Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na mimi niende moja kwa moja katika mchango wangu. Nitakwenda kuanzia walikoishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu hususan Mheshimiwa Nape Nnauye.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria inataka watumishi wa umma wapandishwe madaraja kila baada ya miaka mitatu, hiyo ndiyo sheria inavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kumekuwepo na watendaji wa taasisi mbalimbali ikiwemo utumishi wa umma wamekuwa wakishusha nyaraka mbalimbali ambazo zinakinzana moja kwa moja na sheria hii ambayo nimeitaja awali na nyaraka hizi zimekuwa zikielekeza kwamba watumishi wapandishwe madaraja kila baada ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunaye Waziri husika Mheshimiwa Mchengerwa, ningependa atakapokuja ku-wind up atueleze ni kwa nini basi Wizara imeamua kukiuka Sheria hii ya Watumishi wa Umma kwa nini wameamua basi kukiuka sasa sheria hii na sasa wametengeneza nyaraka tofauti kabisa ambazo zinapingana na haki za watumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi nilivyosimama mbele yako wapo watumishi wengi ambao ni takribani miaka sita hawajapandishwa madaraja na nimesema kuna nyaraka ambayo inakinzana na sheria yenyewe ambayo inasema watumishi hawa wa umma wapandishwe madaraja ndani ya miaka mitano, lakini sasa hivi hata hilo ambalo haliendani na sheria wameshindwa kulitimiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu kwamba watumishi wa umma ndiyo kiungo pekee cha Serikali katika utekelezaji wote wa bajeti tunazopitisha, mipango yote ambayo tunaipima, tunaipanga, lakini maslahi yao yamekuwa hayaangaliwi. Kama jinsi ambavyo nimesema watu walipaswa kupandishwa madaraja miaka sita iliyopita na watumishi hawa wanaendelea kuchapa kazi na watumishi hawa wanaendelea kutarajiwa kwamba wa-deliver vizuri kulingana na taratibu za utumishi jinsi zinavyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo unasema ukitaka kumtawala mtu unapaswa kuhakikisha anakula na kushiba. Ikiwa tunahitaji watumishi hawa wa umma waweze kufanya kazi kwa ufanisi hatuna budi kuangalia maslahi yao ikiwemo kupandishwa madaraja, ikiwemo kulipwa/ kuongezewa mishahara, lakini pia ikiwepo kulipwa malimbikizo yote ambayo watumishi hawa wa umma wanayadai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali kuhakikisha inatoa mafunzo kwa watumishi wa umma na mafunzo siyo luxury, siyo kwamba ni starehe, hapana, tunaishi katika dunia ambayo inakwenda kwa kasi, teknolojia zinakwenda kwa kasi. Ninavyosimama hapa mbele yako ni miaka sita imepita hakuna mafunzo yaliyofanywa kwa watumishi wa umma hawa. Lakini watumishi hawa tunategemea na kuwatarajia waweze ku-deliver kulingana na jinsi teknolojia inavyokwenda jambo hili haliwezekani na haliendani na uhalisia kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ufanyike utaratibu wa haraka wa kuhakikisha watumishi hao wa umma wanapatiwa mafunzo na siyo tu suala la kupatiwa mafunzo; watumishi wetu wanapaswa kupata exposure, mtumishi unakuta yupo kazini zaidi ya miaka sita, lakini hajawahi hata siku moja kwenda nje angalau kupata mafunzo au hata kupata exposure tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi dunia inavyokwenda lazima tukubali kwamba watumishi wetu wanapaswa kwenda sambamba na the way dunia inavyokwenda kwa kasi.
