Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalamu wote kwa hotuba nzuri lakini kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Wizara kwa maana ya uboreshaji wa miundombinu. Tumeona madarasa mengi yakijengwa, vyuo vya ualimu vikikarabatiwa, shule kongwe zikikarabatiwa; kwa kweli kwenye upande wa miundombinu mmefanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri ya kuboresha miundombinu bado kuna matatizo makubwa mawili ambayo nitayaongelea. Kwanza, shule zimepanuka au zimeongezeka, wanafunzi wameongezeka mara dufu lakini walimu wameendelea kuwa wachache. Nataka niwahahakishie mimi kama mwalimu kwamba kwenye setting yoyote ya elimu mwalimu ni central, hata ukiwachukua wanafunzi ukaweka chini ya mti lakini ukamuweka mwalimu ambaye ana ujuzi uliokamilika yule mtoto ataelimika. Ukimchukua mwanafunzi ukamuwekea madarasa na vitabu ukamuondoa mwalimu hakuna kitu chochote kitakachoweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inasikitisha kuona kwamba mwanafunzi anamaliza form four kutoka kwenye shule A ana division one na division two, division three anachaguliwa kwenda high school anapelekewa kwenye shule, labda anaenda kusomea tahasusi ya PCB (Physics, Chemistry na Biology) anakuta kuna mwalimu mmoja wa Biology anasoma somo moja kwa miaka yote miwili form five na six at the end of the story mtihani anapewa ule ule kama aliyekuwa na walimu katika masomo yote matatu na mwisho anaambiwa kwamba ameshindwa kwa sababu atakuwa ameshinda somo moja tu. Huyu mtoto hawezi kwenda chuo kikuu, hawezi kwenda mahali popote anakuwa ameharibiwa maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napendekeza kwamba Serikali sasa ingeweka mkakati wa makusudi kuhakikisha kwamba wanaajiri walimu. Nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan juzi ametangaza kwamba sasa angalau tuanze na kuziba zile nafasi zile 6,000 kwa wale waliotoka kwenye ualimu kwa maana ya kustaafu au kuwa kuacha kazi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba katika mazingira hayo wanapokwenda kuajiri hao walimu 6,000 waungalie Mkoa wa Kagera; hadi sasa tuna upungufu wa walimu 7,607 katika shule za msingi na tuna upungufu wa walimu 1,340 katika shule za sekondari. Huo ni mkoa mmoja, je, Taifa zima ikoje? Kwa hiyo, napendekeza kwamba kuwe na mkakati wa makusudi, vibali vitolewe, walimu waajiriwe ili wanafunzi waweze kuipata elimu tarajiwa.

Mheshimiwa Spika, tatizo la pili, kuna malalamiko makubwa sana juu ya elimu itolewayo kwamba haikidhi matarajio ya wanaoipata. Utawakuta wasomi wanalalamika, waajiri wanalalamika kwamba wanafunzi wanaowapata hawana zile stadi zinazohitajika katika viwanda na makampuni yao. Pia wahitimu na wenyewe wanalalamika kwamba elimu waliyoipata haiwapi ajira na wala haiwawezeshi kuweza kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, napendekeza kwamba labda tungejifunza kutoka kwenye nchi ya China. China kwenye miaka 1970 walikuwa wanafahamika kwamba ni nchi maskini duniani, lakini wakagundua kwamba ili waweze kutoka kwenye huo mkwamo lazima waboreshe elimu yao. Wakafumua mfumo wao wa elimu, sasa hivi China ni ya viwanda, it’s a second largest economy in the world, vilevile ni wazalishaji wa mali mbalimbali ambazo zinasambazwa kote duniani. Hii ni kwa sababu waligundua kwamba elimu watakayokuwa nayo ni lazima iwe ni elimu ambayo inakuza ujuzi. Ili tufikie kwenye Tanzania ya viwanda lazima tubadilike, tutoke kwenye hii kufundisha general academic knowledge twende kufundisha elimu ambayo inakuza ajira na ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, China wao walirekebisha sheria zao za elimu, lakini kilichowafanya wafumue mfumo wao wa elimu ni walipogundua kwamba wanahitaji skilled labor ya kuweza kufanya kazi kwenye viwanda wakakuta kwamba huo utaalamu hawana. Tangu wabadilishe mfumo wao uchumi ukakua na kama mnavyojua sasa hivi uchumi wa China unakua kwa asilimia 10 kila mwaka, kwa hiyo wana uchumi mkubwa duniani. Serikali ikaweka fedha nyingi katika elimu, wakafanya reforms mbalimbali na wakaweza kufikia hapa walipofikia.

