Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Wizara imepokea michango mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wabunge wameitoa kwa matamshi na Wabunge wengine kwa kuandika. Pia tumepata ushauri na maoni na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ni muhimu kwetu katika kutekeleza majukumu yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla ushauri na maoni pamoja na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge kwetu sisi ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Madini.
Napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia hotuba yetu. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 22 wamechangia hotuba hii kwa kuzungumza na wajumbe wawili wamechangia kwa kuandika. Nichukue fursa hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, hoja zote zilizowasilishwa hapa na Waheshimiwa Wabunge, sisi kama Wizara tunazichukua kwa uzito wa aina yake na kwamba itakuwa ni tool nyingine ya kufanyia kazi katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha.
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliosema, hata waliotuandikia na hata wale tuliokutana nao tukazungumza nje ya Bunge. Tunaheshimu michango yao, na tutaifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo sasa naomba nijielekeze kutoa ufafanuzi kwa hoja kidogo tu zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kutokana na muda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kueleza kwamba usimamizi wa Sekta ya Madini hautegemei mtu mmoja kwa maana ya Wizara ya Madini, unawategemea sana Waheshimiwa Wabunge ambao wao ndio wawakilishi wa watu mahali huko tunapofanya shughuli za uchimbaji madini. Tumefanya ziara maeneo mbalimbali, tumeona kiu ya Watanzania walio wengi ya kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya Madini na tumewaona Waheshimiwa Wabunge wengi walivyo na kiu ya kuona madini yanawanufaisha Watanzania.
Mheshimiwa Spika, hiyo spirit peke yake kwangu mimi ni kiashiria tosha kwamba usimamizi wa Sekta ya Madini ni wetu sote. Kwa kweli naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, hakuna hoja hata moja ambayo sisi tutaichukulia kama hoja substandard. Hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni tool yetu ya kufanyia kazi na kuanzia leo nataka niwahakikishieni kwamba hoja zote walizozitoa tutaziandikia majibu na tutaziwasilisha kwako ili Waheshimiwa Wabunge waweze kuzipata.
Mheshimiwa Spika, suala la kwanza nieleze kwa kifupi ni suala la local content. Suala hili limeongelewa kwa hisia kubwa sana na Waheshimiwa Wabunge, local content huko ndiko uliko mzunguko wa fedha kwenye Sekta ya Madini. Ukiruhusu mzunguko ulioko kwenye local content uende kwa watu wa nje ukawaacha watu wa ndani, manufaa hayo hayaweza kupatikana.
Mheshimiwa Spika, tulipotoka mbali, tumetoka kwenye mazingira ambayo mchele wa kulisha migodi ulikuwa unatoka nje ya nchi, nyanya zilikuwa zinatoka nje ya nchi, vitunguu vilikuwa vinatoka nje ya nchi, walinzi wanatoka nje ya nchi, Wahasibu wanatoka nje ya nchi, watu wa manunuzi wanatoka nje ya nchi, watu wa Human Resource wanatoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia biashara zilizokuwa zinafanywa na migodi, volume kubwa ya fedha zile ilikuwa bado inarudi nje ya nchi na kwa gharama kubwa sana. Tumefanya mabadiliko hapa tukatoa mamlaka kwa Tume ya Madini ku-approve kila aina ya manunuzi, mgodi sasa hivi hata ukitaka kununua kikombe cha chai, ni lazima upate kibali cha Tume ya Madini. Kwa sababu hiyo nataka nitoe taarifa kwa Bunge lako Tukufu, tulipofika tumepiga hatua kubwa. Leo wakati manunuzi ya Mgodi wa GGM yaliyofanyika kwa mwaka huu tulionao jumla ya Shilingi bilioni 849.9 ni fedha zilizofanyiwa biashara kwa local content kwa wazabuni wa ndani na Shilingi bilioni 182 peke yake ndizo zilizofanyiwa na watu kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, Mgodi wa Buzwagi bilioni 105.8 ni zabuni zilizofanyiwa biashara na Watanzania wa hapa ndani na wakati huo huo bilioni 95 ni watu wa nje. Mgodi wa Shanta bilioni 106.5 ni bidhaa za ndani na huduma zimetolewa ndani, bilioni 30 peke yake ndizo bidhaa kutoka nje au huduma kutoka nje. Mgodi wa WDL bilioni 53.6 ni biashara iliyofanyika ndani na bilioni 5.4 peke yake ni biashara iliyotoka nje. Hatua hii ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, hata bidhaa kubwa ambazo walikuwa wanazungumza Waheshimiwa Wabunge mfano mafuta, vipuri, consumables na vitu vingine vyote kwa kiwango kikubwa ni biashara zinazofanyika hapa ndani. Biashara ya mafuta kwa mfano, kwa Geita, mtu anayefanya biashara ya kupeleka mafuta kwenye mgodi wa GGM ni Mtanzania yupo Geita kwa asilimia 30. Ukiangalia biashara ya kupeleka nguo, kupeleka vitu vyote unavyoviona zaidi ya asilimia 70 biashara hii inafanyika hapa ndani.
