Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mola ambaye ameniwezesha kuweza kuwasilisha hotuba hii hapa. Lakini hali kadhalika kusikiliza hoja za Wabunge, lakini pia kunipa uhai na afya njema. Jambo hilo ni kubwa sana kwangu na hakika Mwenyezi Mungu ahsante sana Mwenyezi Mungu wangu.

Mheshimiwa Spika, ningelipenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kunipa dhamana ya kuhudumu katika Ofisi hii. Lakini nimshukuru Makamu wa Rais, Dkt. Isdor Mpango kwa maelekezo yake. Lakini kubwa zaidi naomba nimshukuru kwa dhati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa, kwa maelekezo yake, Mheshimiwa Majaliwa ni mwalimu, naomba niwaambie kazi yake professional yake ni mwalimu lakini ni mwalimu wa kufundisha kweli kweli, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikushukuru wewe kwa sababu umenipa fursa nimeweza kutoa hoja hapa lakini pia saa hizi kuweza kuhitimisha hoja yangu pamoja na Bunge lako Tukufu nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kupeleka shukrani za dhati kwa wazazi wangu, baba yangu mzee Saidi Ali Jafo Marehemu Mwenyezi Mungu ampatie pepo njema huko alipo lakini mama yangu mzazi Hadija Binti Mwalimu Madega kwa malezi mazuri sana ya kila siku na kuhakikisha kijana wao nafanya kazi kwa uadilifu. Ningelipenda kuchukua fursa hii kuishukuru sana familia yangu, Watoto wangu na Wake zangu wapenzi sana, nawapenda mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua wakati mwingine wananimisi sana...

SPIKA: Jamani makofi haya yawe ya nia njema hayo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA:…lakini kwa ajili ya majukumu ya Taifa letu ili liweze kusonga mbele.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, wangapi?

SPIKA: Na mmoja wa wake zake ni dada yangu, kwa hiyo shemeji yangu huyu bwana. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Naibu wangu Hamad Hassan Chande kwa kazi kubwa ya kushirikiana ambapo tumefanya kazi kubwa kwa pamoja katika kipindi hiki kifupi cha kuhakikisha hotuba hii inafika hapa. Lakini nimshukuru Katibu Mkuu wangu sana Mama yangu Mary Maganga kwa kazi kubwa, Naibu Katibu Mkuu Ndugu yangu Mohamed Abdul Hamis, lakini Professor Esnat ambaye yeye ndiyo Mwenyekiti wetu wa Bodi ya Wakurugenzi katika Baraza la Wahifadhi ya Mazingira, lakini Dkt. Samwel Mafungwa ambaye huyu ni Mtendaji Mkuu wa NEMC.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana watendaji wote katika Ofisi ya Makamu ya Rais kwa kazi kubwa wanayofanya, hakika mmefanya kazi kubwa sana ya kujituma kipindi chote. Nipende kuchukua fursa hii kuwashukuru Kamati zangu za Bunge zile mbili zilizofanya kazi kubwa sana, Kamati ya Sheria na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Lakini niwashukuru Wabunge wote waliochangia hapa ndani kwa michango yao mizuri sana. Wabunge wamekuwa mstari wa mbele kutusaidia sana kutuelekeza na kutushauri mambo mbalimbali hakika Wabunge tunawashukuru sana sana kwa michango yenu mizuri.

Mheshimiwa Spika, hoja yetu hii, nikushuru wewe kwasababu japo muda umekuwa mfupi lakini nimepata Wabunge wachangiaji kwa maneno takribani 26 na mmoja amechangia kwa maandishi. Hii inaonekana kwamba umetumia umahiri mkubwa sana kuhakikisha ndani ya muda mfupi wa Bunge wanapata fursa ya kuweza kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Naibu wangu, ameweza kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali hasa katika maeneo ya Muungano. Na hakika niseme kwamba kwa ujumla tumepokea maoni yote ya wajumbe na Wabunge wa Bunge hili. Lakini sisi jukumu letu kubwa sana ni kwenda kutekeleza kwa nguvu zote. Na bahati nzuri naomba niwahahakishie sisi wengine tutakuwa hatulali katika agenda hii.

