Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naomba kwanza kukishukuru Kiti chako. Vilevile naomba nishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuweza kuwasilisha kwetu hapa bajeti hii ambayo ndani yake mna changamoto nyingi, lakini naamini Bunge hili ndiyo sehemu sahihi kwa ajili ya kupatia ufumbuzi baadhi ya matatizo yao mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaapishwa hapa ulitukabidhi Katiba na Katiba hii kabla ya kuikabidhiwa tulikula kiapo. Maana yake kama sikosei ni wajibu wa Bunge hili, kwa sababu Katiba hii inako ilikotoka mpaka ikaja hapa pamoja na changamoto zote, lakini kubwa ni kwamba tuliapa kuilinda Katiba hii, nadhani mwenyewe umesema hivyo.
Kwa hiyo, mimi naomba kwa wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria, mimi si mwanasheria by profession lakini najaribu kuisoma hii kwa sababu ushauri wako umesema someni, someni, someni, nilikuwa najaribu kuangalia hasa vitu vinavyoitwa changamoto na hapa nataka nijielekeze kwenye changamoto za mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ikikupendeza ninukuu Katiba yako hii kwenye Sura ya Saba, Sehemu ya Kwanza na Sehemu ya Pili. Inasema: “Sehemu ya Kwanza, Mchango na Mgawanyo wa Mapato ya Jamhuri ya Muungano”.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zahor, tusomee Ibara.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara inasema…
NAIBU SPIKA: Ibara namba ngapi?
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 133.
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu, inasema hivi: “133. Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza akaunti maalum itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja”…” Naomba kuishia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba twende kwenye Sehemu ya Pili, Ibara ya 135, inasema: “135.-(1)Fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa fedha za aina iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, zitawekwa katika mfuko mmoja maalum ambao utaitwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.” Naomba niishie hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni nini? Nimesema tulikubaliana kuilinda Katiba hii, ombi langu kwa wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria; nimekuwa nikifuatilia na nikisikiliza maeneo mengi sana ibara hizi kila siku vinapigiwa kelele. Kwa hiyo, naomba Kiti chako na Bunge lako, endapo tutaona kwamba ibara hizi ni tatizo tokea Katiba hii imetengenezwa na ibara hizi kuwekwa kama sikosei ni mwaka 1984, maana yake tunalo tatizo sisi wenyewe kama Bunge kutokusimamia Katiba ambayo tumeapa kuilinda; ombi langu kwako, tulinde Katiba hii; hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, nimefuatilia mijadala mingi kuanzia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mpaka hotuba ya leo ya kaka yangu, Mheshimiwa Prof. Kabudi, lakini nimefuatilia michango ya Waheshimiwa Wabunge, wengi wakizungumzia juu ya ukosefu wa fedha za vitendea kazi na ukosefu wa fedha za maendeleo kwenye maeneo mbalimbali.
Sasa ambalo nimeliona kwa haraka haraka, inawezekana nitakosea mtanisahihisha, kubwa ni kwa sababu sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano tumeacha kufanya kazi yetu ya kuilinda Katiba hii ya kwamba ni kusimamia na kuishauri Serikali. Ndiyo maana tumeiacha Wizara ya Fedha kuchukua nafasi kubwa ya Serikali Kuu yenyewe kuamua nini ifanye nini isifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambalo nimeliona kwa haraka haraka, inawezekana nakosea, mtanisahihisha; kubwa ni kwa sababu sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano tumeacha kufanya kazi yetu ya kuilinda Katiba hii ya kwamba ni kusimamia na kuishauri Serikali. Ndiyo maana tumeiacha Wizara ya Fedha kuchukua nafasi kubwa ya Serikali Kuu yenyewe ya kuamua nini ifanye nini isifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapitisha bajeti hapa kama Wabunge, lengo letu na imani yetu ni kwamba tunakwenda kutekeleza kitu ambacho tumekipanga. Sasa ushauri wangu ni mdogo tu, kwamba kwa sababu Katiba hii imetupa nafasi ya kuunda Joint Financial Account na Joint Financial Committee. Ombi langu ni kwamba turudi kwenye basics hizi za sheria, kwamba Katiba hii tukiisimamia Wizara ya Fedha ifanye kazi zake mbili tu; moja, kutengeneza policy ambayo itatuwezesha kutafuta fedha na pili, ifanye kazi ya kukusanya fedha, period. Ili tuwaondolee wenzetu wa fedha makelele kwamba hamtupi, hampendi, hamtaki. Siyo kama hawapendi, lakini fedha haitoshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Bunge hili lifanye kazi yake ya kusimamia na kushauri ili liwe na nafasi ya kuweza kusema; kwa sababu nadhani tunayo Appropriation Committee hapa, sasa hii ifanye kazi ya kusema tumekusanya mbili; hizi zitakuwa za kazi hii na hizi zitakuwa na kazi hii. Wizara ya Fedha ifanye kazi zake mbili tu ya kutengeneza policy na kukusanya fedha ili Bunge hili liamue kwamba fedha hizi zitumike kwa aina eneo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)