Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi ninakwenda kujikita kwenye eneo moja tu, eneo la utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu na tunatambua kwamba utawala bora ndiyo nguzo muhimu sana kwenye mipango yoyote. Ukiangalia kwenye sustainable development goals, utawala bora ni nguzo muhimu. Ukiangalia kwenye Dira ya Taifa, utawala bora ni nguzo muhimu lakini hata ukiangalia kwenye mipango ambayo tunakuwa tunajadiliana humu ndani, haiwezi kutekelezeka kama eneo la utawala bora haliwezi kuwekewa nguvu inayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni lazima ili kuweza kuboresha eneo la utawala bora tutafute vichocheo vikubwa ambavyo vinachochea na kuhamasisha utawala bora katika Taifa letu. Katika tafiti zangu ambazo nimekuwa nikizifanya na tafiti mbalimbali ambazo nimekuwa nikizisoma nimegundua kitu ambacho ni very interesting. Nimekuja kuona suala la utawala bora, tafiti nyingi zinaonesha wanawake wana mchango mkubwa sana kwenye good governance na sehemu hii napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa Rais mwanamke wa kwanza katika Taifa letu, lakini kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke East Africa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rekodi tuliyoiweka kama Taifa, tumeithibitishia dunia ya kwamba Taifa letu hatuna doubt wala dispute ya uwezo na umahiri wa mwanamke katika masuala ya uongozi. Ni ukweli usiopingika kwamba mama ameanza vizuri. Nampongeza na namuunga mkono kwenye jambo ambalo amelizungumzia jana la kuunga jitihada zake za nguvu kabisa kuwapa vipaumbele wanawake. (Makofi)
Mimi nina ombi moja kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais, ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ilani ambayo ilitumika kwenye kampeni 2020, ukiangalia ukurasa wa 281 Ibara ya 231(j) inasema hivi; Serikali ya CCM itabaini na kutekeleza mikakati ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika maamuzi na uongozi kwenye nyanja za kisiasa na kiuchumi hadi kufikia 50 kwa 50. Na bold hadi kufikia 50 kwa 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna wakati mwingine sahihi ambao kama wanawake wa Taifa hili tunautegemea kama kipindi ambacho mama Samia Suluhu Hassan atakuwa madarakani kwa ajili ya kutekeleza jambo hili. Suala hili tusilitazame katika sura ya kisiasa, suala hili tulitazame katika sura ya usimamizi wa masuala ya kiuchumi na masuala ya utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wamepimwa na wamethibitika kuonekana kuwa ni waadilifu na wana uwezo mkubwa sana kusimamia masuala mbalimbali katika Taifa letu. Lakini pia sisi hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo, nimesoma miaka mitano iliyopita Germany, nimeangalia sheria yao na ninayo hapa, Germany wametunga sheria, yaani kwa upande wao hilo suala halina mjadala. Uwakilishi wa wanawake not less than 30 percent kwenye mashirika yote ya umma, pamoja na private sector. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hapa kwetu Tanzania wanawake wameonesha jitihada kubwa sana katika kufanya shughuli zao. Nimesoma taarifa ya utafiti uliofanywa na Tanzania Chamber of Commerce, industry and Agriculture (TCCIA); wanasema hivi, wanawake wa Tanzania ndiyo lion share, I mean ndiyo majority share, I mean ndio wamiliki wakuu wa biashara ndogo ndogo na biashara za kati. Wanawake hawa wanasimamia zaidi ya asilimia 95 ya idadi ya biashara zote Tanzania. Wanachangia zaidi ya asilimia 35 ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Naomba nitumie jukwa hili la Bunge lako Tukufu kumuomba Mheshimiwa Rais apambane huko aliko na sisi kama Wabunge kwa nafasi yetu tutamsaidia. Ninaomba kutoa taarifa, ninakusudia kuleta Muswada Binafsi Bungeni wa kutaka not less than 30 percent ya viongozi wa mashirika ya umma wawe wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba taasisi zote zinazo-deal na masuala haya waweze kunisaidia kwa ajili ya kupata information za kuweza ku-package hoja yangu ambayo nitakuja kuleta Muswada Binafsi. Lakini pia niwaombe na Waheshimiwa Wabunge wanaume watuunge mkono sana katika hili. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Engineer Manyanya.
