Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba nianze kwa kumuuliza swali Waziri wa Viwanda na Biashara. Waziri wa Viwanda na Biashara nataka ulijibu Bunge letu, unataka kujenga viwanda vya nini? Focus yetu ni viwanda gani? Maana unapotaka kujenga viwanda, ukisema unataka kila kitu niweke kiwanda tumeanza na kushindwa. Nilidhani umefika wakati tuamue focus yetu iwe kwenye maeneo ambayo tuna comparative advantage. Ukiniambia leo tunaweza tukashindana na China, India na nchi zile ambazo zimefanya vizuri tutapata tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, atuambie kwa hali ya dunia inavyokwenda, Tanzania tunaweza tukaanza na viwanda vya namna gani. Ukienda leo pale Silcon wameanzisha teknolojia lakini wana invest kwa ajili ya teknolojia hii, wanafanya research, wameandaa mazingira kwa ajili ya viwanda vya teknolojia. Ukienda Auto Mobile duniani inajulikana, siyo wote wana Auto Mobile. Ninachouliza kama Tanzania tunatakiwa twende kwenye viwanda vya namna gani? Mimi nimesoma hapa, ukiangalia mwanzo mpaka mwisho sioni tunakwenda kwenye viwanda vipi, yaani focus yetu ni nini. Tusipokuwa na focus tutarudi kule kule tulikotoka miaka ya nyuma. Ndiyo maana unasema leo mara unataka uanzishe hiki, uanzishe hiki, hatuwezi kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niulize, maana yako mambo ambayo tusipoyaweka sawa tutakuja kushindwa huko baadaye. Mimi nasema kama nchi tunge-concentrate kwenye viwanda vya agro-industries kwa sababu tuna malighafi. Leo tukiamua kama nchi, maeneo manne tu tufanye kweli kweli, mfano Kiwanda cha Mbolea, kiwanda kikubwa ambacho tuna uhakika tutazalisha mbolea ambayo itatumika Sub-Sahara Africa, tutapata fedha nyingi sana kama nchi na tuta-save dola nyingi sana za ku-import mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili, ni viwanda vya sukari, hizi kelele hizi ni kwa sababu hatujaamua ku-invest kwenye viwanda vya sukari. Tukiamua ku-invest kwenye viwanda vya sukari Tanzania tuna hekta karibu milioni nne unazoweza kufanya irrigation, tunaweza kuzalisha karibu tani milioni mbili za sukari, tutatumia ndani na nyingine tutauza nje na tutafaidisha sana wakulima wetu ambao wako kwenye hayo maeneo. Namba tatu, mafuta ya kula, tuna michikichi, tuna alizeti, tu-concentrate hapo kwa kuanzia. Namba nne ni leather industry kwa sababu tuna mifugo mingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akija hapa anasema kila mtu atajenga kiwanda awe na uhakika atashindwa, kwa sababu viwanda vinahitaji Serikali tuungane, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Nishati na Madini lazima wote tuongee lugha inayofanana. Ukisoma vitabu hapa, ukasoma Mpango, lugha haifanani. Sasa tunataka kujenga viwanda gani? Imefika wakati lazima tuambiane, tunawaunga mkono lakini lazima kuwe na coordination unity ambayo inawaunganisha tujue direction ya namna moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha anataka kukusanya kodi, lakini kuna wakati lazima tutumie kodi kutoa incentive ili viwanda viweze kujengwa. Ili viwanda viweze kujengwa wenzetu wamefanya research, kuna mambo lazima tuhangaike nayo, lazima uangalie micro-stability ya nchi. Micro-stability yetu inasemaje? Kama huangalii hili investor haleti fedha zake! Lazima uangalie skills and education, hapa kwako mambo ya elimu yakoje? Lazima uangalie infrastructure kwa maana ya umeme, maji na transport system. Lazima uangalie teknolojia, hali ya innovation na teknolojia wewe unafanyaje, kwako pakoje?
