Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha salama siku hii ya leo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa Hotuba yake nzuri yenye kuleta mustakabali mwema katika Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naanza kuchangia kwenye sekta ya mazingira, nchi yetu ya Tanzania ni nchi ambayo ina Bara, ina na Visiwa kwa pande zote mbili za Muungano. Sisi tumerithi nchi yenye Bara na Visiwa, ni vyema na sisi tukawarithisha vitoto vyetu nchi ikiwa kamilifu, kama ilivyo kwa maana ya Bara na Visiwa vyake.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuna changamoto kubwa katika maeneo ya fukwe na maeneo mengine ya maziwa kwamba, tayari bahari au maji yanapanda juu na kuyafikia maeneo ya makazi ya watu. Kuna visiwa duniani tayari vimeshapotea kwenye ramani ya dunia, kwa hivyo na sisi ni vyema tukahifadhi mazingira yetu ili visiwa vyetu visije vikapotea kwenye ramani ya dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye sekta hiyo hiyo ya mazingira tumeambiwa na kwenye Hotuba ya bajeti kwamba, Wizara ina mpango wa kuzuia utumiaji wa kuni, makaa. Lakini ni vyema pia, kuna baadhi ya uzalishaji mali katika sekta ya biashara, unatumia kuni nyingi na hivyo ni vyema tukaangalia hasa kwenye kukausha tumbaku. Tumbaku inatumia miti mingi katika kukausha. Ni vyema sasa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mazingira ikakaa pamoja, ili kuweka namna bora ya ukaushaji wa tumbaku kwa kutumia mashine nyingine za kisasa ambazo hazitumii kuni na mikaa na kukata miti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuna Taasisi zisizo za Kiserikali nyingi tu, zinajihusisha na uhifadhi wa mazingira na uoto wa asili. Ni vyema Taasisi hizo zikatambuliwa rasmi kwasababu, kuna baadhi ya Taasisi nimezikagua, wanatumia fedha zao mfukoni kuhifadhi mazingira na uoto wa asili. Wengineo wana misitu karibu ya heka (10), (15) wanahifadhi wenyewe uoto wa asili. Kwa hivyo, ni vyema katika hiyo mifuko inayokuja, ikaangalia pia na hizi Taasisi zisizo za Kiserikali iweze kutekeleza jukumu letu hili kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye upande wa Muungano, Muungano wetu jana umetimiza miaka (57) na leo imeongezeka siku moja. Muungano huu unakwenda haukutembea na ndio maana kila kitu kinachokuwa kinakuwa na changamoto zake. Na Muungano wetu unakuwa kwasababu kuna changamoto za makuzi. Naipongeza Serikali kwa kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, iendelee na hatua hizo za kutatua changamoto hizo kwa wakati muafaka na kuzitangaza kwa wananchi. Kwasababu, wanufaika wa Muungano huu ni nchi na wananchi ni vyema pande zote mbili za Muungano zikafaidi matunda ya Muungano kwa maana Bara na Visiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto mbalimbali zikitatuliwa wananchi watakuwa na furaha na Muungano wetu. Changamoto za kibiashara, changamoto za kiuchumi, changamoto za ajira kama zilivyosemwa. Mambo haya yakienda sambamba na sawia mambo mengi yatatatuliwa kutokana na changamoto za Muungano.
Mheshimiwa Spika, nikiendelea, Tanzania ni nchi ya amani, Tanzania viongozi wote walioanza kuiasisi Tanzania kutokea Hayati Mzee Karume na Mwalimu Nyerere na viongozi wote waliofuatia, wameuimarisha Muungano wetu kwa vitendo na waliopo ni matumaini yetu watauendeleza kama walivyosema wenyewe, wameahidi. Mheshimiwa wetu Rais Samia, Makamu wa Rais, Rais wetu wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi wako sambamba na maamuzi na mapendekezo ya watangulizi wao nawapongeza kwa hilo na sisi tuko nyuma yao kuwaunga mkono, kuhakikisha Muungano huu unadumu milele na milele kwa faida yetu tuliopo na faida ya vizazi vijavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jina la Tanzania ni jina zuri sana, jina lenye haiba, jina lenye mvuto nampongeza aliyetunga jina hili la Tanzania kwa dhati ya moyo wangu. Jina limetupatia heshima kubwa sana, jina la Tanzania. Ni vyema sisi wananchi wa Tanzania tukatunza amani yetu ya Tanzania kama jina letu lilivyo lina mvuto wa haiba ya Tanzania.
Naomba tumpe muda Rais wetu, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu watuletee maendeleo ya nchi yetu na kutekeleza majukumu yote yaliyoachwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli wako na dhamira ya dhati kabisa kuwaletea wananchi maendeleo. Si vyema kwa sasa hivi wakaanza kuwachokonoa, ni muda mfupi tu wana malengo makubwa, wana maono makubwa ya kutuletea maendeleo sisi watanzania. Naomba tuwape ushirikiano, tuwape imani zetu kama tulivyo. Kiungo kikubwa cha Muungano wetu kinaashiria pia kwenye hili Bunge lako.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninakupongeza wewe na Naibu wako kwa kuliongoza Bunge letu hili vizuri kwa salama na Bunge letu tukatekeleza majukumu yetu kama tulivyopangiwa kutoka pande zote mbili za Muungano tukiwa wawakilishi wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi iko salama, mipaka ya nchi iko salama. Ni matumaini yangu kwamba, na sisi wananchi tutahakikisha kuunga mkono viongozi wetu na vyombo vyote vya usalama, kuhakikisha nchi yetu hii itakuwa salama kwa faida yetu na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, Tanzania ina jina kubwa na ina historia kubwa, Muungano wetu uendelee kudumu kwa maslahi yetu na vizazi vijavyo. Ahsante nakushukuru sana. (Makofi)