Mheshimiwa Spika, tutahakikisha eneo la Muungano na Mazingira tunaenda kuweka legacy kama tulivyoweka huko nyuma katika maeneo mengine. Hili ni jukumu letu kubwa tunaenda kulifanya kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeweza kuona kwamba kulikuwa na suala zima la hoja kwamba Hospitali kuna suala zima la mikataba mingine inashindwa kusainiwa, tumeichukua hoja hii lakini naomba niwajulishe kwamba katika ule upande wa Hospitali ya Mnazi Mmoja na Ujenzi wa Barabara ya Chakechake mpaka Wete kule Pemba tayari jambo hili limeshafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwaambie Waheshimiwa Wabunge licha ya haya mawili tayari yameshafanyiwa kazi lakini yote yaliyokuwa pending tutahakikisha na ndio maana nimefanya ziara mara mbili kule Zanzibar tayari kuhakikisha mambo yote yapo pending tunayafanyia kazi. Naomba muwe na imani ya kutosha kwamba tutaenda kuwashughulikia, changamoto zote za Muungano ambazo tunajua kwamba hili jambo litaweza kutatua matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye suala zima la mfuko ule wa TASAF niwashukuru Wabunge wote wa Zanzibar, na juzi juzi nilikuwa natembelea miradi kule Zanzibar hasa miradi ya TASAF kwa kweli Miradi ya TASAF ya Zanzibar imefanya vizuri sana hasa katika upande wa majengo ya shule za sekondari na shule ya msingi. Lakini hali kadhalika vituo vya afya, na jukumu langu kubwa naomba niwahahakishie Wabunge mnaotoka upande wa Zanzibar katika upande wa miradi hii inayoelekea upande wa Zanzibar tutakuja kuisimamia kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Spika, na miongoni mwa ziara yangu nitakuja kuifanya ni kutembelea miradi yote ya Muungano sambamba na miradi yote ya Mifuko ya Jimbo ambayo fedha zimepelekewa kwa ajili mfuko wa Jimbo. Na hili nitaomba Wabunge tushirikiane kwa pamoja nitakapokuja kule nitawajulisha tuweze kukagua miradi yetu ya Mfuko wa Jimbo uliokuwapo upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana katika utekelezaji wa eneo hilo sasa hivi kiwango cha fedha kimeongezeka sasa kutoka shilingi bilioni 12 sasa Zanzibar katika kipindi kinachofuata kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye changamoto itapata takribani shilingi bilioni 36.7. Kwa hiyo, maeneo yote yenye changamoto tutahakikisha kwamba tunaenda kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, zile sheria ndugu yangu ulizozungumza zote kwa kadri iwezekanavyo tutaenda kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la mfuko wa pamoja ni miongoni mwa kero au changamoto za muungano tutaenda kuzifanyia kazi, kwa hiyo ndugu zangu Wabunge naomba tuwe na subira tu katika maeneo hayo, yote tutaenda kuyafanyia kazi kwa kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, na katika upande wa Mazingira niwashukuru sana Wabunge wote mmejadili kwa kina agenda ya mazingira. Na hasa nikushukuru sana ulipozungumza suala zima ya ile mifuko mitatu ambayo ingeweza kutatua changamoto ya kimazingira, ni kweli mifuko hii ipo na bahati nzuri nchi mbalimbali wanatumia fursa hii ya mifuko hii. Wanatumia wanapata mafanikio makubwa sana na nikushukuru sana Mbunge mchango wako mkubwa sana, jambo hili tumelichukua kwa umoja wetu wote tutaenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hata hivyo, juhudi kubwa iliyofanyika mpaka hivi sasa kupitia NEMC na Wizarani hapa tumeshaanza kupata miradi mipya hivi sasa, takribani tumesha- source fedha zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni Ishirini na Sita, Laki Tisa Arobaini na Saba, Mia Sita Arobaini ya Sita ($26, 947,646) hii tayari ni kazi tayari imeshaanza kufanyika. Na nimetoa maelekezo kwa watendaji wangu pale nimewaambia sitaki watendaji wanaokaa bure bure nataka watendaji wanaofanya resource mobilization. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yetu ni nini? Twende kupambana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na eneo hili tutaenda kulifanyia kazi kwa nguvu zote. Na hata hivyo nitaomba sana wenzangu Waziri Wizara ya Fedha kama ulivyosema tutashirikiana kwa karibu. Vile vikwazo vyote ambavyo vilikuwa ni changamoto kwa pamoja kama Serikali tutahakikisha suala zima la fedha zinazoingia basi ziweze kwenda kutekeleza miradi kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge aminini kwamba kipindi hiki tutahakikisha kwamba tunaenda kutekeleza utaratibu mzuri wa kwanza kupatikana fedha, la pili lakini kuhakikisha zile fedha zilizopatikana lazima ziende zikatekeleze Miradi ya Maendeleo. Hili ni jukumu letu kubwa tutaenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la mabadiliko ya tabia ya nchi tuseme kwamba tumejipanga na hasa maeneo ya fukwe ambayo sehemu zingine zimekatika. Na ndio maana Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kazi pale Dar es Salaam, eneo la barabara ya Barack Obama. Lakini hata hivyo kuna kazi kubwa inayoendelea kufanyika kule Pangani Tanga na maeneo mbalimbali hasa upande wa Zanzibar, ambao tumezungumza wazi kwamba kuna maeneo mengine yanamomonyoka, kwa hiyo ni jukumu letu kubwa kwamba tunahakikisha tunafanya kila liwezekanalo maeneo hasa yenye changamoto ya kimazingira twende tukalishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna yale maeneo ambayo yalizungumzwa wazi kwamba kuna baadhi ya maeneo hasa maeneo ya visiwa, visiwa ambavyo vipo hatarini katika kuzama na hili hatulitarajii ila tunaomba Mwenyezi Mungu atuepushe katika hilo. Kiwango cha maji kimeongezeka kweli katika bahari lakini kupitia Ofisi yetu tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kupitia mifuko hii mitatu jinsi gani tunaweza kupata fedha za kusaidia maeneo yenye changamoto.

