Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia. Kwanza naomba nimpongeze Waziri wa TAMISEMI na Manaibu wake, pia Katibu Mkuu na Manaibu wake wa Afya na Elimu. Sisi Wabunge wote humu tunalia na TARURA. Tusikilize ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu ili uchumi wa viwanda uendelee tunahitaji barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo barabara nyingi ambazo ni muhimu kwa kusafirisha mazao ya wakulima na tunapoangalia uchumi, tunawaangalia hasa wakulima ambao wanaweza kusafirisha mazao yao. Kwa hiyo, naomba sana TARURA iongezewe fedha na michango ya Wabunge inayozungumzwa kuongeza tozo kwenye simu, hilo lisikilizwe. Hatuna ubabaishaji kwa sababu hatuhitaji kukaa miaka 40 bila kujenga barabara zetu. Tunahitaji kukaa miaka mitano tumalize barabara zote za wananchi ili uchumi uweze kukua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuongeze tozo kwa sababu wanaosafiri ni hao hao wananchi, wanaotaka maendeleo ni hao hao wananchi. Kwa hiyo, tuongeze tozo kwenye mafuta pamoja na mitandao ili kuhakikisha kwamba barabara zetu zinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo barabara muhimu sana ya Isolo, Kabila Isawida ambayo inahudumia Wilaya ya Itilima pamoja na Magu. Ninayo barabara ya Kisamba - Sayaka ambayo inahudumia barabara ya Wilaya ya Busega pamoja na Magu. Ninayo barabara ya Mwamanga kisasa ‘B’ ambayo nayo kwa kweli ni barabara muhimu sana katika uchumi wa Wilaya ya Magu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. Magufuli ya kuboresha barabara ya Bujora - Kisesa kwenye makumbusho ya Wasukuma, imejengwa kilometa 400 bado kilometa 1.3. Naomba iingizwe kwenye barabara ambazo zitawekewa lami katika miji hii midogo midogo. Pia tunapoboresha miji na majiji tukumbuke pia kwenye Halmashauri zetu, nasi tunahitaji kuwekewa barabara za lami kwenye Wilaya zetu ili angalau wananchi waweze kupata huduma za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Afya tumefanya kazi kubwa sana, lakini wenye umri wa kwangu miaka 47, ni muhimu sasa nikapatiwa fedha ili tuweze kuikarabati hospitali hiyo na yenye ionekane kwamba ni hospitali ya kisasa. Pia kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kugawa Wilaya ya Magu pamoja na Wilaya ya Misungwi na Nyamagana kidogo kuwa Wilaya mpya ya Kisesa. Hii Wilaya nayo inategemewa ianze ili kusogeza huduma kwa wananchi wetu. Tumejenga vituo vya afya, kinachohitajika sasa ni vifaa; X-Ray pamoja na cold room katika Kituo cha Afya cha Tangala pamoja na Kabila na Lugeye ili kuhakikisha kwamba vinatoa huduma iliyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi wa P4R wa kujenga madarasa umeleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania, umepunguza uhaba wa madarasa katika shule zetu. Ushauri wangu ni kwamba, fedha hizi kama itawezekana, kwa sababu kuna maboma ya wananchi, kwa sababu fedha hizi zinapokuja, kwanza zinakwenda kujenga maboma mapya. Kwa sababu tuna maboma ya wananchi ambayo yameshajengwa tayari, fedha hizi ziwe zinamalizia. Sikija shilingi milioni 20 zimalizie maboma mawili, tunakuwa na madarasa mawili badala ya kujenga darasa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninalo jengo la Halmashauri. Mwaka huu wa fedha tuliomalizia lilitengewa shilingi milioni 750, tumeletewa shilingi milioni 136, ni vizuri fedha ambazo zimebaki ziletwe ili tuweze kuendeleza ujenzi ule. Bajeti ya mwaka huu umetutengea shilingi bilioni moja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga, muda washilaga.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Ahaa!

SPIKA: Mmh!

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mhesimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja nikiamini kwamba Wizara hii Waziri na Makatibu Wakuu na Watendaji wadogo wadogo kama akina Ntuli na akina Cheyo wanafanya kazi. Ni Wizara barabara, itakwenda bam bam.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)