Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI. Niungane na wenzangu kumpongeza Waziri wa TAMISEMI na kusema kwamba Wabunge tuna imani naye kubwa kwamba atafanya kazi nzuri kwa sababu tunamfahamu ni mchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nianze kuipongeza Serikali kwa kutuletea pesa nyingi ndani ya Manispaa ya Mkoa wa Tabora. Mimi ni Diwani ndani ya Manispaa ya Tabora ndiyo maana naongea sana kuhusu Manispaa, lakini pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa mkoa mzima. Tulikuwa tunahangaika sana jengo la utawala kwa muda mrefu lakini bajeti hii imetuonesha kwamba tumepewa shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi huo, lakini tumeletewa bilioni moja, mia moja hamsini kwa ajili ya hospitali ya wilaya na zahanati tatu; Zahanati ya Igosha, Igombe na Ituru, tunashukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa kabisa ambalo tuna shida nalo sisi wananchi wa Mkoa wa Tabora, la kwanza nimwambie Mheshimiwa ndugu yangu Mheshimiwa Ummy, tuna shida ya kukata Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora ni mkubwa, ni mkoa wa zamani, una historia kubwa, lakini haujawahi kukatwa. Imekatwa Mikoa midogo na Mkoa wa Tabora umeachwa.

Nimwambie Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Tabora, Tanga na Morogoro ndiyo mikoa pekee haijakatwa na inasababisha kutopata huduma sawa sawa kwa wananchi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, mikoa hii mitatu na yenyewe ikatwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Tabora Mjini lina population karibia watu 400,000, lakini ni Jimbo moja lenye Kata 29. Namwomba Mheshimiwa Waziri apitie majimbo yote aone kipaumbele gani kilitumika kukata haya majimbo? Kuna majimbo yana Kata sita, yana population ya watu 20,000 mpaka 30,000 na kuna jimbo lina watu 400,000. Serikali imetumia mchakato gani kupata haya majimbo? Hiki kitu kinaleta maswali mengi. Unakuta mtu anakata sita… (Makofi)

SPIKA: Hiyo hoja muhimu sana hiyo, maana Kongwa ina watu 400,000 Jimbo moja, endelea Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Hata naongea hapa na Naibu Spika, anasema yeye kwake ana kata 36 zenye population zaidi ya watu 500,000. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri, hata kwake Tanga Jimbo lile ni kubwa. Sasa yeye labda ataona aibu kujikatia Mheshimiwa Waziri, lakini sisi utukatie. (Makofi)

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa jitaje.

T A A R I F A

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, naitwa Stella Ikupa. Naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Munde kwamba hata Dodoma Mjini ina kata 46. (Makofi)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Ikupa.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumwombe Mheshimiwa Waziri apitie majimbo yote na aangalie vigezo. Kama Mheshimiwa Waziri kuna jimbo dogo dogo yaunganishe. Kwa kweli kama nia ni njema na kama mnataka kufuata ukweli, majimbo makubwa myakate.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye masuala ya watumishi. Tabora Manispaa tuna shida moja; Tabora inaitwa Tabora Manispaa, lakini tuna Kata 12 ziko vijijini. Kwa hiyo, tunapokwenda kwenye mgao wa walimu, tunaambiwa hii ni Manispaa, ina walimu wengi, lakini tuna Kata 12 zina uhaba mkubwa wa walimu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nimeongea na Afisa Utumishi anipe idadi kwamba tulikuwa tunatakiwa kuwa na walimu wangapi kwenye ikama na tunao wangapi; lakini nilikuwa njiani nimechelewa kupata. Pia watumishi wa Afya kwenye zile Kata 12 ambazo zipo vijijini ambazo zipo ndani ya Manispaa pia watumishi ni wachache sana, tunaomba msaada wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imetuletea fedha nyingi za barabara na ujenzi wa majengo chungu nzima, lakini tuna watumishi wachache sana wa ujenzi. Kwa mfano civil engineer, quantity surveyor na ma-technician wa ujenzi wamekuwa wachache sana kwa sababu tunashindwa kusimamia miradi, hakuna watumishi wengi kama inavyotakiwa kwenye ikama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Tabora tuna Kituo cha Afya kikubwa sana Serikali imetujengea, kina majengo matano, lakini majengo matatu yanafanya kazi. Jengo la operation halifanyi kazi kwa sababu hakuna vifaa vya theatre. Kila kitu kimekamilika, bado vifaa vya theatre. Naiomba sana Serikali ituletee vifaa vya theatre kwenye zahanati yetu ya Mailitano. Pia tuna jengo la Mortuary ambalo tunashindwa kulitumia kwa sababu hakuna yale ma-freezer makubwa ya mortuary. Mheshimiwa Waziri nadhani umenisikia, tunakuomba sana, sana, sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunayo Hospitali yetu ya Wilaya, Serikali imetuletea fedha nyingi, lakini bado hatujapata fedha kwa ajili ya vifaa tiba kwa ajili ya hospitali yetu ya Wilaya.niiombe sana Serikali iweze kutuletea fedha kwa ajili ya vifaa tiba vya hospitali ile ya Wilaya, kwa sababu mpaka sasa wananchi wa Manispaa ya Tabora wanatibiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Wanasababisha msongamano mkubwa, wanasababisha lawama kubwa kwa madaktari kuonekana hawafanyi kazi ipasavyo, lakini ni kwamba hatuna Vituo vya Afya hatuna Hospitali ya Wilaya; na pale ni mjini population ni zaidi ya watu 400,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)