Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kutoa shukrani zangu kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu. Nianze kwa kuunga mkono hoja na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Biteko na timu yake na Wizara ya Madini kwa ujumla kwa ushirikiano ambao wanatoa kwa Wizara tunapotekeleza majukumu yetu. Kwa hiyo, nawapongeza na kuwashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba, tumepewa jukumu la kulinda mgodi wetu wa Tanzanite kule Mererani, lakini labda niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, pia ni kwa mujibu wa Ibara ya Katiba ya…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nimeshawaomba tena na tena; eeh, taratibu.

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, utanilinda dakika yangu.

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 105 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inatupa fursa ya kuendeleza kusimamia ulinzi na maeneo ambayo ni muhimu ya kimkakati. Kwa mgodi huu tunaoulinda pia kwa maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama, tunalinda kule Mererani.

Mheshimiwa Spika, niseme, ukipewa kazi ya ulinzi, siyo jambo dogo na hasa lazima tuzingatie weledi ili tuweze kuvuka salama. Kwa hiyo, jeshi letu linafanya kazi nzuri, uniruhusu niwapongeze sana Askari walioko kwenye maeneo haya, wanafanya kazi kubwa kwa uadilifu wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kuna changamoto nyingi, lakini vijana hawa ambao wako kwenye eneo la Mererani kwa ujumla, Mheshimiwa Mbunge alijaribu kukumbusha hapa kwamba tunakagua watu kati ya 8,000 na 10,000, lakini kwa hali halisi ukienda kwenye eneo tunakagua zaidi ya 10,000. Kuna siku ambazo tunakwenda mpaka kukagua watu 15,000 kwenda 20,000; na tulikuwa tuna sehemu mbili tu za kukagulia.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Wizara ya Madini kwamba baada ya kuwa na maombi ya kuongeza maeneo ya ukaguzi, sasa kuna vyumba takribani 10 vinaongezwa ili tuendelee kuboresha ulinzi katika eneo hili. Kwa hiyo, vijana walioko pale wanafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, ukifanya kazi ya ukaguzi unalazimika wakati mwingine kufanya upekuzi na hii ni kawaida pale ambapo unakuwa na mashaka. Mashaka yanatoa uthibitisho kwamba, saa nyingine tutakapokuwa na mashaka tunakamata haya madini ingawaje Waheshimiwa Wabunge hapa umesikia wakizungumza kwamba, labda ni kidogo kidogo; lakini hiyo kidogo tunayokamata kwangu mimi naamini kwamba inazuia madini kuvushwa kwa wingi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba tutaendelea kufanya kazi hiyo, lakini tunavyofanya ulinzi, tunafanya doria, lakini tukiwa katika maeneo ya ulinzi tunashirikisha vyombo hivi vya ulinzi mbalimbali. Kwa hiyo, hatuko peke yetu. Mheshimiwa Mbunge Ole-Sendeka hapa rafiki yangu amezungumza hapa na kwa uchungu mkubwa, lakini niseme tu kwamba kazi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ole-Sendeka atakumbuka kwamba tulivyotembelea tukiwa na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Ole-Sendeka namshukuru, alikuja na tulikwenda kukagua sehemu ya ukaguzi tukiwa na Mheshimiwa Mbunge. Nawapongeza sana Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa sababu ya namna nzuri walivyofanya kumshirikisha Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Mbunge alitoa hoja zake na rai yake kwenye Kamati.

Mheshimiwa Spika, pia tarehe 12 mwezi wa Nne wakati tulikwenda kwenye Kamati kujibu maelekezo ya kamati baada ya ziara ile ya tarehe 16 mwezi wa Tatu, tulikuwa tumepata maagizo ambayo ninayo; yako maagizo 13 ya Kamati; na kati ya maagizo yaliyokuwepo, liko agizo la kufunga scanner katika maeneo ya ukaguzi ambalo wenzetu wa Utumishi na Utawala Bora wanalifanyia kazi. Tutakapopata scanner tutakwenda kutoka kwenye hii tradition way ya kukagua, tuanze kukagua kisasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Ole-Sendeka alipata nafasi wakati wa ziara na wakati wa Kamati. Haya maelekezo yaliyotoka kwenye Kamati ninaamini kabisa Mheshimiwa Ole-Sendeka yana mchango wake kwenye Kamati. Nami naamini hivyo kwamba tunaendelea kuyafanyia kazi. Niseme kati ya maagizo haya, yako maagizo sita ambayo tayari tulishayatekeleza kwa kushirikiana na Wizara ya Madini, vile vile yako mengine ambayo yako kwenye hatua, tunaendelea kuyatekeleza.

Mheshimiwa Spika, naomba wananchi na wachimbaji waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vyetu. Vyombo vyetu vinafanya kazi kwa weledi na kwa uzalendo wa hali ya juu na saa nyingine tutawasikitisha kuwaletea tuhuma au niseme kuwaletea maneno ambayo yatawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Spika, mimi kama nimepewa dhamana kwenye Wizara hii, nitaendelea kusimamia maelekezo ya Kamati, nitaendelea pia kusikiliza Waheshimiwa Wabunge na nimhakikishie tu Mheshimiwa Ole-Sendeka kwamba tuko pamoja kwenye jambo hili, pale ambapo tutapata scanner tutakwenda kufanya ukaguzi kwa staha na kwa uzalendo na kwa kushirikiana na wananchi. Ahsante sana.