Mheshimiwa Spika, CSR inayozungumziwa, tulipotoka tukiangalia Mheshimiwa Musukuma na Mheshimiwa Kanyasu watakuwa mashahidi; kabla hatujarekebisha sheria hapa CSR fedha zilizokuwa zinatumika zilikuwa nyingi na tena hazina uhalisia na wala ile miradi iliyokuwa inatumika hayakuwa mahitaji ya watu wanaozunguka migodi, matokeo yake yakawa ni nini? Matokeo yake ni kwamba fedha nyingi zinaonekana zipo traded kwenye migodi, lakini watu wanaozunguka ile migodi bado ni maskini wa kutupwa, bado watoto wao wanakaa chini hawana madarasa, bado watu wale hawana maji.
Mheshimiwa Spika, tukafanya mabadiliko kwenye sheria hiyo Mheshimiwa Musukuma atakumbuka shule moja pale Geita ilijengwa kwa bilioni tisa wakati shule ile haina ghorofa tulivyokwenda kufanya valuation tukakuta fedha hizo hata nusu yake isingeweza kutosha tumefanya marekebisho. Leo mpango wowote wa CSR unaotaka kufanywa na mgodi mtu aliye na wajibu wa kuusimamia mpango huo ni halmashauri husika na halmashauri yenyewe ina kazi mbili, baada ya kuwa imejiridhisha na mpango huo unaendana na mahitaji ya halmashauri kazi ya pili ni kuangalia value for money.
Mheshimiwa Spika, kuna wakati fulani kuna miradi ilikuwa inatengenezwa, wanakwambia mfuko mmoja wa simenti unauzwa Sh.30,000 wakati ukienda kwenye soko unakuta mfuko mmoja unauzwa Sh.15,000. Mambo hayo yote tumeyabadilisha sasa hivi value for money inaangaliwa na manufaa haya yanaonekana. Mheshimiwa Kanyasu hapa atakuwa shahidi Geita ilivyokuwa kabla ya kusimamia sheria hii na sasa hivi ni tofauti sana, imebadilika kwa sababu miradi mingi halmashauri wanasimamia.
Mheshimiwa Spika, yako matatizo tunayapokea ya usimamizi na nidhamu ya matumizi ya fedha; sisi kama Wizara Madini ambao tuna wajibu wa kusimamia local content pamoja na TAMISEMI, tutaendelea kusimamia matumizi ya fedha hizi ili yaweze kuwa na tija.
Mheshimiwa Spika, limezungumzwa jambo moja la Mradi wa Niobium. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Njeza, hili jambo linaweza likaonekana Wizara tunachelewesha, nimwombe Mheshimiwa Oran Njeza awaambie wale wawekezaji tuliokuwa tunaendelea nao waje tupo tayari.
