Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia kwenye hotuba iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma ambaye imempendeza kwamba tuendelee kuwa na uhai huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kuishukuru sana Serikali na kuipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kuimarisha na kuboresha sekta ya madini nchini. Wote tunafahamu kwamba biashara ya madini sifa yake kubwa kwa kipindi kilichopita ilikuwa ni biashara ya kificho. Ilikuwa inaonekana ni biashara ya ujanja ujanja, biashara ya kupiga dili, biashara ambayo Watanzania walikuwa wanaisikia pembeni pembeni, lakini Serikali iliamua kuleta heshima kwenye matumizi ya rasilimali madini katika nchi hii. Ikaweka mikakati ambayo leo hii Watanzania ni washiriki kwenye biashara hii muhimu. Imeipa heshima biashara hii, kwamba katika Afrika leo nchi za kiafrika zinaiangalia Tanzania jinsi ambavyo imeleta mageuzi ya umiliki wa rasilimali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali. Mkipitia hotuba ya bajeti na taarifa yetu, mtaona jinsi ambavyo mchango wa sekta hii umekuwa ukiongezeka kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Sekta hii inasimamiwa vizuri, hongereni sana Wizara, hongereni sana Serikali. Wakati tukitoa pongezi hizi, tusibweteke, tuongeze jitihada kwa sababu bado nafasi ya sekta hii kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wetu bado ni kubwa sana. Tufanye zaidi ili sekta hii itusaidie Watanzania kuondokana na umasikini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitoe rai, Bunge lililopita liliunda tume ambapo jukumu lake lilikuwa ni kuishauri Serikali juu ya jinsi gani nzuri ya kuboresha sekta hii. Mheshimiwa Spika aliunda tume iliyoenda kuchunguza Mererani, vilevile aliunda timu iliyoenda kufuatilia mambo ya almasi. Bado utekelezaji wa mapendekezo ya tume zile haujakwenda kikamilifu. Tuongeze speed Serikali kushughulikia mambo yale ili kuondoa sintofahamu zisizo na msingi ambazo bado ziko kwenye sekta hii. Rai yangu ya kwanza ni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nataka kuipongeza Serikai kupitia Wizara kwa jinsi ambavyo imelisimamia Shirika letu la STAMICO. Shirika hili ilifika mahali tulikuwa tukizungumza humu ndani ya Bunge tunasema sasa lifutwe, lakini sasa kuna mabadiliko makubwa. Shirika hii linafanya kazi nzuri. Sasa kama tulikuwa na kigugumizi cha kulipa mtaji shirika hili kwa kisingizio kwamba halifanyi vizuri, kisingizio kile sasa kimeondoka. Twendeni tukaliongezee mtaji Shirika hili ili liwe jicho letu na msimamizi wetu na ushiriki wetu kwenye sekta ya madini kiuwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza STAMICO kwa ubunifu ambao umetuwezesha kuwa na refinery yetu kule Mwanza. Muda mrefu tumekuwa tukipiga kelele kwamba ifike mahali Benki Kuu inunue dhahabu, lakini kwa sababu huko nyuma tuliunguzwa vidole, wenzetu wa Benki Kuu wamekuwa na kigugumizi cha kununua dhahabu kupitia STAMICO na Wizara. Tumeondoa kigugumizi kile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna refinery ya kisasa inayotumia teknolojia ya kisasa ulimwenguni, dhahabu itakayosafishwa pale, purity yake ni 99.9, hatuna sababu ya kutonunua dhahabu sasa na kuiweka kwenye reserve zetu za Benki Kuu. Tukifanya hivyo, tunakwenda kuhakikisha sarafu yetu inaimarika. Sasa tusiwe na kigugumizi kwenye kufanya hilo. Tuna refinery ile, twendeni kwa haraka kuanza kununua dhahabu tuiweke kwenye reserve yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo STAMICO bado kuna changamoto. STAMICO na kampuni zake tanzu bado kuna madeni makubwa ya wazabuni waliokuwa wamefanya kazi na STAMICO. Tumefanya kazi ya kupitia, kutathmini madeni hayo kwa muda mrefu. Vyombo vyetu vya kiserikali vimefanya kazi hii, tuache kigugumizi cha kuwalipa wazabuni wale. Tena twende tukawalipe kwa haki, tusitumie ujanja ujanja wa kukwepa madeni yale, twendeni tukawalipe stahili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tumelisema kwenye taarifa yetu, Mheshimiwa Rais alipokuja hapa, aliagiza kwamba sasa twende tukachimbe madini yetu kwenye maeneo ya hifadhi. Rai yetu, tunaomba Wizara ije kwa haraka kufanya mapitio ya sheria zote zinazogusa eneo hili; yale yanayoleta ukinzani wa kauli ile (agizo lile la Rais) kufanyika, tuzifute, tuje na sheria mpya zitakazowezesha jambo hilo; na jambo hili tulifanye kwa haraka ili madini yale yaweze kutusaidia ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu Mererani. Tunafanya kazi kubwa lakini bado ina changamoto. Teknolojia tunayotumia au ile mitambo tunayotumia, bado kuna changamoto ambazo tumezisema ndani ya Kamati, twendeni tukatumie teknolojia za kisasa kuhakikisha pale kwenye geti tunadhibiti ipasavyo; na kule kwenye kamera zetu tuhakikishe tunaunganisha mfumo ule na mfumo wa kutunza kumbukumbu wa Taifa ili taarifa zetu zisipotee. Hili tunalisema hata kule Mwanza kwenye refinery, zile kamera zetu zinatunza kwa miezi sita, twendeni tukaunganishe mfumo ule na taasisi yetu ya kumbukumbu ya Taifa ili tusipoteze kumbukumbu zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado uwezeshaji wa wachimbaji wadogo tulifikirie zaidi, tuje na maarifa mengine. Najua Wizara imefanya kazi kubwa ya kuzungumza na mabenki, lakini tufanye kazi zaidi ili upataji wa mitaji isiwe kigugumizi, iwe ni jambo rahisi kwa wachimbaji wetu kuweza kupata mitaji ya kuingia kwenye uchimbaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwasilishaji wa taarifa yetu amepongeza tozo ile ya asilimia moja ambayo imefutwa, nami naongeza sauti yangu hapa, tunaipongeza Serikali, lakini kuna kazi ya kufanya. Tulipokwenda field bado wachimbaji na wauzaji wa madini walikuwa hawana taarifa kwamba sheria ile imefutwa, bado kuna watendaji wetu walikuwa wanatumia kodi ya zamani ambayo ilikuwa imefutwa. Twendeni tukalirekebishe jambo hili, na pale ambapo watu walitozwa kodi ambayo tayari ilikuwa imeshafutwa, twendeni tukafanye utaratibu wa watu wale kurudishiwa fedha zao. Maana tulichokusanya ni haramu kwa sheria. Twendeni tukawarejeshee fedha zao lakini tufanye kazi kubwa ya kutoa elimu ili sekta hii iweze kupata mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, vibali vya wale masonara kutoka nje bado kuna kigugumizi, twendeni tukaangalie utaratibu mzuri utakaotuwezesha kupata teknolojia ile kwa wepesi ili masonara wale wanapokuja kutoka nje, waweze kurithisha ujuzi ule kwa Watanzania. Baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)