Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili bajeti muhimu zaidi kuliko zote nchini. Tunajadili bajeti yenye kuhudumia watu wengi zaidi kuliko bajeti yoyote nchini; tunajadili bajeti ya Taifa la sasa na hasahasa Taifa la baadaye, nawaonesha takwimu kuthibitisha maelezo yangu haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 50 hivi sasa, asilimia 50% ya Watanzania hawa wapo chini ya miaka 17. Maana yake nusu ya Watanzania ni watoto, hii ni kwa mujibu wa takwimu ya Taifa. Katika watoto hawa takribani milioni 25, watoto milioni 12 wapo kwenye shule za awali, msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za awali. Utafiti wa hali ya uchumi wa Taifa mwaka 2014 inaonesha idadi ya wanafunzi katika elimu ya awali imeongezeka kwa 1.9% kutoka wanafunzi 1,026,466 mwaka 2013 hadi kufikia wanafunzi 1,046,369.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi. Utafiti huo huo unaonesha 2014, idadi ya wanafunzi katika elimu ya msingi ilipungua wanafunzi 8,202,892 kutoka wanafunzi 8,231,913 sawa na upungufu wa 0.4%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sekondari. Utafiti huo pia unaonesha mwaka 2014, idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita ilipungua hadi wanafunzi 1,704,130 kutoka wanafunzi 1,804,056 sawa na upungufu wa 5.5%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Basic Education Statistics (BEST) watoto wa Kitanzania milioni nane wapo kwenye shule zetu za msingi, milioni nne wapo kwenye shule zetu za sekondari; kwa maana hiyo hapa tunazungumzia robo ya Watanzania wapo madarasani, mashuleni, wengine wamekaa chini kwa kukosa madawati, wengine matumbo hayana kitu kwa kutoka familia fukara na shule hazina chakula na wengine wanagombania kitabu maana hakuna vitabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri robo hii ya Watanzania inafundishwa na Walimu wasio na hamasa kutokana na mishahara midogo, kukosa makazi, kutopandishwa madaraja na hata wengine kuwa walevi wa kutupwa kutokana na stress za maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia na mamilioni ya watoto wetu wanaweza kuwa wanafundishwa na Walimu walevi, nani atawawajibisha ilhali ukaguzi wa elimu hautiliwi maanani? Nani atathubutu kuwawajibisha ilhali hatuhangaiki kutatua kero zao? Naomba kuwaambia robo ya Taifa letu tumeliweka mashakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, robo ya wananchi wanapata bajeti robo, Wizara ya Elimu ina bajeti ya sh. trilioni 1.3 hivi; tunaambiwa nyingine ipo TAMISEMI, ni vema Serikali ikaweka bajeti nzima ya Wizara ya Elimu pamoja na wazi ili tuweze kujua kwa uhakika kama 25% ya wananchi wanapata 25% ya bajeti yetu ya Taifa, lakini hata tukiweka zilizokwenda TAMISEMI bado bajeti yetu ya elimu ni chini ya 10% ya bajeti nzima. Tunawanyima watoto wetu haki yao ya kupata elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili ya chekechea na miaka mitatu ya shule ya msingi ni muhimu sana, lakini sisi sote tunajua hali ya watoto wa Kitanzania ni mbaya sana, hakuna msaada wowote wa Kiserikali, Kisera au Kisheria kuhusu siku za mwanzo za mtoto. Hali hii inabidi ibadilike kama tunataka kujenga Taifa lililoelimika kwa mujibu wa Dira ya Taifa 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya utafiti ya uwezo yanaonesha kuwa katika kila watoto 10 wa darasa la tatu ni watoto watatu tu wenye kuweza kusoma sentensi ya darasa la kwanza na kukokotoa hesabu za darasa la kwanza, hii inaonesha watoto wetu hawapati fursa ya kusoma vizuri katika miaka yao ya mwanzoni shuleni. Jamani tuwekeze kubadilisha hali hii na tukiweza kuwekeza tutapata kizazi cha watoto wenye uwezo mkubwa wa elimu wenye kupenda kusoma, wadadisi na wabunifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 50% ya vijana wanaomaliza darasa la saba hawaendelei na elimu ya sekondari, pia 75% ya vijana wanaomaliza kidato cha nne hawaendi kidato cha sita. Hivi sasa Sera yetu ya Elimu inaunganisha elimu ya sasa ya msingi na elimu ya sasa ya sekondari na yote kwa pamoja kuwa elimu ya msingi kwa miaka 10, vijana hawa wanaomaliza hawaendelei, wanakwenda wapi? Rasilimali hii inapotelea wapi? Hapo ndipo tunapohitaji elimu ya ufundi stadi na ufundi mchundo.
Naipongeza Serikali kwa kuamua kuviunganisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na VETA. Ilani ya uchaguzi ya chama chetu iliahidi kujenga VETA kila Halmashauri ya Wilaya toka mwaka 2005. Namwomba Mheshimiwa Waziri tutekeleze ahadi hii ili kuwapa stadi za maisha vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuamue kugeuza Jeshi la Kujenga Taifa kuwa VETA, kila Kambi ya Jeshi isajiliwe kuwa VETA ili wale wanaokwenda Jeshini kwa miaka miwili, mwaka mmoja uwe wa kupata skills maalum za maisha, apewe mkopo wa vifaa, tutoke kwenye maneno twende kwenye vitendo. Tutumie rasilimali za nchi kujenga vyuo, kufundisha Walimu wa vyuo hivi na kujenga Taifa la watu wanaofanya kazi ama kuajiriwa au kujiajiri, suala la VETA liwe ni mpango malum na utekelezwe na jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni kuhusu Walimu. Nashauri Kada Maalum ya Elimu ya Awali (Chekechea mpaka Darasa la Tatu) kada hii iwe na mafunzo maalum na motisha maalum, vyuo vikuu vitoe shahada maalum za kada hii na tuwe na mradi maalum wa utafiti wa namna watoto wanajifunza kutokana na kada hii na hawa wasiwe Walimu wa kawaida. Walimu wa watoto wetu wadogo wawe Walimu maalum na mishahara yao iwe malum.
Kama tunataka kujenga Taifa la watu wanaojifunza tuanze sasa kuwekeza kwa Walimu na watoto wetu katika hatua za mwanzo kabisa. Tubadilishe Tanzania ndani ya kizazi kimoja tu kwa kuwekeza kwa Walimu wa watoto wetu kuanzia ngazi za chini; let us derisk the Nation, let us build the foundation, education at early age is the foundation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja ya Waziri wa Elimu.