Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Omar Ali Omar

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa fursa hii ya kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na cabinet yake kwa kutuletea Bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba katika askari ambao wanastahili kupongezwa ni Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa sana nchini kwetu. Lakini Jeshi la Polisi linafanya kazi katika mazingira magumu mno. Jeshi la Polisi toka mwaka wa 2015 hawajapata nyongeza ya mishahara; Jeshi la Polisi halijapata increment; halijapata kupandishwa vyeo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani, hongera sana; huyo ni Mbunge wa ACT – Wazalendo.

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, lakini kwa kweli kwa masikitiko makubwa, tena makubwa mno, ukienda hata majengo wanayokaa askari polisi ni majengo ambayo hayastahiki. Kwa mfano Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo natoka mimi, Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba hata nyumba ya kukaa hana. Mpaka sasa hivi tunavyoongea hana nyumba ya kukaa kwasababu ya kwamba nyumba ile imekuwa mbovu kabisa, hawezi kuishi. Kwa hiyo, hii ni kuonesha kwamba Jeshi la Polisi hatujalipa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna nyumba za maafisa ambazo zimejengwa kule Finya, Mkoa wa kaskazini Pemba, mpaka sasa hivi nyumba zile hazijamalizwa. Hata Naibu Waziri aliwahi kufika katika eneo lile na akaona majengo yale hali halisi yalivyo na akashindwa kushughulikia lile suala mpaka leo hii. Kwa hiyo, tunataka sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, je, nyumba ile itamalizwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukitoka maeneo hayo, Ofisi ya Polisi ya Mkoa wa Kaskazini Pemba haikaliki, inavuja kama pakacha. Kwa kweli inasikitisha sana, kuna vyumba ambavyo ndani ya ofisi ile hawafanyi kazi tena askari polisi kwasababu vimekuwa vichakavu na kwasababu ofisi inavuja sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwenyewe binafsi tarehe 1 Machi nilifika katika Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba na kujionea kwa macho yangu kwamba lile eneo liko katika hali ya hatari. Jengo liko hatarini, toka mwaka wa 1970 mpaka kaja kalifungua Mheshimiwa Hayati Moringe Sokoine mwaka 1979, jengo lile mpaka leo halijafanyiwa ukarabati wa aina yoyote. Hii ni kuonesha kwamba askari wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo, hilo tuliangalie.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama wanavyosema Waswahili, kidonda kikioza sana basi hata nzi hakitaki. Hii ni kuonesha kwamba hata lile jengo lenyewe la polisi, Kamanda wa Polisi hana hata pa kuishi, kwa kweli hili ni jambo la kusikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika eneo lingine la askari polisi; Kisiwa cha Pemba kina bandari bubu16. Kutokana na muda itaweza kuzitaja, lakini Pemba ina bandari bubu 16. Kwa hiyo, hizi bandari bubu ndiyo bandari ambazo zinatuhatarishia amani katika Kisiwa cha Zanzibar. Kwasababu kama tunavyojua kwamba mipaka yetu inahitaji kulindwa na askari polisi ni moja katika jamii ambao wanastahiki kulinda mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu hayo makubwa lakini askari polisi hawana vitendea kazi. Mkoa mzima wa Kaskazini Pemba una gari moja tu la Kamanda wa Polisi, magari yote yamelala, kwa sababu ya ukosefu wa vipuri, mafuta na upungufu pia wa askari. Kwa taarifa tu Mheshimiwa Maida alinifilisi kidogo lakini napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Kaskazini pekee una mahitaji ya askari 150 na hii ni kutonana na kwamba kumetokea mambo mengi; askari wameumwa, wengine wamestaafu na wengine wamefukuzwa kazi. Kwa hiyo, kutokana na hali hiyo ya ukosefu wa askari, bandari hizi bubu ndizo ambazo zinatumika katika kuingiza uharamia wa kila aina ikiwemo madawa ya kulevya. Kule Zanzibar mahakama zetu zina kesi nyingi ambazo zinahusiana na madawa ya kulevya. Hii ni kuonesha kwamba maeneo ambayo yanatumika kupitisha madawa ya kulevya ni bandari bubu na idadi ndogo ya askari ambao tunao katika vituo vya polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kusikitisha sana Kamanda ana dhamana ya kuwalisha mahabusu badala ya dhamana ile kuwa ya Serikali. Kwa kweli wanapata misaada kutoka kwa wasamaria wema, wenyewe wanawaita wafanyabiashara werevu wanaojua athari…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Omar Ali Omar, dakika tano ni chache, lakini nakushukuru sana.

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, lakini mngetuongeza tuko wachache. (Makofi)