenye huduma kwa wananchi muda wote niiombe Serikali iwekee kipaumbele, tuna hitaji Daraja la Loya lijengwe kwasababu limeanza kupigiwa kelele zaidi ya miaka 10. Niombe Serikali iweze kusaidia katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya TAMISEMI 2021/ 2022 sijaona wametutengea fedha za kuweka vifaatiba katika kituo chetu cha afya. Tumejenga majengo mazuri, Serikali imewekeza fedha nyingi, tunashindwaje kuweka vifaatiba ili wananchi wetu waanze kutumia yale majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majengo yamekaa kila siku tunapeleka wanafunzi wanakwenda kukalia, yanakuwa machafu nyoka wanaingia kwenye majengo. Niiombe Serikali, kwa hivi vituo ambavyo vimekamilika, wapeleke vifaatiba ili wananchi waanze kupata huduma. Vile vile tuna majengo mengi ya zahanati lakini kwenye bajeti hii wametuwekea kila jimbo angalau watapata zahanati mbili. Nina maboma zaidi ya 10 yapo, wananchi wameweka nguvu zao wanahitaji wapate huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwananchi anapochangia hela yake ya kwenda kujenga kitu, ana malengo nacho kwasababu amepata shida kwa muda mrefu. Kwa hiyo, yale majengo naomba Serikali itanue wigo wa kuongeza bajeti ya kujenga haya maboma. Sisi kazi yetu tunanyanyua maboma lakini Serikali mnapokuja na Mpango wa zahanati mbili mbili, kwa hiyo, nitachukua zaidi ya miaka 20 kumaliza maboma yangu. Niiombe Serikali, kwenye bajeti hii watuongezee ili wananchi wanapotoa nguvu zao basi waone matokeo kwa uharaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru, niachie wigo na wenzangu waendelee kwasababu niliomba tu dakika tano na wewe umenipa. Ahsante, nashukuru sana. (Makofi)