Mheshimiwa Spika, hili ndiyo jukumu letu kubwa tutaendelea kulifanya, na hii nipende kusema kwamba ushauri wa kamati kama ulivyoshauri kama kwa ujumla wake tulivyosema kwamba tutajitahidi sana katika kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi maeneo haya yote kwa ujumla wake. Lengo ni kwamba wananchi wa maeneo ya Tanzania yote waweze kupata fursa ya kuona Serikali yao imeweza kuwahudumia kwa kadri ilivyoweza.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna mambo mengi yamejitokeza na mambo haya imeonekana ni suala la elimu. Ni kweli elimu ni changamoto lakini katika maeneo yote mawili, upande wa Muungano kuelewa lakini upande wa Mazingira na ndiyo maana watu waliofuatilia jana tukio la jana tulifanya lile makusudi, lengo letu ni kwamba tuweze kutumia rasilimali chache katika upelekaji wa elimu. Tumeanza mwaka huu tumeweza kutoa elimu katika utaratibu wa makongamano lakini hata hivyo lengo letu kubwa ni kuhakikisha elimu hii tunaianza kuipandikiza kwa Watoto wetu wa shule za msingi na shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimeelekeza katika Ofisi yetu suala zima la muungano tunaenda kuendesha mashindano ya insha kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari. Na hao wanafunzi watakaofanya vizuri lengo ni tuwape zawadi nzuri. Lengo ni kwamba kupitia insha itasaidia sana kuweka knowledge ya watoto kuelewa suala zima la muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima, mpango kabambe wa agenda ya kuhakikisha kwamba suala la mazingira, Wabunge wote mliojadili suala la mazingira ni kweli tatizo la mazingira ni kubwa mno, lakini jambo hili lazima awareness iwe ya kutosha. Lakini tuwe na jinsi gani mkakati wa kutosha kila mmoja wetu aweze kushiriki, ndiyo maana kupitia Ofisi yetu mwaka huu nimezungumza katika hotuba yangu mnamo tarehe 5 Juni, Tanzania tunaenda kufanya kitu cha kwanza ambacho hakijawahi kufanyika nchini mwetu,hili ni jambo gani? Tunaenda kuya-group yale mambo yote mliyozungumza humu katika jambo moja inaitwa kampeni kabambe ya kimazingira ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kampeni hiyo hatuachi mtu, kampeni hiyo tunaenda kuishindanisha mikoa kwa viashiria vyote tutakavyoviweka. Mifuko ya plastiki, upandaji wa miti, utengenezaji usafi. Kwa hiyo, mikoa yote itashindana. Tutashindanisha Halmashauri za Miji yote, Majiji yote, Halmashauri za Wilaya, tutashindanisha kata mpaka mitaa mpaka vijiji. Na tutataka tuwape Wabunge tuzo, Mbunge ambaye Kijiji chake kilikuwa cha kwanza Tanzania, hii ni kampeni kambambe ambayo tunaenda kuifanya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunaenda kuzishindanisha Wizara zote, Wizara ya Jenista Mhagama na Wizara ya Lukuvi yupi katika eneo lake alitunza mazingira mazuri. Kwa hiyo, Wizara zote zitashindana, Taasisi zote za Serikali zitashindana, Taasisi za, Private Sector zote zitashindana. Hii ni kampeni kambambe. Tunaenda kushindanisha hotel zote kuanzia One Star to Five Star mpaka Guest House ipi ilitunza mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaenda kushindanisha vyuo vikuu vyote Tanzania ni chuo gani kilikuwa the best ndani ya Tanzania katika utunzaji wa mazingvira. Tunaenda kushindanisha vyuo vya kati vyote vilivyoweza kutunza mazingira mazuri, tunaenda kushindanisha shule za Sekondari na Shule za Msingi. Hospitali za Rufaa za Mikoa, za Wilaya, vituo vya afya mpaka nani hii, katika upande huu wa elimu na upande wa afya watakaoshinda tunawapa special bonus.

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Wabunge zile shule za sekondari zitakazoshinda tumekusudia tuwape magari maalum ya shule, shule kumi bora tunaenda kuzitafuta.

