Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii, lakini nikushukuru wewe kwa kuniruhusu kuwa mchangiaji wa tatu wa Wizara hii ya Madini. Nimpongeze sana Waziri na Naibu wake Profesa Manya kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa bajeti nzuri ambayo wametuletea hapa. Bajeti ambayo inatuonyesha wazi kwamba, lengo lake ni kututoa katika mchango wa Taifa wa asilimia 5.2 kwenda kwenye asilimia 10 Mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa malengo ni makubwa, ni karibu mara mbili, mchango wa Taifa unatakiwa kuwa karibu mara mbili, labda nirudi kwenye bajeti yenyewe sasa. Bajeti iliyopita, tuliweka bajeti ya shilingi bilioni 62 na katika matumizi ya kawaida tulibajeti bilioni 54, lakini bajeti ya maendeleo ilikuwa bilioni 8.5. Ukienda kwenye utekelezaji wake, utaona ile bajeti ya matumizi ya kawaida ni karibu inatekelezwa kwa asilimia mpaka mwezi Machi ilikuwa karibu asilimia 112, lakini bajeti ya maendeleo imechangiwa tu kwa shilingi bilioni 1.7. Hii inaonyesha kwamba imechangiwa kwa asilimia 22 tu kwa malengo tuliyokuwa nayo. Ikionyesha kwamba nia yetu ni njema kwenda huko tunakotaka kwenda, lakini mchango wa bajeti ya maendeleo wa Serikali kwenye Wizara hii ni mdogo, asilimia 22, lakini malengo yetu ni kwenda mara mbili. Kwa hiyo, kuna tatizo hapa wanatakiwa wawezeshwe sawasawa na malengo tuliyojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda mwaka huu, tuna bilioni 66 kama bajeti; matumizi yetu yatakuwa bilioni 51.8, bajeti ya maendeleo bilioni 15, imekuwa kama mara mbili hivi. Sasa ukijiuliza kwenye trend kama mwaka jana tumetoa 1.7 bilioni, je mwaka huu tutatoa ngapi? Kwa hiyo, kwa ushauri wangu hapa kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunatoa pesa ya kutosha kwenye bajeti ya maendeleo. Bila hivyo tutaendelea kuona ukuaji mdogo kwa sababu ni lazima input iwe kubwa ili tuone matokeo makubwa. Pamoja na ukuaji huo ukiangalia mwaka 2017, pato la Taifa lilichangiwa kwa asilimia 4.8, lakini 2010 asilimia 5.2. Sasa tunatakiwa kuingiza pesa nyingi kwenye bajeti ya maendeleo ili tuweze kuona maendeleo ambayo tunayatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye uchimbaji unaoendelea pamoja na ukuaji huu niliouona. Tunakusanya maduhuli; ukiangalia kwenye ukusanyaji wa maduhuli, tumekusanya maduhuli mengi maana yake ukiangalia kwenye bajeti hii, utaona kwamba rasilimali watu tulioingiza huko ni kubwa ndiyo sababu, bajeti ya kawaida ya matumizi ni kubwa sana kuliko bajeti ya maendeleo. Sasa je, kwa nini tusiji-involve kwenye teknolojia kupunguza hiyo bajeti ambayo ni ya matumizi ya kawaida iende kwenye bajeti ya maendeleo ili tuweze kukimbia kwa haraka zaidi? Kwa hiyo, kuna kazi kubwa ya kufanya hapo, kwa mfano, mwaka huu inaonekana imepungua kidogo kama bilioni tatu na tukaongeza kwenye bajeti ya maendeleo. Je. Kwa nini tusiendelee kuipunguza hii kwa ku-employ teknolojia, ili tuhakikishe kwamba sasa tunaweza kukimbia zaidi kuliko tunavyokwenda sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine hawa wakusanyaji wa maduhuli, nitawaonyesha uzoefu wa huko ninapotoka Jimboni Busanda. Asubuhi tunapoamka, samahani nitatumia neno zito inawezekana wengine wasilijue, kwenye illusion, mahali ambapo tunakwenda kuingiza carbon zetu kuchenjua dhahabu. Utakuta illusion ziko labda 10 au 15 lakini group la kudhibiti la kwenda kukusanya maduhuli ni moja. Kwa hiyo, utakuta illusion namba kumi itafikiwa saa tisa jioni kwa hiyo, ni hoja yangu kwamba ushauri wa Serikali waongezwe hii timu ya ukusanyaji wa maduhuli huenda tukakusanya kuliko tunavyokusanya sasa. Wasiendelee kuwa wale wale kwa sababu, tumekusanya kidogo kwa sababu na wale tuliowaweka kwenye utaratibu huo ni wachache. Tuwaongeze hawa ili watu wetu wasiwe na shida ya kuwapata wakati wa ukusanyaji wa maduhuli haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka nishauri, tumesema kuna ujenzi wa hawa wachimbaji wadogo wadogo, tuwawezeshe wachimbaji wadogo, hili nimekuwa nalisema mara nyingi, ni wapi wanapowezeshwa hawa wachimbaji wadogo? Tulisema STAMICO wanafanya kazi hii, wachimbaji wetu wadogo kwa sababu ya teknolojia na utafiti mdogo tuliokwishaufanya ndani ya nchi kwenye madini, wamehamia sasa kuchukua nafasi ya wafugaji kuishi nomadic life. Wakisikia leo madini yanasemwa yako Singida, wanakimbia Singida; wakisema yako Songea, wanakwenda Songea. Je, sisi hatuna map yetu inayoonyesha kwamba dhahabu iko wapi, helium iko wapi, makaa ya mawe yako wapi, ili hawa watu wasihamehame kwa mtindo huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho nataka niseme, kuna mahali watu wetu wanachimba uchimbaji mdogo, lakini dhahabu inatakiwa ichimbwe labda kwa wachimbaji wakubwa, inapatikana labda kilometa moja. Tumefanya utafiti huu ili tuwaambie wasiendelee kuchimba hapo dhahabu iko mbali hawataweza kuchimba kama wachimbaji wadogo wakaipata?
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nafikiri niishauri Serikali, tutengeneze Mfuko wa Madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ili vifaa vya uchimbaji vipatikane mahali fulani wanapoweza kuazimwa au wanapoweza kulipia, kwa sababu, sasa hivi hatuna mahali. Ukimwambia mtu aanze kuchimba leo dhahabu au aanze kuchimba makaa ya mawe, atahitaji bilions of money kufikia hayo madini, ana hiyo mitambo? Hana. Hivyo, naomba tutengeneze Mfuko wa Wachimbaji Wadogo ambao tutau-tax kutoka kwenye mapato yetu tunayoyapata sasa hivi ili watu wajue kuna center ya kuweza kuwasaidia mahali fulani ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, swali langu, Wizara inayo mpango endelevu wa madini ndani ya nchi hii? Tuna deposit ya dhahabu, tuna deposit ya almasi, je tunajua tutakuwa nayo hii dhahabu na almasi kwa miaka mingapi? Tukiulizana leo, tusije tukaendelea kuchimba baada ya miaka 15 tukabaki tuna sifuri na mwisho wa siku hatujawa na mpango endelevu ambao unatuonyesha ni nini tunakifanya ndani ya nchi! Wizara iandae mpango endelevu unaoonyesha haya madini tuliyonayo yanaweza kwenda mpaka muda gani? Ili mashimo yaliyochimbwa kwenye maeneo yetu kwa kuwa wao ndiyo wanaosimamia mazingira ya maeneo yaliyochimbwa, yaanze kufukiwa kwa sababu yamekuwa mengi sana katika maeneo tuliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisemeā¦.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)