Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kutoa mchango wangu kwenye kuelekea kuhitimisha mjadala huu wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha utayari na dhamira yake kubwa katika kuboresha sekta ya afya kwa manufaa ya wananchi.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake kama Rais achilia mbali historia yake ya awali ya kuitendea haki sana sekta hii tayari ameshafanya maamuzi makubwa mazito katika kuimarisha Sekta hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Spika, Baadhi tu ya maamuzi aliyoyafanya ni mtaji na msingi muhimu sana katika maendeleo endelevu ya sekta hii, ambapo kwanza amemteua Naibu Waziri mahsusi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamisi jambo ambalo litaimarisha sana uwezo wa sekta hii kuwagusa wananchi wa makundi haya ya jamii yaliyo msingi wa maendeleo ya Taifa (Wanawake, Watoto, Wazee na Vijana na masuala yote ya usawa wa kijinsia).
Mheshimiwa Spika, breaking news nzuri kabisa, Mheshimiwa Rais ameridhia na ametoa bilioni 80 mwaka huu mwezi huu Aprili 2021 ziende kuimarisha eneo la upatikanaji wa dawa, vipimo na vifaa tiba, eneo ambalo limezungumzwa kuwa kero kubwa sana kwa wananchi wetu sasa hivi. Utaratibu wa kununua dawa hizi haraka sana unaendelea ili tuzifikishe mahali sahihi. Hii ni nyongeza ya fedha iliyotolewa kipindi cha Julai mpaka Desemba ya bilioni 43, zikaongezwa nyingine kama 18 jumla bilioni 59 ambazo zilishaenda, ziko huko zinaendelea kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Spika, vilevile kama ambavyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alitoa taarifa Bungeni hapa Mheshimiwa Rais pia ametoa maelekezo kwamba, ujenzi wa hospitali za Halmashauri kwenye maeneo ambayo zilikuwa hazijajengwa uendelee. Kwa hiyo utaona ni namna gani Mheshimiwa Rais amejitoa kuimarisha sekta hii, nasi tunampongeza. Katika kipindi cha muda huu mfupi ambao amekaa inabidi sasa sisi tumuunge mkono na Wizara yangu itashirikiana sana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha kwamba hatumwangushi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue sasa fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kuteuliwa kwake kushika nafasi hii nyeti ambayo ni mhimili wa huduma zote nchini ikiwemo huduma za afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto wanakoishi ambao 70% ya wananchi wote wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, nampongeza kwa hotuba yake nzuri ambayo imegusa vizuri sana utashi wa kisera tunazozitoa sisi Wizara ya Afya na miongozo ya kisera katika kuendeleza sekta hii ngazi ya afya ya msingi. Wizara yangu itatoa ushirikiano wa kila namna kuhakikisha kwamba maendeleo ya sekta hii ngazi ya halmashauri yanatimia sambamba na sera inavyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani kwa Wabunge wote waliochangia mambo mbalimbali ambayo mengine yamekuwa ni michango darasa kwa wataalam wote wa sekta ya afya tulio ngazi zote. Tuwaahidi kwamba tutayafanyia kazi, machache nitayataja hapa kama matano tu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile alichangia kwenye masuala ya rasilimali watu yaani kuna upungufu wa rasilimali watu ambapo sasa Wizara imepokea hoja hii na inatambua upungufu mkubwa wa watumishi na imewasilisha maombi ya bajeti kwa mwaka huu 2021/2022 tunaouendea takriban bilioni 144 kwa ajili ya kuwaajiri watumishi wasiopungua 2,775 tunaamini kwamba bajeti hii itapitishwa na sisi pia hatutakuwa wachoyo tutakaa na TAMISEMI kuangalia kwamba tunawatumiaje hawa watumishi hasa waweze kugusa maeneo yale ambayo tumeyapigia kelele kwamba vituo vimejengwa na havifanyi kazi bado.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ajira hizi Wizara imebaini kuwa kuna haja ya kuimarisha uwajibikaji wa watumishi waliopo katika vituo vyetu. Kwanza kuwapangia maeneo kwa tija na kuwapa motisha waweze kufanya kazi kwa moyo Zaidi. Hivyo, tutashirikiana na Wizara zote za kisekta ikiwepo Utumishi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuja na mpango wa jinsi gani watumishi wetu wanaofanya kazi vizuri watambuliwe kokote waliko, maana suala lingine kuwa na watumishi na suala lingine watumishi wale kuwa productive, efficiency inakaaje.
Mheshimiwa Spika, kuhusu maendeleo ya miundombinu ya afya, Wizara imesikia hitaji la kumalizia ujenzi wa miundombinu na kukarabati ile ya zamani pamoja na kuweka vifaa tiba stahiki, mitambo mbalimbali ya huduma za afya na magari ya wagonjwa (ambulance). Kwa kuwa Wizara yangu inahusika na kutafuta rasilimali toka vyanzo mbalimbali ikiwemo kuwashawishi wadau wa maendeleo waweze kutoa fedha, tutatekeleza jukumu hilo kwa nguvu zote na rasilimali tutakazopata tutazielekeza katika siyo tu hospitali za rufaa za mikoa kanda na Taifa bali tutalenga kuimarisha vituo hivi vya afya vya ngazi ya msingi kwenye halmashauri ili kupunguza rufaa za kwenda kwenye hospitali kubwa za kibingwa.
Mheshimiwa Spika, aidha, tutabuni mbinu nyingine mbalimbali za kuwashirikisha wadau wetu hasa sekta binafsi ili pale tunapokuwa na ufinyu wa bajeti kupitia PPP tuweze kuhakikisha tunakaa vizuri, wananchi wetu hawa tunaowapeleka kwenye bima ya afya kwa wote waweze kunufika na kuona faida ya huduma hizi wakiwa na bima hizo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu dawa na vifaa tiba na vipimo, kama nilivyosema tumepata hizi fedha na Serikali imekuwa ikijitahidi kuwekeza fedha nyingi, lakini sasa Wizara imeenda mbali kufuatilia nini hasa kinajiri eneo hili. Tumebaini changamoto nyingi huku zikiwa zinaweza kuepukika, kuanzia kwenye mfumo wa manunuzi changamoto za watumiaji, ikiwemo namna wanavyosimamia mtaji wa bidhaa za afya na bidhaa zenyewe zinapofika mikononi mwao kule kwenye vile vituo.
Mheshimiwa Spika, changamoto zingine ni namna gani watumishi wetu wamejiandaa kutoa huduma kwa weledi wenye mvuto customer care ili watumiaji wanaofika kwenye vituo vyetu wasiwe tu wale wa msamaha, waje na wale wanaoweza kulipa na wenye bima. Hili eneo tutashirikiana kulifanyia kazi ili hawa wanaoajiriwa wakawe na tija.
Mheshimiwa Spika, hivyo tutatendea haki utafiti huu na yatokanayo yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambapo tumeshabaini maeneo yetu ya kufanyia kazi hususan uwajibikaji dhidi ya vitendo vya ukosefu wa uzalendo, ubadhirifu na ufujaji na kutojali. Kwa kufanya hivyo tutamtendea haki Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maamuzi magumu aliyoyafanya kuwa licha ya sekta nyingi ambazo zinahitaji fedha hizi ameona kwamba atupe kipaumbele sekta ya afya kwa billioni hizi 80.
Mheshimiwa Spika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri, lakini hujaunga mkono hoja.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimeunga mkono hoja na bima kwa wote Muswada unakuja Bungeni Juni kabla hatujamaliza Bunge. Ahsante.