Mheshimiwa Spika, bado tumemaliza mambo mengi tunabishana mambo mawili tu; madini ya niobium, wao wanataka tuya-treat kama madini ya viwandani ambayo yanatozwa mrabaha wa asilimia tatu, sisi tuna ya-group yale madini kama madini ya metal na yenyewe yanatozwa asilimia sita. Sasa ubishani huo hatuwezi kuu-resolve kwa kuzungumza tu, ni lazima waje tuzungumze.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunalozungumza nao ni kwamba wanataka wachimbe kwenye Kilima cha Pandahill wakishachimba processing ya madini hayo wayaondoe kwenye Kilima waende wakafanye kwenye process ya EPZA. Sheria ya Madini inaeleza uchimbaji wa madini ni chain nzima, kuanzia uchimbaji na process. Sasa tunawaambia tukifanya tendo la kutenganisha huu mradi, uchimbaji ukafanyika kwenye mgodi na process ikafanyika mahali pengine, kwanza tutakuwa tumevunja Sheria ya Madini, lakini pili kwenye EPZA kuna misamaha mingi sana ya kodi.
Mheshimiwa Spika, kodi ya mapato ya asilimia 30 itakuwa na msamaha kwa muda wa miaka 10; kodi ya zuio na kodi nyingine pamoja na kodi ya pango, bado tunaendelea kujadiliana nao. Bahati mbaya baada ya kuwa tumewaambia hoja hizi hawakurudi tena. Kwakuwa Mheshimiwa Mbunge anaweza kuwa sasa...
SPIKA: Waheshimiwa wote mnaokuja kukaa na kuongea Mheshimiwa Waziri Mkuu nilishatoa maelekezo, lakini basi nawaagizeni mtakaa kiti kile kama AG hayupo, mumlinde angalau afya yake na yeye. Haiwezekani watu 50 au 60 kila siku wanakutana naye hapa kwa hapa, hebu jaribuni sana kupunguza, hata kama ni Mawaziri kama hauna shida ya maana usiende pale, kwa sababu ana wajibu wa kuwasikiliza Wabunge na wale mnaokwenda basi kaeni kiti cha mbali pale kidogo ili kuweka ile distance ambayo ni salama. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, endelea.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo milango yetu ipo wazi Kampuni ya Panda Hill wakaribie wakati wowote tuzungumze, lakini watusaidie na wao ni lazima tulinde manufaa ya nchi yetu kwenye rasilimali madini, kwa sababu hizi rasilimali kuna siku zitakwisha.
Mheshimiwa Spika, kuja jambo lingine hapa limeelezewa la TEIT, kwamba TEIT hajapata fedha. Naomba kutoa taarifa hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba TEIT walishapata fedha za maendeleo Sh.850,000,000 ambazo wamekwishapata kwenye bajeti yao. Hata hivyo, kuna mzozo mmoja unaozungumzwa hapa wa reconciliation ya bilioni 30 ambao Mheshimiwa Jesca alikuwa akiueleza sana. Ni bahati njema kwamba Mheshimiwa Jesca amekuwa consistent na jambo hili Bunge lililopita kwenye bajeti alieleza tulitoa majibu, lakini sijachoka tutatoa ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, kilichotokea, hakuna hata shilingi moja iliyoibiwa wala kupotea, kilichotokea TEIT wanachofanya wanakwenda kwenye mgodi X wanaomba malipo waliyolipa Serikalini, wanapewa iwe orodha ya malipo. Wanakwenda Serikalini wanaomba kile walichopokea, wanafanya reconciliation. Kilichotokea ni kwamba reporting ya Serikali na reporting ya migodi miaka yao ya fedha inatofautiana, ndio maana tulivyomtuma CAG Novemba, 2019 alituletea taarifa ya hoja hiyo, hizo fedha zote zilionekana hata kwenye bank statement zipo.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa bado linaendelea kuzungumzwa, nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Jesca na Watanzania hakuna shilingi hata moja itakayoliwa kwenye migodi, inasimamiwa kwa uwazi na kwa ukweli na hata kwenye Semina tuliyoifanya uliyotupa kibali, Mheshimiwa Jesca nilimwambia, nadhani hapa leo aliamua kutuchangamsha kidogo kulirudia jambo hili, lakini majibu anayo.