T A A R I F A
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, napenda kumpa taarifa ndogo tu Mheshimiwa Jesca kwamba kwa jinsi ambavyo ameweza kuinukuu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwa jinsi ambavyo ameweza kusikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Rais ya jana na kwa jinsi ambavyo anaendelea na mchango wake, kwa kweli naamini kama Kambi ya Upinzani itakuwa inaendelea kutoa michango positive na kuwa pamoja katika timu moja katika Bunge, mambo mengi ambayo tulikuwa tunayapanga yataendelea vizuri. (Makofi)
Kwa hiyo mimi nampongeza kwa positivity, uchanya wake katika mchango huu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa, hiyo sio taarifa. Malizia mchango wako. (Kicheko)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niendelee kwenye eneo lingine dogo la transparency. Unapozungumzia utawala bora suala la transparency haliepukiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up anisaidie. Sitaki sana kujua sababu gani iliwafanya mkajiondoa kwenye OGP (Open Government Partnership). Wote tunajua hii Open Government Partnership wakati mmejiunga mwaka 2011 na bahati mbaya au nzuri sijajua ni kwa kusudi gani mkaja mkajitoa, mmepeleka barua yenu kule kwenye committee tarehe 29 Juni, 2017. Mmetaka kujiondoa na mmejiondoa kwenye umoja huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la sisi kujiunga kwenye Open Government Partnership lilikuwa linawasaidia sana watafiti wa Taifa hili, lilikuwa linawasaidia sana NGO’s, wasomi wa Taifa hili. Walikuwa wana uwezo wa kupata taarifa mbalimbali ambazo wanazihitaji kwa ajili ya kusaidia hata katika masuala haya ya kujadili bajeti, tulikuwa tuna uwezo wa kupata references ambazo zimefanywa na researchers, lakini pia hata wanafunzi wetu ambao wako shuleni OGP imekuwa ikiwasaidia sana wao kupata taarifa na kuwasaidia katika masuala yao mbalimbali ya kitaaluma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais hebu turudi kwenye OGP, kuna tetesi ambazo nimezisikia kwamba mmejiondoa kwenye Open Governance Partnership kwa sababu kuna namna nyingine mmetafuta ya kutaka kutoa information zenu kupitia umoja fulani ambao uko Afrika, lakini it’s kind of kutaka kufunika funika vitu hivi. Mimi ninaomba sana Serikali, turudi kwenye OGP. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la uhuru wa vyama vya siasa. Katika Taifa letu mara nyingi sana tumekuwa tukishuhudia vyama vya siasa hususan vyama vya upinzani vimekuwa vikikosa fursa ya kufanya mikusanyiko ambayo kikatiba ipo kihalali kabisa.
Ninataka nimuombe Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais katika suala hili hebu rekebisheni hapa. Hivi vyama vina haki kabisa ya kikatiba ya kufanya mikutano ya hadhara. Vina haki ya kikatiba ya kukutana na wananchi na kueleza sera zao. (Makofi)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.
T A A R I F A
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu muongeaji asipotoshe, Mheshimiwa Rais jana amezungumza, anataka kukutana na vyama vyote vya siasa, wazungumze waone nini sasa wanaweza wakaendesha nchi yao pamoja. Haya masuala ya kwamba sijui vyama vimezuiwa kupiga nini, sijui kufanya mikutano, yanatokea wapi? Naomba nitoe Taarifa. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca Kishoa.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasikitika sana kusema kwamba sijajua kama Mheshimiwa Mbunge ni kweli hafahamu au laa! Suala la kufanya mikutano ya siasa sio suala la Mheshimiwa Rais kutuambia, ni suala la Kikatiba ambalo linatakiwa lifanyike katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii tukianza kuiendesha kwa matamko na sio kwa kufuata misingi ya Kikatiba tutapotea. Ni muhimu sana ili Serikali iweze kuwa ni Serikali ambayo inazingatia utawala bora basi itoe fursa kwa vyama vya kisiasa kufanya mikutano yao.
WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa muda tulionao hiyo itakuwa Taarifa ya mwisho.
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, taarifa inatokea upande ule. Mheshimiwa jitambulishe.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Francis Isack Mtinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji kwamba nchi yetu haijawahi kuzuia mikutano ya vyama, kilichokuwa kinatakiwa ni kwamba kila mtu kwenye Jimbo lake akafanye mkutano. Kwa hiyo, anaposema kwamba tumewahi kuzuia mikutano, anapotosha. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Jesca Kishoa, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei lakini niseme tu kwamba mimi nazungumzia vyama vya siasa sio mkutano wa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sijajua kwa upande wenu hili ninyi mnalifanyaje, lakini sisi wa vyama vya upinzani tunakuwa tuna mikutano ya hadhara ambayo ni kama chama ambacho kinajumuisha viongozi wa chama wanakwenda kutangaza sera ya chama chao na wananchi wanapata elimu ili kuweza kupima chama gani ambacho kinafaa kushika madaraka.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bil akufuata utaratibu)
WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa. Asipotoshe, aseme ukweli.
NAIBU SPIKA: Subiri, subiri.
Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane, mikutano ya vyama vya siasa huwa ni mikutano ambayo iko kwenye katiba zao. (Makofi)
Hiyo mikutano hufanyika kwa vipindi fulani na hiyo mikutano hata Chama cha Mapinduzi huwa ile mikutano sio ya hadhara. Kwa mfano tarehe 30 Aprili, 2021 Chama cha Mapinduzi kimetangaza kitakuwa na Mkutano Mkuu, Mkutano Mkuu unaenda kufanyika pale JK Convention Centre. Ule niyo utaweza kuita ni Mkutano wa CCM, lakini ameenda Rais mahali unasema huo ni Mkutano wa CCM, ule sio mkutano wa CCM, ni mkutano wa Rais. Mkutano wa Chama cha Mapinduzi ni kama huo tunaoenda kesho kutwa. Sasa ukisema mikutano ya vyama vya siasa imekatazwa, kuna chama kiliitisha mkutano halafu ukakatazwa?
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
NAIBU SPIKA: Ngoja, tuelewane vizuri. Hata Katiba tuwe tunaisoma vizuri, leo naongea nikiwa nimekataa. Hata Katiba tuisome vizuri. Katiba ikishaweka zile haki kule, imeweka na mipaka yake na usisome kifungu kimoja ukata kukisimamia hicho ukasahau kingine. Katiba yetu inazungumza haki nyingi sana. Ile haki ya kwako wewe haitakiwi kuzidi pua yako ili usiisumbue haki ya mtu mwingine.
Kwa hiyo lazima utaratibu ufuatwe na ndiyo maana Bunge letu hutunga sheria ili kuvikazia vile vifungu vya Katiba. Kwa hiyo, ukizungumza tu hivi jumla mtu anawaza kuna katazo labda liko mahali, hapana, tuelezane vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Jesca Kishoa malizia mchango wako.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki sana kubishana na Kiti chako, lakini niseme tu mimi ni miongoni mwa wahanga wakubwa sana kwenye suala hili la mikutano ya hadhara.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie hoja yangu.
NAIBU SPIKA: Haya, malizia sekunde 30. Naambiwa hapa muda wako umekwisha.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusisitiza vyama vya siasa tunahitaji kupata uhuru wa kikatiba wa kufanya mikutano ya hadhara. Ni kwa muda mrefu sana na mimi nimekuwa ni muhanga katika eneo ambalo nilikuwa nikiwakilisha kama Mbunge wa Mkoa wa Singida kuanzia term ya Bunge lililopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikizuiliwa kufanya mikutano yangu ya hadhara na wananchi kwa sababu ambazo hazieleweki. Kuna wakati mwingine wamekuwa wakitoa sababu za kusema kwamba hali ya…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana. Muda wako umekwisha.