Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hotuba ya Makidirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 12 wamechangia hotuba hii, kati ya hao Waheshimiwa Wabunge 10 wamechangia kwa kuzungumza ndani ya Bunge na Waheshimiwa Wabunge wawili wamechangia kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Tumepokea maoni na ushauri wao ambao unalenga kuboresha utendaji wetu na utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa ujumla. Maoni na ushauri wao uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni wenye tija na tunaahidi kufanyia kazi. Aidha, tunaishukuru sana Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa maoni yao mazuri ambayo tutayazingatia na kuyatekeleza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wa michango yao na nyingine tutaziwasilisha kwa maandishi kwa ufafanuzi zaidi. Mheshimiwa Joseph Anania Thadayo kuhusu suala lake la Mabaraza ya Ardhi, lile la upande wa Mahakama, uliliweka vizuri nami nisingependa tena kulizungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mabaraza ya Ardhi na changamoto, napenda kufafanua kwamba Mabaraza ya Ardhi yameanzishwa rasmi na sheria inayotawala mabaraza hayo. Mwaka 2000 Serikali ilifanya tathmini kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria kuhusu utendaji wa Mabaraza ya Ardhi hayo na kubaini kuwepo kwa changamoto zifuatazo: changamoto za kimfumo, changamoto za kimaadili na changamoto ya uhaba wa rasilimali mali na changamoto ya kiutendaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, uamuzi wa Serikali ni kuwa mabaraza hayo yabaki chini ya Wizara ya Ardhi na TAMISEMI na yaboreshwe. Kwa hiyo, Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kushirikiana na Wizara husika ili kuboresha mifumo ya utendaji wa Mabaraza hayo ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji masuala yote aliyoyaainisha yanayohusu vifungu vya Katiba vya 133 na Ibara ya 135 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mambo hayo tumeyapokea, ni mambo yanayohusu Muungano na yatawasilishwa Serikalini ili yajadiliwe na Ofisi ya Makamu wa Rais, lakini pia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, napenda nitoe indhari kwake kwamba Katiba haijitekelezi yenyewe, inatekelezwa na sheria, ndiyo maana yako mambo ndani ya Katiba ambayo huchukua muda kutekelezwa kwa sababu lazima sheria zijielekeze katika utekelezaji mzuri wa aina hiyo. Mambo ambayo ndani ya Katiba yamechukua muda kutekelezwa siyo kwa sababu Serikali haitaki yatekelezwe, lakini ni mambo ambayo yanahitaji mashauriano, majadiliano, maelewano ili hatomaye yatakapotekelezwa yatekelezwe kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespha Kabati, kwanza ni kuhusu kucheleweshwa kwa mashauri bila sababu za msingi na ametoa mifano ya mashauri ya mauaji na ubakaji hasa huko Iringa. Hata hivyo, ningependa kusema kwamba, zipo sababu nyingi za mashauri hayo kuchelewa na sababu hizo ni mtambuka zinazohusu Mahakama, wadaawa, mawakili, mashahidi na wadau wote wa utoaji haki kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikija katika mashauri ya ubakaji na hasa yanapohusu wanafamilia, moja ya changamoto kubwa zinazopatikana ni ndugu kutokutaka kupelekana Mahakamani ili kulindana na Mahakama haiwezi kutoa maamuzi kuhusu masuala hayo bila mashahidi kwenda Mahakamani na kutoa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naafikiana na Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba, kesi za mauaji ni nyingi kiasi katika Mkoa wa Iringa na sababu zake inafaa zibainishwe na wataalamu wa sosholojia na anthropolojia, kwa nini Iringa kesi za mauaji ni nyingi ili twende kwenye kiini cha matatizo ya watu wa Iringa kwa mujibu wa maelezo yake kwamba mauaji ni mengi, hatimaye pia tupunguze idadi ya kesi zinazokwenda Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kesi za mauaji nazo zinahitaji uchunguzi wa kutosha kabla ya kutoa maamuzi yanayohusika. Kwa hiyo, nalo ni eneo ambalo litafanyiwa