Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Amour Khamis Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na hii Wizara kwa kweli viongozi wake wamekwenda shule sana. Nawaombea Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala awaongoze, lakini pia awape mwelekeo mwema katika kutuongoza Jamhuri hii ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, niishukuru Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa hata jimboni kwangu pale wamenisaidia sana. Kuna majengo mazuri sana ambayo yamefadhiliwa na UAE na haya tumeletewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni njema sana kwetu na tunaishukuru sana na tunashukuru viongozi wa Tanzania kwa kutufikiria jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwa kuwa wamekuwa na imani ya kutusaidia jambo hili, kuna mambo mengine mazuri wanaweza wakatusaidia kama vile barabara na hata ile bandari inayotegemewa kuwa bandari ya samaki kwa ajili ya zile meli nane zile zinazotegemewa kununuliwa kwa Tanzania, naamini itajengwa Tumbe kwa kwa sababu, pale itarahisisha sana biashara baina ya Tanzania na Kenya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nataka nichangie kuhusiana na mazingira. Jimbo la Tumbe na Jimbo la Konde yameathiriwa sana na bahari. Jimbo la Tumbe bahari imeshafika kwenye soko pale na lile soko limejengwa kwa gharama sana. Katika mchango wa lile soko ni Jamhuri ya Muungano ndio imechangia pale, lakini maji yakipanda juu lile soko linafikwa sasa hivi, kwa hiyo, wakati wowote ile bahari itachukua eneo kubwa la ardhi. Kwa hiyo, naomba sana Wizara hii ya Muungano ifikirie jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri juzi alipokuwa akijibu swali alisema kwamba, kuzuia mambo yale ni kwa gharama kubwa sana, lakini naamini kutuhamisha Pemba sio gharama kubwa sana. Kwa hiyo, atutafutie hata eneo lingine hapa Tanzania bara na ndio neema za Muungano hizo kwamba kile kisiwa kikizama sisi tuwe na mahali pa kukimbilia huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jambo hilohilo la mazingira, mimi sijui kule kwetu kuna tatizo gani la mazingira kwa sababu, mikorosho inakatwa ovyo na Wizara hii ipo, miembe inakatwa ovyo. Yaani miti inakatwa kimsingi na hakuna ule ufuatiliaji wowote.

Sasa mazingira haya tunayozungumza hapa, sina hakika kwamba yanahusika huko, lakini kama yanahusika, namwomba sana kabisa Waziri na Naibu wake na kwa sababu Naibu Waziri yupo Pemba pale, basi siku moja aje Jimbo la Tumbe tuangalie namna zao la mikorosho linavyoathiriwa na miembe inavyokatwa. Sasa hivi wakati wowote kutakuwa jangwa na kukiwa jangwa maana yake ni kusema kwamba, bahari itaongeza speed ya kupanda juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wazazi wetu, wazee wetu, waasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, walivyofanya jambo hili la Muungano maana yake walifanya kwa nia safi kabisa. Huwezi ukafanya umoja kama huna nia safi. Hawa walikuwa na nia safi kabisa na wakawashawishi Watanzania waliokuwepo wakati ule wote wakaridhia kwamba, wafanye Muungano huu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa nina masikitiko kidogo kwamba, watu wametumia nguvu kubwa sana kuuchafua Muungano huu. Sasa naiomba sana Serikali ifikirie namna kwanza ya kutupa, kwa sababu Bunge hili ni jipya sana, kutupa semina angalau mtu asishindwe cha kujibu wakati akiulizwa. Pia naiomba Wizara hii inayohusika na mambo ya Muungano kwa sababu, nilisoma eneo katika kanuni zetu kwamba, ile Mifuko ya Jimbo ikishapelekwa Zanzibar watu wanatakiwa ku-report nini kimefanyika kutokana na hiyo Mifuko.

Mheshimiwa Spika, sasa Mifuko ile imetumika katika miaka 25 hii iliyopita, kuanzia mwaka 1995 mpaka juzi kwa kweli, hatujaona faida yake. Sasa Mheshimiwa Waziri akija hapa atatueleza labda angalau kwa lile Jimbo la Tumbe tu ambalo natoka niwaambie nini kwamba, Jamhuri ya Muungano hapa ilileta fedha shilingi milioni 20 kila mwaka na ilifanyiwa jambo gani. Fedha hizi hizi ndio zilizotumika kuwashawishi wananchi kule Pemba na Zanzibar kwamba, Jamhuri ya Muungano ndio adui wa Wazanzibari. Limefanyika sana jambo hilo mpaka sasa hivi sawa na kusema tu kwamba, yani wengi wa wananchi wanaamini kwamba…

MBUNGE FULANI: Taarifa.

SPIKA: Bahati mbaya muda umeisha.

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)