Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia Ofisi ya Rais, Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kwenda kwenye hoja zangu moja kwa moja nakumbuka siku moja hapa Mheshimiwa Spika aliongea kauli ambayo ilinigusa sana, kuna jambo lilitokea Wabunge tukapiga makofi, akasema wakati mwingine Wabunge tunapiga makofi hata hatujui tunapiga makofi kwa jambo gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo jambo linanikumbusha wakati wa kampeni nilivyokuwa Arusha Mjini, nilikwenda kufanya ziara kwenye viwanda viwili, Kiwanda cha A to Z na Kiwanda cha Sunflag. Wafanyakazi wale waliniuliza maswali ambayo kila siku nayakumbuka; kwanza walitaka niwahakikishie kwamba nitakapokwenda Bungeni sitakuwa Mbunge wa makofi na ndio hata kwa mambo ambayo yanaumiza wananchi, la pili wakaniambia je, naweza kutoa hoja zenye maslahi ya wananchi au nitakwenda kuunga kila kitu mkono hata kama kinaumiza wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakanikumbusha kwamba wanasema wana hasira sana na hoja ya kikokotoo. Kwa hiyo, na yenyewe pia walisema niiweke kwenye maanani, lakini pia wakataka niweke kichwani kwangu changamoto iliyopo ya kima cha chini cha mshahara kati ya wafanyakazi wa sekta binafsi na wafanyakazi wa sekta ya umma ambapo wafanyakazi wa sekta binafsi wanaohusika na mambo ya kilimo na nguo kwenye viwanda, kima cha chini ni 100,000/= lakini wa Serikali ni 300,000/=. Kwa hiyo, hayo mambo ambayo nimesema leo niwakumbushe kwamba na mimi nayakumbuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajielekeza kwenye mambo mawili; jambo la kwanza nakumbuka Serikali yetu ya Awamu ya Tano ilifanya zoezi moja muhimu sana na zoezi nyeti sana, zoezi la kuhakiki vyeti vya watumishi wetu. Lilikuwa ni zoezi la lazima, lilikuwa ni zoezi ambalo linatusaidia kufanya usafi kwenye sekta nzima ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninakumbuka tarehe 7 Machi, 2018 ilitoka Taarifa ya mwisho ya Serikali ambayo ilituambia wafanyakazi 511,789 ambao ni sawasawa na asilimia 96.71 walikuwa ni wafanyakazi waliohakikiwa, lakini wafanyakazi 14,409 ambao ni sawasawa na asilimia 2.82 walikuwa ni wafanyakazi ambao walibainika wana vyeti fake na wafanyakazi 1,907 walikuwa ni wafanyakazi ambao walikuwa bado hawajapeleka uthibitisho wa vyeti vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ambayo nataka niijenge hapa, pamoja na kuunga mkono zoezi la Serikali la kuwatambua watumishi wenye vyeti fake na kuchukua hatua stahiki, lakini lazima tukumbuke hawa watumishi walifanya kazi ya kuitumikia nchi hii. Hata masuala ambayo tunajivunia leo wao pia ni sehemu ya kazi ambayo tumeifanya. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kujenga hoja kupitia Wizara yetu hii ya Utumishi ni vizuri sasa wafanyakazi hawa tukaangalia utaratibu wa kuwapatia haki zao kwa sababu, wakati wanafanya kazi waliweza kukatwa fedha ambazo zikaenda NSSF, leo zile fedha zimekwenda kule zinamnufaisha nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wafanyakazi hawa wengine walipitisha muda wa kisheria, miaka 15, miaka 20 na kuendelea, walistahili pia kulipwa kiinua mgongo. Kwa hiyo, pamoja na Serikali kuwaondoa kazini nilikuwa naomba Serikali hii ya Awamu ya Sita ikaangalie jambo hili kwa jicho la huruma, ikawaangalie wananchi hawa wananchi 14,409 ambao wana familia zinawategemea wakaweze kupata kiinua mgongo chao wakapate na mafao yao na baada ya hapo tuendelee sasa kuchukua watumishi wenye sifa. Maana sisi kama Serikali pia tulichangia kuingiza watumishi hawa kwa sababu waliingia kwa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili niende kwenye mchakato mzima wa kuwapandisha vyeo watumishi na madaraja na mimi nakiri hotuba ya jana ya Mheshimiwa Rais imetupunguzia maneno kwa sababu watumishi wa umma walikuwa na kilio kikubwa sana. Watumishi wa umma toka mwaka 2015 walikuwa hawajapandishwa mishahara. Watumishi wa umma wamekuwa na matatizo mengi sana kwenye madaraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la madaraja sio suala jepesi kama tunavyoliona. Mimi nakumbuka mwaka 2012/2013 wakati nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kweye bajeti ya mwaka 2012/2013 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe Mji alisahau kuwaingiza watumishi kwenye mchakato wa kupanda vyeo, watumishi ambao waliajiriwa mwaka 2009. Matokeo yake ni kwamba wale TSC au kwa maana ya TSD huko zamani ambao lazima kikao chao kikae kiweze kuwapitisha hakikuweza kukaa eti kwa sababu hakuna posho, watumishi wakakosa haki yao ya msingi ya kupanda madaraja na baadaye wakatakiwa waandike barua ya kuomba kupata daraja la mserereko.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hoja yangu ni nini; lazima tuangalie vizuri mfumo wetu wa kuwapandisha madaraja watumishi. Kwa sababu nimeambiwa taratibu ambazo zinafuatwa, taratibu ya kwanza tunaangalia bajeti. Mfano mwaka huu tumeajiri watu 800, uwezo wetu wa bajeti wa kupandisha ni watu 300, tunabakisha watu 500 ambao wao watakuja kupanda mwaka mwingine wa fedha. Kumbuka hawa wameanza kazi pamoja, huyu ana TGS D atatoka D atakwenda E, ambaye ameanza naye kazi pamoja atabaki kwenye TDGS D ile ile ambayo italeta manung’uniko na malalamiko makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeambiwa pia wanaangalia tange kwa maana ya seniority list, lakini pia wanaangalia na OPRAS. OPRAS ambayo ina changamoto nyingi inatakiwa kuwe na malengo, lakini pale kuwe na resources. Unakuta malengo yanakuwepo, lakini resources zinakuwa hazipatikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nataka niseme kwamba, changamoto ya madaraja ya watumishi ni kubwa tofauti na ambavyo tunaiona. Nilikuwa nataka niishauri Serikali ni vizuri sasa, kwa mapendekezo yangu, tukaunda tume au tukaunda timu maalum ambayo itafanya kazi ya kupitia changamoto za madaraja ya watumishi kwa miaka yote iliyokuwepo. Vinginevyo wale ambao wanaweza wakalalamika watapata solution, wale ambao hawawezi kuwafikia Serikali watabaki wananung’unika na mwisho wa siku tunaanza kuwatupia mzigo Maafisa Utumishi wakati tunafahamu kwamba Afisa Utumishi hawezi kupandisha nje ya bajeti na hawezi kupandisha nje ya utaratibu wa Serikali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)