Mheshimiwa Spika, limeongelewa jambo lingine la blacklisting ya wafanyakazi, ni kweli wapo wafanyakazi kwenye migodi wanakuwa blacklisted na nilishatoa maelekezo pamoja na wenzangu Wizarani kwamba, watu wanaoweza kuwa blacklisted ni wale waliotenda makosa makubwa sana. Mtu amechelewa kazini siku mbili unamfukuza kazi, halafu una m-blacklisting asiajiriwe kwenye migodi mingine, tulishatoa maelekezo ni marufuku na kuna Watanzania wawili waliokuja kwangu waliokuwa na kesi za namna hiyo niliwaambia wawaondoe kwenye orodha yao ya blacklisting.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii niwaombe Watanzania wale wote walioajiwa kwenye migodi, wajenge image ya nchi yetu, tunapambana kuhakikisha kwamba Watanzania wanachukua ajira zote kwenye migodi, hivyo ni lazima wawe waaminifu. Leo ninavyozungumza migodi mikubwa ya GGM asilimia 97 ya wafanyakazi wote ni Watanzania. Migodi ya North Mara asilimia 98 ni Watanzania hata Country Manager wa Mgodi wa North Mara kwa maana ya group nzima ya BARICK hapa Tanzania ni Mtanzania anaitwa Georgia na ni mwanamama yupo, amekuja hapa. Yule mgeni aliyekuwepo hapa tumemaliza mkataba wake ameondoka Georgia sasa…
SPIKA: Meneja wa mgodi huo unaohusika hebu asimame. Makofi kwake waheshimiwa. Hongera sana dada yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, unaweza ukaendelea.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo…
SPIKA: Mheshimiwa Meneja hawajakuona kamera hizi hazijakuonesha. Hata Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaona, hata mavazi yake enhe! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Waziri wa Madini, endelea.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Labda wengine, lakini mimi niliwahi kwenda kwenye mgodi mmoja nitatoa mfano, nikazungumza maneno mengi na wenye mgodi. Baadaye wakaniomba side meeting, wakaniambia tunaomba na wasaidizi wako tukae kule chumbani, jambo walilokuwa wanalalamika ni uaminifu wa baadhi ya watu wetu, kwa kweli wanatuchafua wote, wanatuondolea heshima wote. Wale wanaopata nafasi ya kusimamia migodi hii wasimamie kwa haki na weweze…
SPIKA: Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa vile anaongelea neno la uaminifu. Nilizungumza hapa siku moja nimepigwa na mitandao yote, kwamba ninaongea kitu cha kufikirika. Leo Waziri anasisitiza. Endelea Mheshimiwa Waziri jambo hili, uaminifu unalipa. (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, lingine wale Watanzania kama kina Georgia wanaopata nafasi za kuendesha migodi hii, wawasaidie Watanzania wengine. Wanaowa-blacklist Watanzania hawa ambao wapo kwa kuwaonea wala sio Wazungu tusiwasingizie, ni sisi wenyewe. Nataka niwahakikishie jambo hili haliwezi kufanyika tena tumeshatoa maelekezo kwa watu wote wahakikishe wale waliofanya makosa makubwa ndio wanakuwa blacklisted, lakini makosa madogo madogo ya kawaida mtu amechelewa kazini, hayo haya-qualify mtu kuwa blacklisted. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii vile vile tumekuwa na changamoto ya utoaji wa fedha kutoka kwenye benki zetu. Huko tulipotoka makampuni makubwa yalikuwa yanasema benki za ndani ya Tanzania haziwezi ku-finace miradi ya uchimbaji madini. Nataka nitoe taarifa kwako na ndio maana tuliwaalika watu wa CRDB na NMB, hivi leo mradi uliokuwa umekwama kwa miaka mingi kotokana na corona, wawekezaji wamekwenda ku-list huko nje kutatufa finance wamekosa, wameamua kurudi kwenye benki za ndani na sisi tukawaita ili tuweze kuzungumza nao na Mheshimiwa Waziri Mkuu akaweka mkono wake wa kutusaidia kuzungumza na benki hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafurahi kusema kwamba mradi mmoja wapo mkubwa wa uchimbaji wa graphite hapa nchini wa Ruangwa huko Lindi Jumbo tayari CRDB wametoa fedha zote za kuendesha huo mradi. GGM wana mkopo wanapewa na Benki ya NMB zaidi ya bilioni 250, uwezo huo uko ndani. Sisi tunachowaambia mabenki inawezekana huna fedha zote za ku-finance hii miradi, tufanye synergy ya benki mbili au tatu. Mbona kwenye miradi mingine wanatuletea, unakuta Exim ya China imeungana na Barclays ya London wamefanya synergy wana-finance mradi uko Tanzania na mabenki yetu yanaweza kufanya hivyo na hilo wametuelewa, sasa miradi mingi inatolewa fedha hapa ndani.
