Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Madini. Baada ya mageuzi makubwa katika sekta hii ya madini, tumeshuhudia sasa mabadiliko makubwa. Mchango wa sekta umeongezeka, kukua kwa sekta kumeongezeka kwa kiasi kikubwa. Mchango wake sasa hivi ni asilimia 5.2 ya pato la Taifa na bado unaendelea kwenda, imekuwa projected kwamba, utaongezeka zaidi. Kwa hiyo, niwashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote ambao wameweza kutufikisha hapa na hasa kwa kuweza kutupa matokeo ya haraka kwenye maeneo mbalimbali ya sekta hii na hasa kwenye utoroshaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kama nitakavyoeleza hapo baadaye tumeshuhudia sekta hii kukua lakini, hatujashuhudia sekta hii kuongeza uzalishaji kwa maana ya migodi mipya. Nianze kwa kusema Bajeti ya Wizara hii ni bilioni 66.8; kati ya hizo, bilioni 15.0 ni miradi ya mkakati na katika miradi ya mkakati tunaona kuna bilioni kama tatu zinakwenda STAMICO na bilioni 3.5 zinakwenda GST. Ni jambo jema kwa sababu, wengi wameongea hapa kwamba utafiti ni jambo la muhimu. Nipende kukazia maisha ya sekta ya madini yanategemea sana utafiti na utafiti wa uhakika. Wengi wamelia na kusema maneno mengi hapa hata kwa wachimbaji wadogo kuhusiana na suala la utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kusema kukua kwa sekta hii na kuongezeka kwa mchango wa sekta hii, kwa kiasi kikubwa bado naweza nikasema sio himilivu, inatakiwa tufanye kazi za ziada na sababu kubwa ni kwamba, bado sekta hii kwa kiasi kikubwa inategemea dhahabu kama zao ambalo ndio hasa linaifanya hii sekta ionekane na itoe mchango mkubwa. Kwa maana hiyo basi, kama nia ni kufanya by 2025 tufikie asilimia 10 ya pato la Taifa, bado tuna kazi kubwa kwa sababu, napenda kuliambia Bunge lako kwamba, dhahabu ina tabia ya kupanda bei na kushuka bei.
Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba bei imekuwa ikipanda na nilishawahi kusema humu ndani kuna majira yanakuwa mabaya. Kwenye sekta ya madini tunasema kuna bust na kuna boom, tupo kwenye boom la madini lakini bust na yenyewe iko mahali fulani. Kwa hiyo, tujiandae na cha kufanya kama nilivyosema mara ya mwisho tuanze kuangalia madini mengine na madini haya, tunasema ni madini ya viwanda (industrial minerals). Tuna madini ya kila aina katika nchi hii, tuna utajiri mkubwa cobalt, graphite, helium gas, rare earth, mwenzetu mmoja ameongea kuhusu niobium hapa asubuhi, kwa hiyo, tuangalie haya.
Mheshimiwa Spika, vile vile, tujitendee haki kwa kuangalia ukuaji wa sekta hii, kwa kuangalia jambo la exploration. Ni ukweli usiopingika kwamba, sekta ya utafiti kwa maana ya pesa ambayo inaingia ndani ya nchi yetu kufanya utafiti imepungua sana kama haipo kabisa. Hata kwenye Bajeti ya Mheshimiwa Waziri sijaona akiongelea pesa ya utafiti na utafiti unaoendelea ndani ya nchi kwa pesa inayotoka nje kuja kufanya utafiti hapa ndani, ni ya muhimu. Lingekuwa ni jambo jema tukafanya utafiti kwa pesa zetu, tunalipenda lifanyike hilo, maana litatupa nguvu ya kuweza kujua nini kiko wapi kwa ukubwa gani na kwa miaka mingapi? Hiyo itatusaidia kuweza kuongea na watu wote ambao wanataka kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali halisi tuliyonayo, inabidi tukubali kwamba uwezo huo hatuna. Tukitaka tufanye ili tujue kila kitu kiko wapi katika nchi hii, hiyo bajeti tunayoongelea ya bilioni 400 au 500 ya Wizara ya Madini itabidi tuzidishe mara tatu au mara tano tuizike yote kwenye exploration. Sidhani kama litakuwa ni jambo la busara wakati tuna mahitaji mengi makubwa. Hata hivyo, sekta binafsi inaweza kuifanya hilo, tena kwa vizuri kabisa. Tukubaliane kabisa kwamba, katika utafiti kuna utafiti wa aina mbili; kuna utafiti ambao unafanywa na migodi ambayo ipo tayari sisi tunaita, brown exploration na utafiti huu unaendelea bado kwa migodi ile kwa sababu, wanataka wao waendelee kuongeza mashapo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utafiti tunaouongelea ambao ni mkubwa wa kuongeza na kukuza hii sekta, ni utafiti unakwenda kwenye maeneo mapya ambayo bado hayajaonekana tunaita green field exploration. Tunahitaji kuwa na uwekezaji kwenye eneo la green field exploration, ni muhimu kwa uhimilivu wa sekta ya madini.
Mheshimiwa Spika, nNipende kusema vile vile pesa nyingi za uwekezaji katika sekta hii ya madini kwa upande wa exploration, mara nyingi ni pesa za watu mbalimbali wanakusanya na kuziweka na kuzifanya ziwe available kwa nchi au kwa wawekezaji. Nadhani baada ya miaka mitano ya kuwa na mafanikio mazuri baada ya mageuzi makubwa kwenye sekta hii, lazima tuanze kujiuliza maswali magumu. Hatuna budi kujiuliza ni kwa nini kwanza, hatupati hizi pesa kutoka nje za uwekezaji kwa maana ya exploration?
Mheshimiwa Spika, vile vile ni miaka 10 sasa, hatujaona migodi mipya ikifunguliwa katika nchi yetu. Tunasikia michakato ya kutaka kufungua migodi, lakini ni wazi tunatakiwa kuwa makini sana ili tuweze kuhakikisha kwamba nchi yetu inanufaika, ni jambo jema. Pia ni wazi kwamba, bado tunaweza tukanufaika kwa kufanya fine-tuning tu katika sheria zetu. Hatuna sababu, tumefanya makubwa kwa kufanya mengi ya kubadilisha sheria, lakini kuna mambo madogo tunaweza tukayafanya ambayo yanaweza yakatupa faida zaidiā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Deo Mwanyika, dakika tano zimeisha.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, tuliambiwa dakika saba.
SPIKA: No, ni tano! Ili orodha niliyonayo iweze kutimia, tunashukuru sana. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, basi, naunga mkono hoja. (Makofi)