Mheshimiwa Spika, kitu cha kwanza walichofanya wakahakikisha kwamba elimu msingi ambayo inaenda mpaka sekondari ikawa compulsory (ni ya lazima). La pili, wakarekebisha mitaala. Mitaala yao sasa hivi 1/3 ya mtaala ndiyo inafundisha general academic knowledge, 1/3 ya mtaala wa China, elimu kuhusu fani mbalimbali zinazohitajika katika Maisha lakini 1/3 lazima huyu mtoto ajifunze kazi mojawapo ambayo inapatikana katika Serikali yake ya Mtaa kwa sababu wanategemea kwamba ataenda kuajiriwa kule. Vilevile wameanzisha kozi mbalimbali ili kufikia mahitaji ya viwanda. Kuna mahusiano na mikataba inawekwa kati ya shule na viwanda kila mwisho wa term wanafunzi wanaenda kwenye viwanda kusudi waweze kunoa ule ujuzi wao na wanafunzi kutoka kwenye familia masikini walikuwa wanalipiwa karo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, elimu ya kukuza ujuzi wanaianza mapema kabisa wakiwa kwenye junior secondary school ambapo sasa si watoto wameshapata ujuzi huu, wanapomaliza junior secondary school ambayo iko kama kwenye form two hapa wao asilimia 11.6 wanaenda moja kwa moja kwenye ajira kwa sababu tayari wana ujuzi, wanaweza kuajiriwa sehemu mbalimbali. Asilimia 88.4 hawa wanaendelea na senior secondary school lakini kati ya wale walioenda kwenye senior secondary school asilimia 47 wote wanaenda kwenye VETA na vyuo vya ufundi kusudi sasa waweze kupata ujuzi ambao unahitajika. Mwisho wa muhula wanafunzi wanaenda kwenye viwanda lakini kabla ya graduation kila mwanafunzi lazima apite kwenye internship kama tunavyoona hapa madaktari wanafanya.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa upande wa walimu ili uweze kufundisha kwenye secondary lazima uwe na angalau degree moja. Sisi hapa tunapeleka division three na there was a time tulikuwa tunapeleka hata division four. China wanapeleka wale cream ndiyo waweze kuwa walimu waje wawafundishe Watoto vizuri.

Mheshimiwa Spika, wakati wa likizo walimu lazima waende viwandani, wawasiliane na wenye viwanda na wenye makampuni wajue, je, wanachofundisha darasani ndiyo kinachohitajika? Aidha, walimu ambao wako kwenye vyuo vya ufundi ni lazima kila mwaka aende kukaa kiwandani kwa muda wa mwezi mmoja akiwa ananoa skills zake. Ili mwalimu apande cheo kama tunavyoona kwa mapolisi lazima kwanza afanye practical training kwenye kiwanda. Kama tunavyoona polisi lazima asomee vyeo na wao wanaenda wanafundishwa ndiyo wanaweza kupanda vyeo.

Mheshimiwa Spika, mwisho wanawa-expose hawawafungii, wanaenda kwenye nchi mbalimbali wanajifunza best practices halafu wakija wanaboresha mfumo wao wa elimu. Pamoja na kozo ndefu lakini wana kozi fupi za kumnoa mtu. Sisi hapa mtu akiajiriwa mpaka astaafu hajawahi kwenda kwenye kozi nyingine. Kwa hiyo, anafundisha hata elimu ambayo imepitwa na wakati, wao wana re-training, on job training na kadhalika. Ndugu zangu nasisitiza elimu ya ujasiriamali kwa China ni lazima. Kwa hiyo, nafikiri tukiiga mfano huu tunaweza tukaboresha elimu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba Wizara ya Eilimu na wote wanaohusika na mambo ya elimu wakubali kwamba kuna tatizo kwenye mfumo wetu wa elimu. Wafungue mjadala mpana kusudi Serikali, waajiri kwa maana ya makampuni na viwanda, wasomi pamoja na watunga sheria kwa maana ya Bunge tujadili tuangalie mfumo wetu kuna tatizo wapi? Kitu gani kinakosekana na tuongeze nini hiyo ndiyo itaweza kutupeleka kwenye dira yetu ya uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)