Kwa hivyo basi, ushauri wangu kwa Serikali na hususan kwa Wizara husika waangalie uwezekano mkubwa sana wa kufuta hii damage ya kuwa na watumishi ambao takribani miaka sita hawajapata mafunzo na mwisho wa siku ndiyo maana tunawakuta Wakuu wa Wilaya mfano Mkuu wa Wilaya tu anakwenda kwenye eneo lake la kazi, anakutana na watumishi wale ambao wako chini yake, badala ya kuwaelekeza namna ya kufanya kazi, hata akikuta wamekosea kidogo mwisho wa siku anawachapa viboko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunaweza kudhani kwamba wanafanya makusudi, wakati mwingine hawajui hata wajibu wao, mwisho wa siku wanadhani hata kupiga viboko ni sehemu ya majukumu yao. Ndiyo maana nasema suala la mafunzo kwa watumishi wetu wa umma ni lazima na ni takwa la kisera. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo upande wa utumishi tunatambua au niseme natambua kwamba zipo taratibu na kanuni zinazotuongoza au zinazoongoza Wizara husika kuwajibisha watumishi wa umma pale ambapo wanakutwa na makosa mbalimbali. Lakini hivi ninavyoongea na wewe hapa kupitia Bunge lako Tukufu, wapo watumishi wengi ambao wamewekwa bench kwa masuala mazima ya nidhamu. Watumishi hawa wengine wamekaa zaidi ya miaka mitatu/minne mpaka mitano wako bench wanafamilia, wanatunza familia, wanapeleka watoto shule maisha yao yote yanategemeana na kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watumishi hawa hawapewi hata ile nusu mshahara ambayo kikatiba kisheria na kikanuni unapokuwa umewekwa bench, haujakutwa na hatia lazima ulipwe nusu mshahara. Lakini mtumishi huyu yuko miaka minne na wakati yuko kazini alikopa, wote tunatambua mishahara ya watumishi wetu hawa siyo mikubwa, haiwezi ikawafanya wakaishi comfortable.
Kwa hiyo, watumishi hawa wamekuwa wakikopa walipokuwa kazini, wapeleke watoto shule, wale, walipe kodi za nyumba, wengine hata kujenga hawana uwezo wa kujenga. Lakini leo hii wamewekwa bench kwa takriban ya miaka minne hawapewi hata senti wanaishije. Je, unadhani wale ambao wapo wanaendelea na kazi wanapokuwa wanaona yanayowapata hawa waliopo bench watashindwa kuchukua rushwa, kweli watakuwa ni waaminifu? Haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe kupitia Wizara na Mheshimiwa Mchengerwa nimekuwa chini ya uongozi wako ukiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Katiba na Sheria, nakujua utendaji kazi wako naujua, commitment yako naijua kwa Taifa hili, nikuombe chonde chonde uangalie ni namna gani sasa ya kwenda kufuatilia mambo haya wengine wamesimamishwa siyo kwa sababu wanamakosa, ni kwa sababu waliowasimamisha wana bifu na tu ni kwa sababu wanawasimamisha wanadhani wanawezafanya chochote as long as wao wako kwenye madaraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ambalo nimelisema kuhusiana na Wakuu wa Mikoa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wote tunatambua hawa ni wateule wa Mheshimiwa Rais. Unapokuwa mteule wa Mheshimiwa Rais, ukaenda huko chini katika majukumu yako ya kila siku unakwenda kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, sasa unapofika kule ukafanya vitu ambavyo haviendani na miongozo ambayo sisi wenyewe tuliisaini kama watumishi kwamba tutakuwa na maadili, tutaongoza kwa kuongozwa na miongozo hii ya maadili, mwisho wa siku Serikali ambayo inasimamiwa na Mheshimwia Rais inapata taswira mbaya kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-wind up natamani nisikie angalau unatoa tamko kwa Wakuu wa Wilaya, kwa Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi ukiwaelekeza namna ya kufanya wakati tunaandaa mafunzo ambayo nimeweza kuyasema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme jambo moja lingine niombe au niseme ushauri kwa mambo yote ambayo nimeelezea hapa kuhusiana na watumishi wa umma, kwa mambo yote ambayo nimeeleza hapa hususiana na utawala bora, Mheshimiwa Waziri nikuombe mambo makuu matatu; la kwanza chonde chonde waangalie watumishi hawa wa umma ambao waliwekwa bench ambao mpaka sasa hivi wengine wamekimbilia vijijini, vijijini na kwenyewe wamekuta matatizo ya wazazi wao hawawezi kabisa kujisaidia wao hata kusaidia familia zao, uchunguzi ufanyike haraka Mheshimiwa Waziri, ufanyike uchunguzi ambao hawana hatia warudi kazini na wakirudi kaziniā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga ahsante sana.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sekunde nimalize ushauri kwa Serikali. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Utashauri kwa maandishi muda wetu hautoshelezi ahsante sana.