Kwa hiyo, Wabunge kazi kwenu tunataka tuwashangilie Wabunge kumi ambao shule zao kumi zimepata magari hapa hapa Bungeni jambo hili tunataka tulifanye, hii ni kampeni kabambe. Lakini tunaenda kushindanisha migodi yote ipi inatililisha maji ya sumu kuharibu afya ya wananchi, kwa hiyo, tunaenda kushindanisha migodi yote na hali kadhalika tunaenda kushindanisha Hifadhi zetu zote. Tunataka tupate Hifadhi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niwaambie maeneo hayo yote na tutapata zaidi ya washindi 152, washindi hao tutawapeleka kwa ajili ya Local Tourisms tutawafanya kuwapeleka katika hifadhi mojawapo ya kitalii wakiwapo Wabunge maeneo yao waliyoshinda hii yote itakuwa ni special kazi ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kampeni hii tutaenda kufanya jambo lingine kubwa katika kampeni kabambe. Suala zima la upandaji wa miti ya matunda katika taasisi zote tunaenda ku-add value katika agenda ya nutrition katika Taifa letu. Na nimesema hapa wazi kwamba katika zile shule zinazoshinda licha ya upatikanaji wa magari ya shule tutaenda kuwapa suala zima la madawati na vifaa vya kujifundishia katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote waliyojadili Wabunge haya yapo katika Kampeni Kabambe ya Kimazingira ambayo Tanzania tutaiendesha mpaka 2025 kitaeleweka ndani ya Tanzania. Nini dhamira yetu? Tunataka tuone kwamba wageni wanapokuja waseme Barani Afrika miongoni mwa nchi iliyotunza mazingira ni Tanzania. Tunataka tuthubutu kufanya hivyo. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge haya yote mliojadili ndugu zangu naomba ni, naomba yapo. Na tarehe 5 Juni, tutawaalika Wabunge wote katika suala zima la uzinduzi wa hiyo Kampeni Kabambe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kampeni hii itakuwa na mabalozi maalum wakiwepo na Wabunge, tutawachagua Wabunge wawili, watakuwa mahiri, sijajua ni nani atakuwa, aidha Mheshimiwa Ester Bulaya ama ni nani sijajua ni nani. Hao Wabunge wawili na Mheshimiwa Kunambi pale anapiga debe kwa hiyo tutapata Wabunge wawili hao ni balozi. Lakini tutawachukua vijana wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuwa mabalozi wetu katika suala zima la kampeni ya mazingira. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na watu ambao, watu ambao kutoka Private Sector ambao wanauwanda mpana wa kimazingira kushirikiana na Serikali katika agenda hii moja tunataka tuweke katika East Africa Community Tanzania tunataka tuwe ikiwezekana watu wa mfano tunaopigiwa mfano katika upande wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge hoja zote hizi zote tumezijaza. Mlisema mambo ya NEMC, ni kweli NEMC kidogo ilikuwa ni tatizo lakini nimeanza kazi nao.

Mheshimiwa Spika, leo hii nimekutanisha wawekezaji wote waliokuwa na changamoto na ile inayoitwa TAM (Kibali cha Mazingira), watu wengine mpaka walikuwa wanalia pale wanasema wana miaka mitatu hawajapata kibali. Nimetoa maagizo nikasema haiwezekani shemeji yangu kwa mfano Ndugai anataka akaweke kituo cha mafuta pale Kongwa miezi sita hajapata kibali cha mazingira. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, watu wanapata frustration, watu wanataka kufanya uwekezaji lakini NEMC imekuwa kikwazo. Kwa hiyo, nimetoa maelekezo mahsusi, tumei-categorize miradi, group A na group B, hii yote tunataka tuibadilishe nchi yetu. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hapa halali mtu, ni mkikimkiki mpaka kieleweke. Nataka watu waisome Tanzania ya mfano kwanza upande wa Muungano lakini upande wa mazingira, tunataka tusonge mbele. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mwisho nimshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, mchakato huu wa bajeti katika Wizara hii aliuanza yeye. Naomba nimshukuru sana. Kipekee nimshukuru dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, huyu mama Ndugu zangu anapata taabu sana, kipindi hiki cha Bunge sisemi lakini kama ndiyo nyie wengine mngekuwa mnapiga dash kila siku, kazi yake ni kubwa yuko busy. Hata usiku hawezi kupumzika, naomba nizungumze ukweli. Huyu mama naomba niwaambie, kama kazi hii angepewa Ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma ndani ya siku hizi zote tunazokaa hapa naomba niwaambie katika yale mambo fulani asingeweza kabisa kwa kazi hii. Mheshimiwa Jenista Mwenyezi Mungu akulipe sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo yote, sasa naomba niseme naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki. (Makofi)