Mheshimiwa Spika, hata wachimbaji wadogo wengi ningekuwa na muda ningekuletea orodha ya wachimbaji wadogo waliokopeshwa na mabenki ya ndani. Jambo hili mabenki wametupa heshima kubwa kwasababu wameona trust iko kwenye madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho najua kwasababu ya muda yako mambo mengine ni ya kiusimamizi mdogo wangu Mheshimiwa Maganga la Nyakafuru Pamoja na loyalty kwamba ukiweka tu milioni 100 tunakata hapana sheria haiku hivyo. Loyalty utalipa baada ya kuwa umevuna lakini hatuwezi kukata kodi kwenye mtaji tukifanya hivyo tutakuwa tunamuibia Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, na hilo la Nyakafuru tutakwenda lina hadithi zake ndefu Mheshimwa Mkuu wa Mkoa aliunda kamati, kamati imeshatoa majibu alilieleza wakati tuko kwenye ziara na nimemhakikishia kwamba hakuna mtanzania hata mmoja atadhulumiwa wala hakuna mtanzania hata mmoja ataonewa.
Mheshimiwa Spika, lakini la kweli tuchukue muda mwingi kuwaeleza watanzania ukweli kuna drama nyingine watu wanafanya ambazo ukweli ukienda kwenye detail unakuwa wao wanatudanganya viongozi na tunachukua maamuzi ya kuumiza wawekezaji bila sababu ya msingi. Wawekezaji wakubwa tunawahitaji jamani kwenye uchimbaji madini tunahitajiana wote wachimbaji wadogo tunawahitaji, wachimbaji wa kati tunawahitaji na wachimbaji wakubwa tunawahitaji akitokea mmoja katika group hizi akapata matatizo basi tunakuwa na fallback position tukiwaondoa wachimbaji wakubwa kwa kisingizio cha wachimbaji wadogo, mwisho wa siku hatuwezi kukuza hii sekta.
Mheshimiwa Spika, leo tunafurahi tunasema kwamba uchimbaji mdogo na wachimbaji wadogo wamechangia kwenye pato la Taifa kwenye ile gross asilimia 30. Tulikotoka wachimbaji wadogo hawakuwa na maana walikuwa wanachangia chini ya asilimia tano hatua hiyo tumeifikia kwasababu tumewapa heshima lakini heshima hiyo tunayowapa wachimbaji wadogo isigeuke kuwa fimbo ya kuwaumiza wachimbaji wakubwa na wa kati ambao nao wanaweka fedha zao tuheshimiane hatuwezi kutumia kigezo cha uchimbaji mdogo na uchimbaji mdogo
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Waziri malizia.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie uchimbaji mdogo ni hadhi ya muda mfupi haiwezekani mchimbaji mdogo yeye ha-graduate mtoto anasoma darasa la kwanza yeye ni mdogo mdogo lakini ukienda kuangalia finance zake na vitabu vyake ana mtaji mkubwa lazima tuwafundishe Watoto kuona Fahari kuitwa wachimbaji wakubwa ili uchimbaji wa ndani uwe wa kwetu naomba nikushukuru sana. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa tafadhali nisaidie suala la Nyanzaga likoje.
SPIKA: Ameshamaliza hapana hapana hamna taarifa vurugu hiyo hapana Mheshimiwa. Mheshimiwa Waziri huja toa hoja
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha naomba sasa Bunge lako likubali kujadili na kupitisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2021 naomba kutoa hoja.