utafiti zaidi ili kujua ni kwa kiasi gani tutapunguza idadi ya mashauri ya mauaji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maoni ya Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, moja ningependa kumweleza kwamba sababu za mahabusu kulundikana mahabusu, siyo moja tu, ziko sababu nyingi sana ambazo ameshazieleza Naibu Waziri. Kuhusu masharti ya dhamana katika mashauri ya jinai yameainishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Aidha, kifungu hicho kinaeleza wazi kuwa pale ambapo masharti ya dhamana yanataka kuweka Mahakamani mali isiyohamishika, siyo lazima kuweka hati ya umiliki wa mali hiyo, bali ushahidi wowote unaothibitisha umiliki wa mali hiyo. Kwa hiyo, wananchi hawahitaji kupeleka hati hiyo, isipokuwa ushahidi wowote unaothibitisha umiliki wa mali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama pia imetoa mwongozo wa utoaji dhamana unaoelekeza mambo muhimu ya kuzingatia katika kutoa dhamana. Hata hivyo, kama mdaawa yeyote hakuridhika na tafsiri ya Mahakama ya kifungu hicho katika mchakato wa kutoa dhamana, ana haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya juu. Wote tunafahamu kwamba Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika uamuzi wake uliotolewa tarehe 5 Agosti, 2020 katika Shauri la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Dickson Paul Sanga kupitia shauri la rufaa namba 175 la 2020 ilitoa uamuzi wa kueleza kuwa Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai ni kifungu halali kwa kujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ilieleza kuwa kifungu tajwa kinalenga kushughulikia zuwio la dhamana kwa washitakiwa wote waliofunguliwa mashitaka Mahakamani ambapo endapo wataruhusiwa kupata dhamana kunaweza kusababisha kuvurugika kwa amani, utulivu na usalama wa nchi, raia na watuhumiwa wenyewe. Ni rai yangu kwa niaba ya Serikali kwamba, watu wajiepushe na makosa haya na waendelee kuwa raia wema. Siyo nia ya Serikali wala Mahakama kuwanyima watu uhuru wao, lakini Serikali na Mahakama huchukua hatua hizo pale inapobidi na kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Mwasi Damas Kamani; moja, Tume ya Kurekebisha Sheria imekuwa inafanya mapitio ya mifumo ya sheria mbalimbali ili sheria hizo ziakisi mabadiliko yanayotokea na anayeweza kupeleka maombi hayo ni pamoja na Serikali yenyewe pamoja na Mahakama na hata raia anaweza akaiomba Wizara ya Katiba na Sheria kama mlivyofanya sasa, kupeleka maoni hayo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria ili iyafanyie utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kwamba Sheria ya Tume ya Marekebisho ya Sheria haiielekezi tume hiyo kuleta ripoti yake Bungeni. Kwa hiyo, tume haileti ripoti zake Bungeni badala yake, inapeleka ripoti zake kwa Waziri wa Katiba na Sheria ambapo huziwakilisha Serikalini ili zifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo mambo mengi aliyoyaeleza yanahusu sekta ya uchukuzi, sekta ya bima, lakini kwa sababu ameyaelekeza kwa upande wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Waziri wa Katiba na Sheria atayaangalia hayo; na kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, tutahakikisha kwamba mambo hayo nayo tunayatazama na kuona namna gani yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya Mheshimiwa Salome Wyclife Makamba; moja ni kuhusu kupitia sheria za kusimamia mambo ya umri wa ndoa. Kwenye jambo hili ningependa nieleze kwa makini sana kwamba, maelezo yaliyotolewa huko nyuma kuhusu Sheria ya Ndoa ni vizuri tukazingatia kwamba Sheria ya Ndoa isihukumiwe kwa kifungu kimoja tu. Ule msemo wa samaki mmoja akioza, wote wameoza, siyo sahihi kwa Sheria ya Ndoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema niliyowahi kuyasema, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ndio sheria ya kimapinduzi ya ndoa katika bara la Afrika, is the most progressive law of Marriage in Africa kwa hiyo tusiihukumu kwa kifungu kimoja tu. Kifungu hicho kwa