Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Mimi nijielekeze tu kwenye suala la NEMC. Kwanza niwapongeze Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Jafo na mwenzake Chande na maafisa wake wote, wanafanyakazi nzuri na tunatumaini kwamba kazi yao itakuwa nzuri zaidi mbele tuendako. Mheshimiwa Jafo ni mzoefu, tuna uhakika ataendesha Wizara hii vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, sisi Watanzania wa Bara na Visiwani ni wamoja. Toka tumeunda Muungano wetu mwaka 1964 hatujaona kwamba tunabaguliwa. Isipokuwa kuna wanasiasa wenye uchochezi kwa matakwa yao lakini sisi ni wamoja. Kwa umoja wetu tuendelee kupendana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna haja ya kushukuru sana Serikali ya Uingereza na huko tunakoenda tuendelee kuwashukuru. Nasema hivyo kwa sababu gani? Kumbukumbu zinaonyesha mwaka Januari, 1964 wakati wa maasi ya lile Jeshi la Tanganyika King’s Rifles tulizidiwa kabisa kwenye nchi yetu na pengine kipindi hicho Mwalimu angeondoka lakini kwa sababu wenzetu walitupa uhuru bila kinyongo alipoomba msaada walikuja wakatukomboa.

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere nadhani unge-pick topic nyingine.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naendelea na agenda nyingine.

SPIKA: Ahsante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nizungumzie mambo ya NEMC. NEMC wanafanya Environment Impact Assessment ambayo ni Tathmini ya Mazingira lakini katika nchi yetu NEMC imekuwa kikwazo kikubwa sana cha maendeleo.

Mheshimiwa Spika, historia ya NEMC ilitoka Marekani mwaka 1969, wao walianzisha mambo haya baadaye wenyewe hata mikataba ya NEMC na mambo mengine ya mazingira hawaweki, lakini kwetu sisi NEMC imekuwa kikwazo kikubwa sana. Naishauri Wizara na hasa watu wa NEMC tuangalie namna gani tuta-handle hii Tathimini za Mazingira kwenye mambo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, nataka kutoa mfano mmoja, leo ukitaka kuchimba kisima kijijini ni kazi ngumu sana. Kazi ngumu kuliko kawaida! Hata hivyo, vijijini huko tunapokwenda, mapipa ya mafuta ya ma-petrol yamejaa kwenye majumba. Sasa sijui kipi tunataka kusaidia! Sijui tunachokisaidia ni kipi? Mabipa ya mafuta ya petrol na chupa zimejaa kwenye nyumba za watu na nyumba zinaungua, lakini leo mtu akitaka kujenga kisima hata pump moja ni kesi kubwa sana kuliko kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Wizara, mimi ni Mjumbe wa Kamati, tumezungumza kwenye Kamati kwamba tutungeneze utaratibu wa kuangalia tathmini ya mazingira kwenye miradi ambayo wananchi wana uwezo mdogo na wanaweza kuifanyia maendeleo. Tunacho-encourage hapa ni watu wapate maendeleo. Tunawasukuma watu wajenge wapate miradi ya kimaendeleo, lakini NEMC yenyewe inavunja haya maendeleo. Haileti hayo maendeleo.

Mheshimiwa Spika, tuna stage za NEMC, wana hatua nyingi za kufuata kwenye tathmini ya mazingira; kuna suala la scoping, kuna screening. Screening ndiyo ya kwanza, waangalie kama mazingira unayoyaona yanaweza kuathiri watu, wanyama na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, leo hatua zote zinafuatwa. Ili upate kuchimba kisima cha mafuta, uwe na shilingi milioni tatu, shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni 10. Unachimba saa ngapi? Mradi mdogo unahitaji kupata fedha; na fedha zenyewe wameelekeza kwa watu ambao ni wataalamu, waliopewa kufanya kazi hiyo. Wale wataalamu siyo kama Waingereza, siyo kama Wamarekani ni watu wengine wa nje; ukiwapa hela, hawana kitu cha upendo. Wanachohitaji ni hela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mradi wowote wa Tanzania ukifanyiwa tathmini ya kimazingira (Environmental Impact Assessment) hawaendi kufanya review. Hakuna monitoring and review. Wakishaandika kama wameuza, mkimalizana, wanaenda jumla, hawarudi tena. Watarudi kuja kusema oh, tunakufungia kwa sababu hujafanya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba Wizara ambayo ni ya Kamati ambayo nami nimo, kwamba waangalie hili jambo sana. Tumezungumza sana kwenye Kamati, waangalie namna ya kufanya, miradi midogo inayohitaji screening, inayoinahitaji tathmini ya mazingira ipunguziwe hiyo haja ili watu wapate mazingira ya kufanya kwenye jambo lao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kufanya ni sheria za mazingira. Kuna sheria inasema mita 200, kuna sheria ya maji mita 200, kuna sheria ya mita 60; sasa tueleweke kwamba tuna sheria gani tunatumia kwenye vyanzo vya maji? Ni mita
200 au ni mita 60? Sheria hizi za mazingira ziende kwenye kata, vijiji, vitongoji na kwenye halmashauri ili wananchi waweze kuona kwamba sheria hizi zinatumikaje kwenye jambo kama hili ambalo ni nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka kutoa hiyo historia ambayo ilikuwa imeipunguza, lakini nimeongea haya ambayo nimeeleweka.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)