Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nianze pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa kwanza mwanamke kwa asilimia 100 ndani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa narejea mbalimbali za viongozi kuhusiana na mjadala unaoendelea wa Wizara ya Elimu, nianze na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake ya kwanza akiwa Chamwino anaapisha viongozi alizungumzia juu ya mabadiliko ya elimu hasa elimu ya ujuzi, lakini pia tukiwa Chimwanga kwenye maombi maalum ya Hayati Mpendwa wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mipango yake ama vipaumbele vyake 18 kipaumbele cha tano kilikuwa ni cha elimu na ni elimu ya ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini akiwa anahutubia Bunge pia, alizungumzia mabadiliko ya mtaala na mtaala huu huzungumzia hasa kwenye ujuzi, narejea pia katika rasimu ya Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano wakati tunafanya majadala hapa ukurasa wa 25 ilitolewa taarifa ya Tume ya Mipango, Tume ambayo ilionesha kabisa soko la ajira. Soko la ajira haliendani na elimu ya ujuzi inayotolewa sasa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nimshukuru Waziri wa Fedha alitusikiliza na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano amekuja ameeleza vizuri katika mambo manne ambayo Wizara ya Elimu inapaswa kuyatekeleza, moja ilikuwa Sayansi, Teknolojia na ubunifu kwa maana ya SATU. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na nimemsikiliza Waziri vizuri kwenye hotuba yake nimpongeze sana hapa Waziri ameeleza pia na wao kwenye eneo la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu amelieleza vizuri. Lakini kuna eneo ambalo tunahitaji tulieleze vizuri. Katika maelezo yake amesema wale walioshinda ubunifu ndio watawaendeleza, lakini pia ameeleza wataendelea na mashindano kwa watu watakaokuwa wanashinda wataendeleza mashindano na wale watakaoshinda ubunifu ndio wataendeleza.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu hapa ubunifu tunaouzungumza, teknolojia tunayoizungumza sayansi hii tunayoizungumza tunapaswa kwenda mbali zaidi twende tukauhishe vyuo vyetu vya ufundi badala ya kuhangaika na walioshinda. Leo tunayo Tanga Technical, Arusha Technical, tuna Moshi Technical, vyote hivi ukienda kuangalia mazingira yao haifanani kama ilivyo FTC zamani, wakati tunazalisha tunatafuta wazalishaji leo tumeenda ku-transform tumeweka watu wa kusimamia, wasimamizi administrates. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nataka nimuomba Mheshimiwa Waziri wakati anapokuja kueleza vizuri kwenye eneo hili la kuhakikisha tunatekeleza Mpango huu wa Serikali tusibaki na watu walioshinda kuwa wabunifu, twende kuboresha vyuo vyetu tutenge bajeti ili vyuo vyetu hivi viweze kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipo Chuo cha Nelson Mandela ameeleza vizuri hapa Mheshimiwa Waziri na kimetengewa fedha na hizi fedha sio za kwetu za wafadhili zaidi ya bilioni 3.2 nataka niseme jambo hapa hakuna donor ambaye anakuletea fedha ya kufanya utafiti hajakuwekea masharti maana yake atataka ufanya utafiti kwa kile ambacho anataka yeye. Lakini Je, sisi Watanzania tunataka nini, nilitaka Serikali ijielekeze kwa kile tunachokitaka sisi, Chuo cha Nelson Mandela nakumbuka mwaka 2001 Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi za Afrika ulipokaa ulijadiliana namna gani tunakabiliana na teknolojia tuliyonayo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Nelson Mandela na Mkutano huu ninakumbuka uliudhuriwa na Rais wa World Bank wa wakati huo Dkt. James David Worson ambaye ushauri ulitoka vianzishwe vyuo vinne Afrika moja ya chuo kilichojengwa ni Burkina Faso kingine kilijengwa Nigeria na hichi cha tatu kimejengwa Tanzania Arusha-Nelson Mandela Institute cha nne nadhani kitajengwa Zimbabwe. Sasa Serikali yetu na hapa nimshukuru Rais wa Awamu nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa fedha Dola milioni 60 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya chuo cha Nelson Mandela. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, alifanya kazi nzuri sana leo tunazungumza Chuo cha Nelson Mandela kinapata fedha za wafadhili, wafadhili ambao wao wametoa masharti yao ya tafiti wanazozitaka wao yawezekana kwetu sisi zikawa sizo tunazozitaka kwa hali tuliyonayo sasa hivi, nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri sisi lazima pia tuweke mkono wetu tutoe fedha kwa ajili ya kufanya tafiti zitakazotusaidia tuendane na haya maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais ameyatoa lakini na Mpango wetu wa Maendeleo. Kwenye eneo hili litakuwa limetusaidia kupata wataalam wengi wenye utaalam lakini tutakuwa tumepata ubunifu mwingi ambao tutaweze kuusimamia na kuhakikisha watoto wetu wanaweza kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapotaka kuwa na wazalishaji, sisi tumekwenda mbali zaidi tumegeuza maana yake sasa hivi unawazungumzia hawa wa full technician na wengine hawa wa graduate engineers huwezi kumfananisha full technician wa wakati ule na graduate engineer wa leo wala hatujachelewa, hatujachelewa kama China wameweza kuondoa vyuo vyao 600 vyuo vikuu kwenda kuwa vyuo vya Elimu ya Kati sisi hatuwezi kuchelewa tunapaswa na sisi tutafakari kwamba umefika wakati tuimarishe vyuo vyetu vya kati ili kupata wazalishaji wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuna eneo moja hapa muhimu sana competence basic education, nakumbuka tunapozungumzia competence basic education elimu ya maarifa, elimu ya maarifa leo tunazungumzia academic tunazungumzia teaching and learning. Amesema vizuri Mheshimiwa Mpina pale huku nyuma tulikuwa na watu, mtoto anaweza anajifunza kilimo, anajifunza biashara anajifunza vitu vingi sana lakini leo hakuna kwasababu tupo kwenye msingi wa education tu peke yake kwa maana watoto wana ujifunzaji lakini watoto hawana ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nishauri hapa badala ya kuwa na masomo mengi ni lazima tuweke somo la lazima kama somo la Kilimo lianzie darasa la kwanza mpaka chuo kikuu, asome michepuo yake yote lakini awe anasoma badala ya kubaki tu unafundisha mtoto development study what does it mean development study maana yake lazima ajue kabisa anasoma package ya agriculture ambayo ime-compose vitu vingine vyote vilivyopo ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nataka nishauri Serikali, ushauri wangu wa kwanza kamati imeeleza vizuri lazima tuwe na mjadala mpana wa elimu ambao utawahusisha watu wote na kada mbalimbali ili tujue elimu tunayoitaka sisi ipi. Lakini jambo langu moja la msingi tunapaswa kuwa na Baraza la Taifa la Elimu, Baraza la Taifa la Elimu ndilo litakalokuwa linamshauri Waziri, litakalokuwa linamshauri Rais lakini ndilo litakalosimamia elimu kwa ujumla, hii ndio itakuwa ambarella kubwa. Lakini tuna NACTE na TCU hapa tumevigawa vyuo NACTE wanavyuo vikuu TCU wana vyuo vikuu hizi regulator zote mbili zinatuchanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanini tusiwe na regulator moja inayosimamia elimu ya juu yaani tunazungumzia kama TCU wasimamie Universities wabaki kusimamia Universities kwa ajili ya degree lakini kama NACTE wanasimamia vyuo vya kati wabaki kusimamia vyuo vya kati. Lakini suluhu ya haya yote maana yake msingi wake lazima tuwe na Baraza la Taifa la Elimu litakalotufikisha mahali sisi tunapokutaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajengewa shule za kata kwa kata ambazo hazina shule kama shule 300 kwa malengo kuanzia mwaka huu, lakini tutafakari kwa wote shule 300. Nina kata moja tu Mandewe ina shule za msingi saba watoto wanaomaliza pale hawapungui 600 wa kwenda kidato cha kwanza sasa unajiuliza shule moja ya kata niliyonayo ukajenga nyingine kwenye kata ambayo haina maana yake hawa watoto 700 unakwenda kuwaweka, maana shule nzima ni form one peke yake hakuna uwezekano mwingine.
Mheshimiwa Spika, nilitaka niishauri Serikali katika Mpango huu, huu Mpango uishirikishe jamii, jamii ishiriki na yenyewe badala ya shule moja tunaweza kujenga shule mbili mpaka tatu na kuendelea ili kukabiliana na tatizo ambalo tulilonalo na Watoto wengi wanakwenda shule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nikushukuru sana wewe kwa namna ambavyo umeniweka kwenye Kamati hii ya huduma za jamii umenisaidia sana nimalizie pia kuwatakia kila la kheri wale wote ambao wamegombea nafasi hizi kwenye Bunge letu hili nikiwemo na mimi Mussa Sima, ninawashukuru sana na Mungu awabariki. (Makofi)