Mheshimiwa Naibu Spika, njia ya kupata teknolojia ziko njia tatu, moja kutoka nje, mbili through FDI, tatu research and development ili kupata teknolojia ambazo ni locally made. Kama viwanda tutasema tu tutarudi kule tulikotoka na nina hakika hatutoweza kufanikiwa. Tukiamua kuungana tukajiweka kwenye viwanda ambavyo malighafi tunazo Tanzania ambazo ni agriculture tutabadilisha maisha ya watu wetu vijijini na nchi hii itaweza kupata fedha nyingi za kigeni na tutaweza kwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ni Waziri wa Viwanda na Biashara, hali yetu ya biashara ni mbaya. Ukiangalia cost of doing business in Tanzania, kwa ripoti ya World Bank ya 2016 tuna rank ya 139 katika nchi 189, hili siyo jambo jema. Kwa hiyo, lazima Waziri wa Viwanda na Biashara ufanye kazi ya kufanya biashara zikue Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi wamesisitiza kuhakikisha tunaanzisha Bodi ya Kusaidia biashara ndogo ndogo (SMES) wala sioni ukieleza thoroughly, kwa sababu hiyo ndiyo itakayowaokoa hawa wafanyabiashara wadogo wadogo, wataajiri watu wengi, tutapata kodi nyingi sana. Kama haturasimishi biashara tunalo tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitamwambia Mheshimiwa Waziri kwa mfano, wanasema ukitaka kuanza biashara Tanzania sisi tunachukua nafasi ya 129 katika nafasi 189, ukitaka kupata construction permit tunakuwa wa 126, kupata umeme wa 83, ku-register property wa 133, kupata credit wa 152, kuwalinda minority investors wa 122, kulipa tax wa 150, trading across borders wa 180 kati ya 189, enforcing contract wa 64 na resolving insolvency sisi ni wa 99. Waziri wa Viwanda na Biashara lazima uhangaike kuhakikisha unajenga mazingira ya biashara kukua Tanzania. Tusipojenga mazingira ya biashara kukua Tanzania maana yake ni moja tu, hata hivyo viwanda tunavyoviongea havitapatikana, wawekezaji hawatapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasema Waziri anaposhughulika na suala la viwanda na biashara lazima ajue analo jukumu la kuhakikisha biashara inaenda vizuri isidumae. Ili isidumae lazima uondoe hizi bottlenecks! Tanzania tumeumbwa tuna nchi karibu nane zinatuzunguka, hii ni advantage kwetu kiuchumi, je, tunaitumiaje? Lazima mipango yetu iende towards kwenye kuleta biashara na siyo tu biashara hata kufanya biashara Tanzania isiwe tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waziri wa Viwanda ukae na Waziri wa Fedha, concentration yetu isiwe kukusanya kodi tu, lazima tutumie kodi kukuza uchumi. Unakuza uchumi kwa wafanyabiashara, kwa kuweka mazingira ya watu kuleta fedha zao kwako na hatuwezi kuamini kwamba tunaweza tukaleta mageuzi ya viwanda kwa kutumia fedha za bajeti, haiwezekani! Tukidhani unaweza ukatumia fedha za bajeti mjue tunaelekea kwenye kushindwa. Ili mwenye fedha zake aje, asiende Mozambique, Kenya, Rwanda lazima uweke mazingira ya kumkaribisha aone kwamba Tanzania nikienda nitapata zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumehangaika kule Kigoma, Wahindi wanataka kuleta Kiwanda cha Sukari, wamezungushwa mambo ya ardhi karibu sijui miaka mingapi, inawezekanaje? Huku tuna matatizo ya sukari in the country, kuna mtu anataka kuja kuweka kiwanda anazungushwa tu. Lazima haya Waziri wa Viwanda uhangaike nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba Serikali iunde committee ambayo itahusisha watu wa Wizara ya Fedha na Mipango; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Viwanda, Biashara na Uwekezaji; na Nishati na Madini, ili mkikaa muwe mnajua hali inavyokwenda nchini kwa maana ya kuhakikisha mnaondoa bottleneck za biashara nchini ili watu waweze ku-invest Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema Waziri nakuunga mkono, lakini nasema ukisoma mipango yako naona unataka kuanzisha kiwanda everywhere as if viwanda ni jambo rahisi, suala la viwanda siyo rahisi kama tunavyotaka kuiweka, unaweza ukaweka viwanda kesho vyote vikafa. Ndiyo leo unataka kufufua General Tyre, is it our priority? Huo mpira wenyewe umeanza kuulima? Maana unaweka bajeti leo kwa ajili ya General Tyre shamba hujaanza kulima, je, hayo matairi yako yanaweza yaka-compete kwenye biashara nyingine duniani, unaweza u-compete na wengine? Ukiangalia cost zako unaweza uka-make money ama tunataka kurudisha General Tyre out of prestige kwamba na sisi tumefufua, prestige! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara jamani ni economics tuache kuchanganya siasa, biashara na viwanda. Suala la viwanda na biashara, tukachanganya na siasa, nina hakika, hatutakwenda tunakotaka kwenda. Nakuamini Waziri, Serikali ina nia njema, lakini kaeni muwe more focused, tuanze vile tunavyoviweza ambavyo raw materials zake ziko Tanzania na tukizalisha vizuri tutaweza kuuza angalau regionally kabla hatujaenda huko nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru.