Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi, na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi ya kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za makusudi kwa kuweza kuuheshimisha Muungano huu.

Mheshimiwa Spika, ikiwa jana ni siku ya Muungano, aliweza kutoa fedha za Sherehe ya Muungano na kuzigawa kwa nchi mbili hizi. Kwa hiyo, nampongeza sana na ametutia moyo, ameonesha kweli ana nia ya kwenda kuusaidia Muungano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mama huyu, Rais wetu pia anaboresha mawasiliano ya kidemokrasia, ameweza kumpa nafasi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwenda kumwakilisha katika Mkutano wa SADC. Imetoa faraja sana na ninampongeza sana, tunaona kweli njia iliyokuwa na magugu sasa inakwenda kuwa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazuri ambayo yameanza, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu, kumekuwa na changamoto nyingi kupitia Muungano huu, hususan Wazanzibari wakilalamika kupitia mitandao mbalimbali na maeneo mengi. Mengi yanazungumzwa, lakini mimi napenda kulizungumza suala zima la mfuko wa pamoja wa Jamhuri ya Muungano wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo imezungumzwa hotuba…

SPIKA: Mheshimiwa Asya, umesema mfuko…

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, mfuko wa pamoja wa Muungano. Umenielewa? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, leo imekuja hotuba ya Bajeti ya Wizara hii, lakini hatukuona kwamba kuna kipengele ambacho kina uwezo wa kuuchambua mfuko huu ili kuyaweka mambo haya sawa kuutambua kwanza mfuko huu una kiasi gani? Pia mfuko huu mgawanyo wake uko vipi? Wazanzibari wana haki ya kupata asilimia ngapi? Wanadai kiasi gani? Tunaomba mfuko huu uwe unaletwa katika Bunge lako Tukufu na uwe unajadiliwa ili kuyaweka mambo haya wazi na kupunguza kelele za mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchangia katika kipengele cha mazingira. Yamezungumzwa mengi; kumekuwa na Idara ya Mazingira, mimi nitakwenda kujikita zaidi kwenye issue nzima ya mifuko ya plastiki. Serikali ilitoa tamko la kuzuia uingiaji wa mifuko ya plastiki hasa kwa watumiaji na wafanyabiashara ambao wapo ndani ya nchi yetu. Kwa masikitiko makubwa, mifuko inaendelea kutumika na watu wanaitumia, lakini kinachoniumiza, Serikali huwa inachukua hatua kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wako chini, wao kazi yao kuuza mboga za majani pamoja na nyama na vitu vingine, wanawakamata, wanawapiga fine, na kuwafanyia mambo mengi ambayo huwa siyo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jambo hili, wako vigogo ambao ndio wanaoingiza mifuko. Tukiendelea kuwakandamiza wananchi wa chini, hatujaweza kuwasaidia. Tunatakiwa twende tukawatafute wahusika na wanajulikana; waweze kusema na kutoa hili tamko ambalo limetoka kwamba lisifanyiwe implementation kwa wafanyabiashara wadogo, wakatafutwe ambao wamewekeza na wanaoingiza mifuko hiyo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiona mambo mengi, ni kwa sababu hao ambao wanaleta mifuko hii wanahifadhiwa kwenye kwapa, lakini wanaumizwa hawa ambao wako chini. Suala hili kama tunahitaji kweli kuwasaidia Watanzania, basi Serikali hii ikaanze kuwashika hawa ambao wanaingiza mifuko hii ndani ya nchi yetu, ndipo wakamalizane na watu wa chini kwa sababu muuza mboga kama hajapewa yeye kifungashio cha mfuko wa plastiki, anakitoa wapi? Mtaji wa mboga ni shilingi 200,000/=. Kwa hiyo, lifanyiwe kazi kweli kweli. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kweli tumeamua kuondoa vifungashio vya plastiki ndani ya nchi yetu, lakini tumekuja na mbadala? Tunatoa vifungashio vya plastiki, je, tumeweza kuwapa mbadala hawa akina mama wanaouza mboga mboga au wauza nyama? Leo mtu anakwenda sokoni na shilingi 2,000/= yake anasema anataka kununua mchicha wa shilingi 500/=, dagaa zake za shilingi 500/= na kitu kingine. Mfuko wenyewe unauzwa shilingi 500/=. Kweli wataweza kuumudu? Kwa hiyo, Serikali inapoamua kupiga marufuku ya kitu fulani, kwanza wafanye utafiti, waje na solution ya kuweza kulisaidia Taifa hili ndipo wapangue hiyo mifuko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile elimu inahitajika sana na watu lazima waelimishwe kwamba tunaondoa mifuko ya plastiki kwa sababu ni hatarishi, wanyama wetu wanaweza wakala, lakini na hawa wanyama sisi tunakula nyama yake na vitu vingine vingi ili kuweza kulisaidia Taifa hili; lakini kutoka tu kusema kwamba tunaondoa mifuko bila kuwatafutia mbadala, bila kutoa taaluma, bila kuwakamata vigogo wanaotuingizia, jambo hili haliwezi kusaidia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, unanipa dakika mbili? (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Malizia dakika moja.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, la tatu,…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Ah, unaona sasa Mheshimiwa Asya unanitia katika matatizo. (Kicheko)

Taarifa inatoka wapi Mheshimiwa? Ahsante, endelea. Mheshimiwa Asya ukae chini ili uandike hiyo taarifa vizuri, uzime hapo, maana taarifa nyingine hizi ni muhimu.

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji kwamba siyo jukumu la Serikali kumwelekeza mwananchi alternative. Zipo alternatives nyingi, tulikuwa nazo tangu zamani. Tuna mifuko ya kushona, tulikuwa tunashona tangu tuko watoto, ipo inatumika. Kwa hiyo, wananchi watumie hizo alternatives. Siyo lazima Serikali iwaoneshe alternatives, Mifuko ya plastiki haitakiwi, ni kazi ya Serikali kuizuia na wananchi watafute njia rahisi kwa ajili ya kupata vifungashio mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa hiyo mchangiaji. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Asya Mwadini Mohammed, taarifa hiyo unaipokea? (Makofi)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mimi leo nimefunga na huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nadhani nilikuomba dakika mbili kwa ajili ya kulisaidia Taifa hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukurasa wa 128 umezungumza mambo mengi ambayo yanapaswa kusimamia katika Muungano huu. Kuna suala la ulinzi na usalama, lakini kwenye ulinzi na usalama kuna Wizara ambayo inahusika katika kitengo hiki. Wizara hii kwa upande wa Zanzibar haina Ofisi, hivyo inasababisha wastaafu wanajeshi ambao ni mama zetu na bibi zetu ambao wanasubiri viinua mgongo, wanalazimika kusafiri kuja bara, kwenda Dodoma na sehemu nyingine kwa ajili ya kufuatilia mafao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iweze kuwasaidia wastaafu hao maana waliitumikia nchi hii. Hivyo, kama waliitumikia wana haki zao sawa na wengine.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)