Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Rashid Abdalla Rashid

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia Wizara yetu hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Napenda sana kumpongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wao kwa ujumla kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutengeneza bajeti hii na hadi kuikamilisha kuileta ndani ya Bunge letu hili Tukufu kwa ajili ya kujadiliwa. Lazima tuthamini nguvu zao, jitihada zao kwa sababu sote tunajua kwamba utayarishaji wa bajeti ya Wizara kama hii unahitaji umakini wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika michango yangu katika Jeshi la Polisi na muda ukiruhusu nitaingia katika idara yetu ya Uhamiaji. Naomba Mheshimiwa Waziri akubali kwamba, Wizara hii kwa maana ya Jeshi la Polisi kwenye Wilaya ya Mkoani ilichukua zaidi ya miaka 20; lilikosa utetezi. Nasema kwamba jeshi hili lilikosa utetezi kwa sababu, majengo yote ya vituo vya Polisi pamoja na Makao Makuu ya Wilaya, basi kimsingi majengo haya hayakubaliki kufanya kazi yakitumika kama ni majengo ya ofisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukianza na Kituo cha Polisi Kengeja hiki kimeoza kabisa na hakifai. Hata Kituo cha Polisi Mtambile nacho kadhalika, hakifai. Tukija kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Polisi Mkoani, hii ndiyo kabisa hayafai kabisa. Kwa sababu, majengo haya yalijengwa kabla ya uhuru. Ni majengo yaliyokuwa yakitumika na Masultani kwa kule Zanzibar. Sasa nilisema yamekosa utetezi kwa sababu majengo haya yalikosa watu wa kuwatetea kwa sababu majimbo hayakuwepo kwenye watu ambao ni makini kwa ajili ya kutetea Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi lilikuwa linaonekana kama ni maadui, kwa hiyo, hata makazi yao yalikuwa yanaonekana vile vile ni ya kiadui adui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvua sasa zinaendelea kunyesha katika Wilaya ya Mkoani, tena ni mvua kubwa, ofisi hazikaliki, zinavuja. Hapa niliposema kwamba walikuwa na kazi kubwa ya kufanya bajeti ya Wizara, ni kwa sababu walikosa hadidurejea ya kuangalia kwamba bajeti iliyopita kulikuwa na makosa gani? Kulikuwa na mahitaji gani katika Wilaya ya Mkoani? Ndiyo maana hapa Mheshimiwa Waziri katuambia kwamba atajenga nyumba 14 katika Mkoa wa Kusini Pemba, lakini kama angekuwa na hadidurejea za bajeti iliyopita, nadhani angelielekeza kwenye ujenzi wa angalau ile ofisi ya Wilaya ya Mkoani badala ya nyumba 14 kwenye Mkoa wa Kusini Pemba.

Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Waziri ni mtu mmoja mkakamavu, makini sana, kwa sababu katika Wizara ambayo alikuwepo aliwahi kufanya ziara ya kuja kukagua mambo mbalimbali ambapo naamini alipotoshwa, lakini alipokuja na akaupata ukweli, mambo yakaenda vizuri. Sasa hapa nayeeleza haya siyo kwa upotoshaji. Nayaeleza ili aandae ziara na nitaomba tuambatane pamoja twende katika Kituo cha Polisi Kengeja, Kituo cha Polisi Mtambile na Makao Makuu ya Wilaya ya Polisi Mkoani, tuone hali zao zilivyo, wanatia Imani. Hili wakati mwingine linasababisha hata ufanyaji kazi unakuwa ni wa kudorora dorora.

Mheshimiwa Spika, mwezi mmoja uliopita, Makamu wa Pili wa Rais alifanya ziara kwenye Wilaya ya Mkoani, akataka kujua kuna kesi ngapi ziko Mahakamani, ngapi ziko Polisi na ngapi ziko DPP, lakini jibu lililotoka pale ni kwamba kuna kesi 21 bado ziko Polisi zikiwa na miezi tisa zinasubiri ushahidi. Kuna ushahidi mwingine hauhitaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Abdalla Rashid Abdalla. (Kicheko)

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Haya. (Kicheko)

SPIKA: Ndiyo ubaya wa dakika tano. (Kicheko)

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, nitamwasilishia kwa maandishi na ninaunga mkono hoja...