maoni yangu wakati ule na bado nayasimamia shauri hilo hilo lingeweza kupelekwa Mahakama ya Rufaa sio kupitia kifungu cha 13 cha ubaguzi bali kupitia kifungu cha haki ya kuishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hapa kama ni afya ni the right to life, lakini kwa kutumia sheria ya kifungu cha ubaguzi, tunaingia katika mtego kusahau kwamba kwa hali halisi ya Tanzania lazima tuwe na ubaguzi chanya kwa faida ya wanawake, lazima tuendelee kuwa na ubaguzi chanya kwa faida ya wanawake, ndio hiyo inaitwa affirmative action ambayo pia ni ubaguzi lakini ni ubaguzi wa aina gani? Ni ubaguzi chanya na hadhari yetu ilikuwa tukiendelea kutumia mwanya wa ubaguzi kwa kifungu hiki tunaweza kuwa tunavunja msingi muhimu ambao umefanya wanawake wa Tanzania wapate ubaguzi chanya ili waendelee, wawakilishe Bungeni na ili wawe katika sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ni kuhatarisha Maisha, ningekuwa mimi napeleka shauri hilo Mahakamani, ningepeleka chini ya the right to life na sio the right against discrimination. Hata hivyo, uamuzi wa shauri la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebecca Jumi, Rufaa Na. 204 ya mwaka 2017 – 2019, Wizara ilianzisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Usimamizi wa Mirathi ili kuainisha umri wa kuolewa au kuoa kwa mwanamke na mwanaume mtawalia na hatimaye Februari, 2021, Serikali iliwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara iliwasilisha mapendekezo ya kubainisha wasimamizi na warithi wa mali moja wa mwenza anapofariki. Kwa kuwa marekebisho ya Sheria ya Ndoa yanaihusisha jamii kwa ujumla wake, Serikali ilishauriwa kuwashirikisha wananchi ili kupata maoni kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo. Kwa hiyo tarehe 17 Machi, 2021, Wizara ilianza tena kufanya mikutano baina yake na viongozi wa dini na baadaye makundi mengine ili kupokea maoni husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeandaa mpango kazi wa kuyafikia makundi yote katika jamii ili kupata maoni yatakayowezesha kupatikana kwa sheria iliyoridhiwa na wote. Hadi sasa Wizara imeweza kukusanya maoni kutoka Mkoa wa Arusha, Mwanza na Dar es Salaam kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kimila na kidini. Wizara itakapokamilisha zoezi la kukusanya na kupokea maoni katika eneo la mirathi na ndoa itayawasilisha mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Ndoa na Mirathi ili kuendana na hali ya maendeleo tuliyonayo bila kuathiri mila, desturi, tamaduni na dini zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi tumeyapokea na ushauri wa Mbunge umezingatiwa isipokuwa ule wa kwenda kulala gerezani huo ni mgumu kidogo, lakini mengine yote tumeyapokea, tutaona jinsi ya kuyakamilisha. Yale matatizo ya wale waliodhaniwa wamevamia hifadhi na matrekta yafuate utaratibu wa kawaida ili kuona ukweli uko wapi, lakini kama kweli waliingia katika hifadhi na hayo matrekta na ni hifadhi ambayo ipo katika bonde la Mto Kilombero ambalo ndilo linalolisha kiasi kikubwa cha maji Mto Rufiji, yaweza ikawa ni uhujumu uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mheshimiwa Mohamed Salum Mohammed Shaafi, Mbunge wa Chonga, kwanza sijawahi kusikia Mahakama Kuu ya Tanzania imeinyang’anya Mahakama Kuu ya Zanzibar shauri lolote, kwa sababu Mahakama haifungui kesi inapelekewa kesi. Kwa sababu Mheshimiwa Salum Mohammed Shaafi ni Mswahili anayekifahamu kiswahili vizuri nataka kuamini hakukosea aliyoyasema na kama ni sahihi aliyoyasema hata mara moja hakuna mahakama yeyote inayoinyang’anya mahakama nyingine kesi kwa sababu mahakama sio ambulance, haifuati mgonjwa, mahakama inapelekewa kesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna kesi inayohusu raia wa Tanzania wenye asili ya Zanzibar katika Mahakama Kuu ya Tanzania basi yupo aliyeipeleka, lakini haiyumkini kabisa Mahakama Kuu ya Tanzania, ikainyang’anya Mahakama Kuu ya Zanzibar kesi. Hakuna mahakama inayojipelekea kesi, lakini kama ni shauri linalosemwa, ningependa niseme hivi, shauri ambalo lipo mahakamani na linaendelea ni shauri la Mashekhe wa Uamsho.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 15 Septemba, 2020, shauri la jinai namba 21 la 2014 lililokuwepo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkoa wa Dar es Salaam lilifunguliwa rasmi katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam mara baada ya upelelezi kukamilika. Mnamo tarehe 17 Septemba, 2020, mchakato wa kuhamisha kesi husika Mahakama Kuu yaani zinaitwa committal proceedings ulikamilika, kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa tarehe tarehe 25 Machi, 2021, lakini kutokana na msiba uliotupata ilisogezwa mbele hadi mwanzoni mwa mwezi Aprili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Mahakama Kuu imeanza kusikiliza kesi hiyo namba 121 ya 2021 kuanzia tarehe 12 Aprili, 2021 na mahakama yenyewe ina uwezo wa kusema ina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo au haiwezi, sio mimi wala mtoa hoja. Kwa hiyo tuiachie Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo sasa imeanza kusikiliza shauri hilo, yenyewe itajua mwenendo unavyokwenda na yeyote ambaye hataridhika na maamuzi ya Mahakama Kuu bado anayo nafasi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo madam suala sasa lipo mahakamani, mikono yetu na midomo yetu sasa imefungwa suala hilo ni sub judice tuiachie Mahakama Kuu sasa iisikilize shauri hilo na ile video inayotembea sana ilikuwa ni video ya maneno hayo niliyoyasema mwaka 2018 kabla ushahidi haujakamilika. Sasa ushahidi umekamilika committal proceeding zimekamilika, kesi ipo Mahakama Kuu, tuiachie Mahakama Kuu itoe uamuzi wake na baada ya kutoa uamuzi wake asiyeridhika ipo Mahakama ya Rufani na mahakama hii ni Mahakama ya Muungano ndio maana yapo mashauri kutoka Mahakama Kuu Zanzibar yanakwenda Mahakama ya Rufani na yapo mashauri kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania yanakwenda Mahakama ya Rufani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar mashauri ambayo hayaji huko ni mashauri yaliyoanzia kwenye Mahakama za Kadhi au mashauri yanayohusu tafsiri ya Katiba ya Zanzibar, mengine yote yanakwenda mpaka Mahakama ya rufani na ndio pekee mahakama ya Muungano na inasikiliza rufani kutoka pande zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena, Mahakama Kuu ya Tanzania haijainyang’anya Mahakama Kuu ya Zanzibar kesi yoyote, ila kesi zimepelekwa na hizi mahakama mbili zina kitu kinaitwa concurrent jurisdiction, sasa haiwezekani mmoja amnyang’anye mwingine, sasa tumtafute mwingine lakini kama yalikuwa ni makosa ya tafsiri, maana yake kesi imefunguliwa huku basi hilo ni jambo linguine, Mahakama yenyewe itaamua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nilieleze hilo ili tuondoe munkari katika jambo ambalo linahitaji umakini mkubwa kabisa ili lisilete dhahama katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makosa yasiyokuwa na dhamana; kama nilivyosema uhuru wa mtu yeyote ndani ya Katiba yetu umewekewa mipaka. Tunazungumzia uhuru bila kwenda kwenye Ibara ya 30 ya Katiba yetu. Ibara ya 30 imeweka mipaka kwa uhuru wowote ule na mpaka wa kwanza mkubwa ni mwanzo wa uhuru wa mwenzako, ndio mwisho wa uhuru wako kwa hiyo hakuna uhuru usiokuwa na mipaka. Uhuru wowote una mipaka na hayo yameelezwa kwenye Ibara ya (30) ya Katiba yetu na pia kwenye maamuzi ya Mahakama ya Rufani ya kesi ya kukuchia ambayo Mahakama ya Rufani iliweka vigezo vya kuwekwa kwa mipaka hiyo ambavyo vipo wazi kabisa. kwa hiyo hata kwenye suala la dhamana mipaka ipo ili kuyalinda na kuyaainisha hayo ambayo yapo ndani ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka ni ya msingi sana kuhusu suala la Liwale. Tupende kueleza tu kwamba palitokea changamoto katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa Mahakama katika Mkoa wa Mtwara na Lindi. Mkoa wa Lindi haukuwa na Mahakama hata moja ya wilaya, tumeshajenga mahakama tatu Mchauka na Liwale ipo katika hatua hiyo. Kwa hiyo Liwale haijasahaulika ila ni kwa sababu ya changamoto kubwa ya mahitaji ya mahakama katika wilaya hiyo na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika muda mfupi tutaona ni jinsi gani pia Liwale tuiweke katika msimamo huo unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niliweka kiporo kidogo suala lililoletwa na Mheshimiwa Restituta Taska Mbogo. Ni kweli kabisa kabla ya uhuru sheria za kimila zilikuwa hazitambuliwi kabisa, wakoloni waliziona sheria za kimila ni sheria za kishenzi na ndoa za kimila ni ndoa za kishenzi, lakini pia Waafrika walikuwa hawapelekwi mahakamani walikuwa wanahukumiwa na Machifu au Watemi na rufaa zao zilikuwa zinakwenda kwa Mkuu wa Wilaya. Zikitoka kwa Mkuu wa Wilaya, kwa Mkuu wa Jimbo, zikitoka kwa Mkuu wa Jimbo zinakwenda kwa Gavana. Mahakama ilikuwa ni kwa ajili ya Wazungu na Wahindi tu, ndio maana tunapata Uhuru mwaka 1961 waliopigania uhuru wa nchi hii na mmoja Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye yeye mwenyewe katika essay yake ya Socialism and Rural Development anaeleza ubovu wa baadhi ya mila zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere bado aliona ni muhimu kwanza kuzitambua sheria za kimila kuwa ni sheria za watu wastaarabu na sio sheria za watu washenzi, ndio maana mwaka 1963 tunafanya codification ya Customary Law lakini codification hiyo ya Customary Law ya mwaka 1963 ilifanya pia mabadiliko ndani ya hizo sheria za kimila na ilitungwa chini ya Sheria za Serikali za Mitaa, kwa mfano kuhusu suala la wanawake kurithiwa wanapokuwa wamefiwa na wanaume zao, sheria ile iliongeza kipengele iwe kwa hiyari yake kama hataki asirithiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hiyo ilikuwa imepiga hatua kubwa kuliko sheria ya maandishi kwa sababu ndio sheria ambayo ilisema kitanda hakizai haramu, maana yake nini, haikutaka ubaguzi wa watoto ndani ya ndoa. Kwa hiyo sio kila sheria ya mila ichukuliwe jinsi ilivyo, ilifanyiwa marekebisho ili iendane na hali inayotakiwa. Sasa sheria hii imetungwa chini ya Sheria za Serikali za Mitaa, ndio maana ni muhimu tena Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Mitaa wazipitie tena sheria za mila na kuziuhisha kwa mazingira yaliyopo, lakini kuzituhumu na kusema sheria zinazotungwa na Bunge tu ndio sheria nzuri, tunarudi kuwatukana wahenga wetu kama walivyotukanwa na wakoloni kwamba sheria zao ni za kishenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siamini sheria za mila ni za kishenzi, yapo maeneo ni muhimu yarekebishwe, lakini kuzitupa moja kwa moja tukumbuke msemo wa Kiswahili Mkataa asili ni mtumwa. Hii isieleweke natetea sheria za kimila hivi hivi, lakini leo tuna mwanya mwingine, Katiba yetu ina sura nzima za haki za binadamu, bado mtu anaweza kwenda mahakamani kusema sheria hii ya kimila kwenye eneo hili inakwenda kinyume na haki za binadamu na mahakama ikafanya marekebisho ya sheria hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo yaliyorekebishwa na mahakama ni kuhusu kwa makabila yale ya ubabani, maana yake hapa Tanzania kuna makundi mawili ya makabila, makabila ya ubabani na makabila ya umamani, hakuna mjomba ni umamani. Kuanza kusema hawa ni wa upande wa wajomba ni kuwadhalilisha akinamama, ni makabila ya ubabani (Patrilineal) na makabila ya umamani (matrilineal).

Mheshimiwa Naibu Spika, huku kwenye makabila ya ubabani ukiisoma kesi ya Benardo Ephrahim dhidi ya Horaria Pastory na Gervas Kaizelege, Mahakama ilisema wazi kabisa sheria ya kumzuia mwanamke kurithi ardhi ni kinyume cha Katiba, ndio sheria ya Tanzania sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hivyo tu, ukisoma shauri lililofanywa na Jaji Kisanga kwenye kesi ya Haji Athuman Issa dhidi ya Routama Mituta imesema hivyo hivyo kwamba, sheria yeyote inayomnyima binti kurithi mali ikiwa ni ardhi ni kinyume cha Katiba. Kwa hiyo tuzisome sheria hizo na maamuzi ya mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona hatari, Watanzania tumeanza kusahau kwamba sisi mfumo wetu wa sheria ni wa common law na kwenye common law huisomi sheria tu, unaisoma sheria pamoja na maamuzi ya mahakama ili kupata jurisprudence ya eneo hilo. Ningeelewa msimamo huu kama ingekuwa tupo continental Europe na nina bahati ya kusoma katika mifumo yote miwili; nimesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, common law nimesoma Freie Universität Berlin ambayo ni civil law. Kwenye civil law hoja hiyo ina msingi, lakini sisi ni lazima daima turejee katika mashauri ya mahakama ili kujua sasa tafsiri ya sheria ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi ni watu wa common law, tuache na sisi wanataaluma sasa tuanze kutoa commentary ili watu wanaposoma kifungu cha Katiba ajue na maamuzi ya Mahakama ambayo yametoa tafsiri hiyo. Hata kabla ya hapo kuna Jaji mmoja Mkuu wa Tanzania tunamsahau mara nyingi sana na ndio alikuwa Jaji Mkuu wa kwanza Mtanzania Jaji Augustino Said; katika shauri la Ndewauyosia Daughter of Mbehanso dhidi ya Emmanuel Son of Malasi ya mwaka 1968 alisema Sheria ya Wachaga ya kuwazuia wasichana kurithi kihamba ni kinyume. Kwa hiyo ukiyachukua maamuzi yote haya, tayari yamekwishakupa mwelekeo wa nini msimamo wa sheria za Tanzania kuhusu hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu, kuna mradi ambao ulianza katika Tume ya Kurekebisha Sheria kwa sababu mwaka 1963 codification ya Customary Law ilifanywa tu kwa makabila ya ubabani, makabila ya umamani hawakuwafanyia codification ya matrilineal na hayo yameleta matatizo makubwa na hasa katika mahakama zetu. Baadhi ya Mahakimu wanaofanya hivyo ni mahakimu ya jinsia ya kike kwa sababu hawajui mfumo wa sheria wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa mmojawapo ni wa Morogoro ambapo baadhi ya watoa haki hawaelewi kwamba kule wasimamizi wa ardhi ya ukoo ni wanawake; ni mama na dada. Kwa hiyo mama na dada wanapokwenda kusema kaka hakuwa na haki ya kufanya hivi kimila hawaelewi na mara nyingi hawaelewi kwa nini wasimamizi wa mirathi ni madada na sio makaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo asilimia 20 ni muhimu Serikali sasa itafanya juhudi ili sheria za kimila za watu wa umamani ambazo mimi naamini zitawasaidia wale wa sheria za mila za ubabani na wao kubadilika wakati ndio huu. Tukizipitia zile sheria hatuna haja ya kwenda kwa wataalam wa gender wa Marekani, wataalamu wa gender wa Ulaya, twende kwa wataalam wa gender wa Kimwera, Kimakua, Kiyao, Kimakonde, Kikwere, Kizaramo, Kikaguru, Kikutu, Kinguu na Kiluguru, tutapata majibu ya jinsi gani ya kumfanya mwanamke achukue nafasi yake ambayo anaichukua katika jamii hizo za sheria za umamani. Tofauti na sisi wengi ambao tunaishi katika sheria za ubabani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nilieleze hili kwa muda kidogo ili niliweke wazi kwamba tunao utajiri ambao utatusaidia ndani ya Tanzania kubadilisha sheria zetu kwa sababu shida kubwa ya gender studies tumeanza kusoma European gender studies.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikwenda katika mkutano mmoja, wao matatizo yao makubwa sasa ni kwa nini bei ya sidiria ni kubwa kuliko bei ya shati. Sasa leo mjadala wa bei ya sidiria kuwa na bei kubwa kuliko shati Tanzania haina maana, sisi maana ni wanawake waweze kumiliki mali, wanawake waweze kufanya hivyo, lakini kwa wao mambo ya kumiliki mali na kufungua akaunti yalikwisha, sasa wanahangaikia bei ya sidiria na bei ya shati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo ambalo linahitaji umakini na niliona niliweke mwisho ili nilitolee ufafanuzi na tulifanyie kazi. Mengine yale yote tutayajibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha naomba tena Bunge lako likubali na kuidhinisha kiasi cha shilingi 78,464,886,000 kwa ajili ya Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Taasisi zake na shilingi 153,228,859,000 kwa ajili ya Mfuko wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.